SoC01 Umewahi kujiuliza Ubongo wa binadamu una ukubwa wa GIGABYTES (GB) ngapi? Fuatilia

SoC01 Umewahi kujiuliza Ubongo wa binadamu una ukubwa wa GIGABYTES (GB) ngapi? Fuatilia

Stories of Change - 2021 Competition

Gnyaisa

Member
Joined
Jul 13, 2021
Posts
23
Reaction score
24
Binadamu ni kiumbe aliyejaliwa uwezo mkubwa wa kufikiri na kupambanua mambo ikiwa ni pamoja na kupambana na changamoto mbalimbali za maisha. Amejaliwa uwezo wa kubadili changamoto yoyote iliyo mbele yake kuwa fursa yenye kumletea furaha, faida na maendeleo katika maisha yake.

Mtaalamu wa masuala ya saikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Northwestern cha nchini Marekani, Profesa Paul Rebel pamoja na watafiti mbalimbali wanaeleza kuwa uwezo wa ubongo wa binadamu wa kuhifadhi kumbukumbu unafikia Petabaiti 2.5 sawa na Gigabaiti milioni mbili na laki tano (2,500,000 GB)! Kompyuta zetu tunazotumia maofisini na majumbani zina uwezo wa wastani wa kuhifadhi kumbukumbu kuanzia Gigabaiti 20 mpaka 1000 pekee. Ili kuweza kueleweka kiurahisi wataalamu hawa wanatufafanulia kwamba nyaraka zote zinazopatikana katika maktaba ya bunge la Marekani (US Congress) zikiwekwa kwenye mfumo wa kielektroniki zinakadiriwa kuwa na ukubwa wa Gigabaiti elfu kumi (10,000) pekee! Kama ubongo wa binadamu ungefanya kazi ya kurekodi kama ifanyavyo kamera ya kurekodia picha za video kwenye runinga, wataalamu hawa wanaeleza kwamba Gigabaiti hizi 2,500,000 za ubongo zingetosha kuangalia picha hizo za video kwenye runinga kwa muda wa masaa 3,000,000 mfululizo! Ungelazimika kuiacha runinga ioneshe picha hizo za video kwa kipindi cha Zaidi ya miaka 300 mfululizo ili kufanikiwa kuzitumia Gigabaiti zote 2,500,000!

Tukiangazia changamoto mbalimbali zinazolikabili taifa letu na njia tunazotumia kukabiliana na changamoto hizo ni wazi kwamba wengi wetu hususani vijana hatujagundua uwezo mkubwa wa ubongo tuliojaliwa na Mwenyezi Mungu. Wakati dunia nzima ikiduwaa na kujiuliza inawezekanaje taifa changa na lenye makabila Zaidi ya 120 kuendelea kuishi kwa Amani, Umoja na Upendo ilihali mataifa yanayolizunguka yakiogelea kwenye dimbwi la damu kutokana na machafuko yasiyokwisha, watanzania tumeendelea kusujudu lawama na manung’uniko hata katika mazingira ambayo tulipaswa kuchukua hatua bila kuhusisha mkono wa serikali. Tumeshindwa kutumia Amani tuliyonayo katika kujiletea maendeleo ya haraka na badala yake tumeungana na dunia katika kuduwaa!

Wakati dunia ikishangaa inawezekanaje maajabu matatu (3) kati ya saba (7) ya bara la Afrika yapatikane katika taifa moja pekee wakati Afrika ina mataifa Zaidi ya 50! Watanzania kutwa tunashinda kwenye mitandao ya kijamii tukisutana umbeya na kushabikia timu za mpira za Ulaya! Mlima Kilimanjaro, bonde la Ngorongoro na mbuga ya wanyama ya Serengeti ni miongoni mwa maajabu mapya ya Afrika huku mto Nile ambao ni ajabu la 4 chanzo chake kikiwa ziwa Viktoria lililoko nchini Tanzania.

Wakati dunia ikishangaa inawezekanaje taifa moja pekee kuwa na mabonde lukuki yaliyojaa maji na rutuba, Watanzania tunaishia kulia njaa na bei ghali za vyakula kila mwaka! Tanzania ina bonde la mto Pangani lenye ukubwa wa kilometa za mraba 53,600 (Ukubwa sawa na mataifa ya Rwanda na Burundi kwa pamoja!), tuna bonde la mto Ruvuma lenye ukubwa wa kilometa za mraba 52,200 (ukubwa zaidi ya taifa la Denmark!). Tuna bonde la ziwa Nyasa lenye kilometa za mraba 37,000 (ukubwa zaidi ya taifa la Ubelgiji!). Tuna bonde la ziwa Rukwa lenye ukubwa wa kilometa za mraba 88,000 (ukubwa zaidi ya taifa la Austria). Pia tuna bonde la Wami Ruvu lenye kilometa za mraba 72,930 (ukubwa mara mbili ya mataifa ya Haiti na Jamaica!). Pia tunayo mabonde ya ziwa Tanganyika, bonde la Ziwa Viktoria na mabonde ya ziwa Eyasi, Manyara na Bubu.

Ni ukweli ulio wazi kwamba tumeshindwa kulitendea haki taifa letu. Ingawa tabia na hulka zetu njema kama watanzania zinafanana na uzuri wa taifa la Tanzania, bado hatujaweza kuidhihirishia dunia kwamba sisi ndio wamiliki wa mlima Kilimanjaro, mbuga ya Serengeti au visiwa maarufu vya Zanzibar. Tunawezaje kuiambia dunia kuwa maziwa makuu ya Viktoria, Tanganyika na Nyasa yako nchini Tanzania ilhali tukiombwa tani laki moja tu za samaki tutaishia kukabana mashati! Tunawezaje kusema madini ya Tanzanite hayapatikani sehemu yoyote duniani Zaidi ya Tanzania ilhali tukiombwa takwimu za miaka kumi nyuma za mauzo ya madini hayo tunawaambia taifa la India ndilo linaloongoza kwa kuuza Tanzanite katika soko la dunia likifuatiwa na Kenya! Tunaanzia wapi kujitapa kuwa binadamu wa kale kuliko wote hapa duniani alipatikana katika bonde la Olduvai nchini Tanzania ilhali watalii wakija kujionea ukweli wa mambo wanakumbana na makundi makubwa ya vijana wakiwa wameshikilia makaratasi ya kubashiri matokeo ya mechi za mpira wa ulaya (maarufu kama mikeka) ili kujipatia kipato bila kutoa jasho!
 
Upvote 1
Vijana hawana vision, hawana passion, hawana wanachokisimamia katika maisha yao binafsi,siku zote tunachofanya ni kutafuta wa kumlaumu na hili linatuondolea hali ya kuwajibika (sense of responsibility). Kama kila mtu atatambua hili at least tunaweza kupiga hatua moja mbele
 
Back
Top Bottom