SoC01 Umuhimu wa kuwa na Dira ya Maendeleo ya Taifa inayotekelezeka kwa wakati na kwa kuzingatia rasilimali zilizopo

Stories of Change - 2021 Competition

Abrianna

JF-Expert Member
Joined
Mar 30, 2021
Posts
4,696
Reaction score
15,390
Utangulizi
Dira kwa maana fupi ni muelekeo. Dira ya Maendeleo ya Tanzania (Tanzania Development Vision (TDV) 2025 ilianzishwa mwaka 1994 na kuzinduliwa rasmi mwaka 1999 ambapo utekelezaji wake ulianza mwaka 2000 lengo kuu likiwa kuongoza harakati za maendeleo ya uchumi na jamii zitakazoiwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati na kuondokana na umaskini uliokithiri ifikapo mwaka 2025. 'www.tanzania.go.tz' (tovuti kuu ya serikali)

Melengo makuu matano yalioainishwa katika Dira ya Maendeleo 2025 ni pamoja na kuboresha hali ya maisha ya kila Mtanzania, kuwepo kwa mazingira ya amani usalama na umoja,kujenga utawala bora,kujenga jamii iliyoelimika na kujenga uchumi imara unaokabiliana na ushindani. (Nukuu kutoka Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025).

Katika andiko hili, nitaangazia malengo makuu matano kama yalivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo 2025. Andiko langu litaangazia pia utekelezaji wa malengo haya na uhalisia wa maisha ya Mtanzania.

Katika uhalisia, Maendeleo ya Nchi yetu kwa asilimia kubwa yamekua yakitegemea Ilani ya chama tawala pamoja vipaumbele vya Rais aliye madarakani. Mfano halisi ni ununuzi wa ndege na ujenzi wa madaraja ambao uliingiza nchi katika madeni makubwa na umaskini. Ni wazi kwamba Dira ya Maendeleo ni kijarida tu ambacho kimetengenezwa kutimiza wajibu lakini hakina nafasi kubwa katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

Serikali imeunda mipango mingi kwa ajili ya utekelezaji wa maendeleo kama vile mpango wa maendeleo wa miaka mitanpo (Five Year Development Plan), MKUKUTA, Mpango wa Big Results Now (Matokeo Makubwa Sasa), Mpango wa maboresho ya utumishi wa Umma,pamoja na Maleongo ya Maendeleo ya Millenia chini ya nchi za Umoja wa Mataifa.

Katika mipango tajwa, yote ina malengo yanayolandana kwa maana ya kutokomeza umaskini kwa kuboresha huduma za afya, elimu, nishati, kilimo, maji, biashara, mahusiano ya kimataifa, ajira, kuboresha utumishi wa umma, kuweka usawa wa kijinsia pamoja na mengine mengi.

Hebu tuangazie miaka kumi nyuma tulinganishe na utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na hali halisi ya Watanzania mpaka leo hii.

Hali ya maisha ya Mtanzania imezidi kuwa duni pamoja na kwamba nchi yetu ipo katika uchumi wa kati wa chini, Mtanzania wa kawaida anashindwa kumudu gharama ndogo za mlo wa siku ilhali tunatangaziwa uchumi wetu umekua kwa asilimia 7% ( NBS 2019/2020).

Katika kujenga utawala bora, hali imezidi kuwa tete, ni wazi kwamba utawala wa sheria umekua jambo gumu katika nchi yetu hali inayopelekea kutokuwajibika kwa pamoja na ubadhirifu wa mali za umma (Rejea ripoti ya CAG 2020).

Katika Dira ya Mendeleo 2025, serikali imeonyesha nia ya kujenga jamii iliyoelimika na inayojifunza kila siku kulingana na mazingira na nyakati tulizopo, tukirudi kwenye uhalisia, kiwango cha ubora wa elimu zetu hakikidhi viwango vitakavyowawezesha wasomi wetu kuingia katika ushindani ndani na nje ya Tanzania, shule zetu nyingi hazina waalimu wa kutosha wala vifaa vya kufundishia, matamko ya kisiasa kwa upande mwingine yamekua yakiathiri mifumo ya elimu.

Kwa mfano mnamo mwezi Desemba 2020, Rais JPM aliagiza somo la historia ya Tanzania lianze kufundishwa katika shue za msingi mpaka sekondari, Wizara ya elimu iliandaa machapisho kwa ajili ya somo husika lakini baada ya Rais Samia kuingia madarakani somo hilo lilisitishwa rasmi.

Kwa upande mwingine serikali ilichangia kupotosha jamii badala ya kuelimisha. Nitoe mfano mdogo wa janga la Covid 19. Serikali ilisimama kidete kuuaminisha umma kwamba janga hili ni vita ya mabeberu dhidi yetu badala ya kutumia wataalamu wa afya kutoa elimu kuhusu namna bora ya kujikinga ili kuepuka maambukizi. Serikali ilienda mbali zaidi na kuhamasisha tiba mbadala na njia za asili ambazo zilitumika katika vituo vya afya pia.

Kauli ya serikali pamoja na viongozi wakuu wa nchi imeleta mkanganyiko pamoja na hisia tofauti juu ya janga hili na kusababisha watu kuishi pasipo kuchukua tahadhari hata baada ya serikali kubadili msimamo na kuamua kufuata njia za kitaalamu. Ukijaribu kuongea na watanzania kumi, tisa kati yao wanaogopa chanjo na kuamini kwamba mabeberu wanataka kutumaliza.

(picha kutoka mtandaoni)

Katika uboreshaji wa utumishi wa umma, vilio vimekua vingi, utekelezaji wa dhima hii umesahaulika kwa miaka zaidi ya mitano iliyopita, vilio vingi vya wafanyakazi kuhusu nyongeza za mishahara pamoja na kupanda madaraja, makato makubwa, na mishahara duni ambayo haikidhi maisha ya kila siku.

Mambo ya muhimu yaliyotajwa katika utekelezaji wa malengo ya milenia ni pamoja na kukuza mahusiano ya kimataifa, kutokomeza umaskini wa kipato na njaa. Kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita, Tanzania imepuuza kwa kiasi kikubwa sana mahusiano ya kimataifa kutokana na misimamo ya kiongozi aliyekua madarakani. Vipato vya wananchi vimeshuka kutokana na tozo kubwa katika bidhaa na huduma, mfumuko wa bei umeathiri pembejeo za kilimo na bidhaa mbalimbali, uonevu kwa wafanyabiashara,ubambikaji wa kesi na kodi uliosababisha biashara nyingi kufungwa. Tunao mfano halisi wa sasa katika tozo ya miamala ambayo imeleta taharuki kubwa kwa wananchi masikini ambao hata kula yao ni ya tabu.

Mapendekezo
• Serikali ianzishe taasisi maalumu kwaajili ya kuandaa na kusimamia Dira ya Maendeleo ya Taifa. Chombo hicho kiwe na kazi ya kuandaa, kusimamia pamoja na kuishauri serikali iliyopo madarakani bila kujali chama.Taasisi hii ihakikishe sera sera na mipango ya taasisi mbalimbali za serikali pamoja na wizara zina uelekeo mmoja na zinashirikiana ka ukaribu. Kwa mfano suala la kuzalisha wahitimu wenye weledi ni lazima liendane na uboreshaji mfumo wa elimu, kwa hiyo ni lazima wizara ya kazi na wizara ya elimu zishirikiane kubaini mapungufu yanayoonekana kwa wahitimu wanaoajiriwa ili waweze kubaini njia bora ya kuboresha.

Taasisi hii ipewe mamlaka ya kusimamia serikali kama ilivyo bunge na mahakama na kwamba ilani ya chama cha kiongozi aliyeko madarakani ilenge kutafuta au kuonyesha njia sahihi za kuipeleka nchi kule ambako dira inaonyesha, hii itasaidia kutekeleza miradi iliyoachwa au iliyoanzishwa na kiongozi aliemaliza muda wake, mfano wakati Rais JPM naingia madarakani alisitisha ujenzi wa bandari ya Bagamoyo kwa madai kwamba mikataba ilikua mibovu na iliyojaa unyonyaji, siku chache baada ya Rais Samia kuingia madarakani mapitio ya ujenzi wa bandari yameanza, hii ni kwa sababu hakuna mfumo wa kusimamia viapaumbele vya maendeleo ya Taifa badala yake kila kiongozi anajiamulia kile anachopenda.

• Ipatikane katiba imara ambayo itasaidia kudhibiti na kusimamia viongozi walioko madarakani na hata baada ya kustaafu kama ilivyo kwa nchi nyingine kama Marekani na Afrika ya Kusini. Hii itahakikisha viongozi wote wanafanya kazi kwa kuheshimu haki za binadamu na sheria na taratibu zilizopo bila kuathiri malengo ya Taifa kwa ujumla. Katiba imara pia itasaidia kuweka uwajibikaji na usawa kati ya watumishi/viongozi, kuondoa ubadhirifu na matumizi mabaya ya madaraka.

• Serikali ijikite zaidi katika kuvumbua vyanzo vipya vya mapato badala ya kujikita katika kuongeza kodi katika huduma mbalimbali za kijamii ili kupunguza mzigo mkubwa wa kodi kwa wananchi na badala yake wananchi wapate unafuu wa maisha. Mfano sekta ya utalii na madini zinaweza kuwa vyanzo vizuri vya mapato kama tukiweka usimamizi mzuri na mifumo ya kuaminika ili kuepusha mianya ya ubadhirifu. Pia serikali ijikite katika kuboresha mfumo wa elimu ili kuruhusu vijana wengi kujiajiri katika nyanja mbalimbali badala ya kutegemea ajira kutoka serikalini.

• Bajeti za maendeleo zilizoidhinishwa na bunge zisitumike kinyume na lengo ili tuweze kutekeleza mipango iliyopangwa katika mwaka wa fedha wa serikali. Huko nyuma tulishuhudia pesa zikipelekwa katika matumizi ambayo hayakuidhinishwa na bunge hali iliyochangia kukwamishwa kwa miradi mingi ya maendeleo iliyoidhinishwa na bunge. Bajeti inayoidhinishwa pia iende sambamba na Dira ya Maendeleo ya Taifa.

• Serikali iunde mfumo shirikishi utakaosaidia wananchi kushiriki katika kuonyesha vipaumbele vya maendeleo pamoja na utekelezaji. Hii itasaidia wananchi kuwa wasimamizi wa moja kwa moja wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao.

• Serikali iwatumie wataalamu wa masuala ya uchumi walioko nchini badala ya kutumia wanasiasa pekee katika kuandaa bajeti na matumizi ya serikali, pia serikali ijenge utamaduni wa kuwatumia wataalamu waliobobea katika fani mbalimbali nchini katika kuandaa na kusimamia sera mbali mbali kwaajili ya kukuza uchumi na kuleta maendeleo ya Taifa pamoja na kuheshimu mawazo na maelekezo ya wataalamu katika sekta mbalimbali hata pale yanapotokea majanga yanayohitaji ufumbuzi wa kitaalamu. Kwa kufanya hivi, tutapunguza au kudhibiti matamko ya kisiasa katika mambo nyeti yanayohitaji ufumbuzi wa kitaalamu kama vile Afya, Elimu na Uchumi.

Hitimisho
Natoa wito kwa viongozi/wenye mamlaka, na watunga sera wa nchi, maamuzi yoyote wanayofanya yanaathiri au kufaidisha jamii nzima, wao ni sehemu ya jamii na hivyo wataathirika au kufaidika na maamuzi hayo kwa namna moja au nyingine. Ni vyema kufanya uchambuzi yakinifu kabla ya kufanya maamuzi ili kuepuka athari zozote zitakazoisababishwa na maamuzi yao ikiwa ni pamoja na kurudisha nyuma maendeleo ya Taifa.

Asanteni Sana​
 
Upvote 1.3K
Kuna mambo mengi sana ambayo yanachukuliwa kizembe, karne hii kuna watoto wanakaa chini, wengine wanasoma nje kwa sababu madarasa hayatoshi, kuna watu wanakunywa maji ya mtoni ambayo ng'ombe wanaoga humohumo, kuna siku umeme unakatika hata siku tatu na hakuna maelezo yoyote kutoka mamlaka husika, kuna wakati ofisi za umma hazifanyi kazi kisa mtandao upo chini.Ukijiuliza sana huwezi kupata jibu sahihi
 
Asante sana Resurrection kwa maoni yako, nakubaliana na wewe kabisa kwamba tunahitaji katiba imara kama nilivyopendekeza hapo juu, tunahitaji tume huru, na tunahitaji pia dira ya maendeleo ambayo kila kiongozi aliyeko madarakani ataongoza kwa kuifuata bila kujali itikadi za chama chake au maslahi yake binafsi

Tukiwa na katiba imara pamoja na taasisi zilizo huru, itakua rahisi kuwawajibisha viongozi wanaotumia madaraka yao vibaya au wanaofanya ubadhirifu katika ofisi za umaa, na hii itasaidia kuleta uwajibikaji na uadilifu.
 
Laiti watunga sera wangekua wanaakili za hivi 🙏🙏🙏
Mkuu vvm Watunga sera wote wanazo hizi akili ila wakishakua kwenye ground akili na mawazo wanaweka pembeni, wanafanya kazi kwa mihemko na matamko bila kuzingatia taaluma zao na maslahi ya watanzania kwa ujumla, ndio maana tukasema tunahitaji huru kikichopewa mamlaka kikatiba kusimamia dira ya maendeleo pamoja utekelezahi wake kwa ujumla
 
Asante sana mkuu Kirchhoff kwa mchango wako na support yako

Dira ipo katika maandishi lakini utekelezaji wake ni asilimia ndogo, kwa kweli tunahitaji ipewe nguvu na izingatiwe ili tuweze kusonga mbele
 
Matatizo yoooteee nchi hii yanaanzia hapo kwenye katiba inayomfanya rais kuwa Mungu mtu, kiukweli huwa namlaumu sana late Nyerere ambaye ndiye muasisi, na mtekelezaji wa muda mrefu kuliko wote wa hii katiba maana alitawala muda mrefu sana kuliko wenzake wote, yet akashindwa hata kusimamia mabadiliko makubwa ya katiba hii. Bahati mbaya nyingine ni kwamba kwa sasa watanzania wengi wanaamini hiyo kazi ya kudai katiba mpya ni ya CHADEMA.
 
Nadhan MKUKUTA na MKURABITA ni mtokeo ya Dira ya Maendeleo na ndo zilizalisha taasis kama TASAF. Swali linakuja mpaka Sasa Zaid ya miaka 20 kuna mafanikio gani yamepatikana?
 
Nakubaliana na hoja yako kabisa. Mzizi wa yote haya ni kuwepo kwa Effective controls zitakazo leta checks and balances ambazo zitaainishwa kwenye Katiba mpya. Hata kama Tunachagua kiongozi ni lazima kuwe na vigezo sahihi, performance review ya utendaji wake na kumuwajibisha na yote haya yanapatikana kwenye katiba ya wananchi na siyo ya watawala.
 
Hili ni pendekezo zuri Abrianna. Wapenda maendeleo wote watakubaliana na wewe kuwa bila katiba imara basi hatutaweza kutoka hapa tulipo.
 
Nadhan MKUKUTA na MKURABITA ni mtokeo ya Dira ya Maendeleo na ndo zilizalisha taasis kama TASAF. Swali linakuja mpaka Sasa Zaid ya miaka 20 kuna mafanikio gani yamepatikana?
MKUKUTA awamu ya kwanza 2005/2006-2009 ulilenga kukuza uchumi, kupunguza umaskini wa kipato,ubora wa maosha ya watu na ustawi wa jamii bila kusahau kuimarisha utawala bora na uwajibikaji, ukisoma malengo ya Dira ya Taifa 2025 hayatofautiani na haya ya MKUKUTA, kwa maana hiyo mambo haya mawili yote yalianzishwa kwa malengo mamoja ila katika nyakati tofauti, kwa kifupi MKUKUTA inachangia katika utekelezaji wa Dira ya Maendeleo 2025 na malengo ya Millenia 2015

MKURABITA kwa maana ya Mpango wa kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania ambao ulianzishwa 2004 ukiwa ni sehemu ya MKUKUTA na lengo kuu lilikua ni kuwapa nguvu ya kiuchumi wananchi na kuwaongezea uwezo wa kumiliki na kufanya biashara katika mifumo rasmi unaozingatia utawala wa sheria

Kwa hiyo hii mipango miwili ni sehemu ya dira na hivyo dira inabaki kama Tawi kuu la mipango ya maendeleo nchini na ni lazima isimamiwe kikamilifu

Ukiangalia MKURABITA tangu kuanzishwa kwake na lengo lake, bado kuna gap kubwa kwa sababu serikali bado haijawapa au kuwajengea wananchi mifumo imara ya kufanya na kumiliki biashara, badala yake serikali imekua msitari wa mbele katika kuangamiza biashara za wanyonge kwa kuweka kodi kubwa na tozo nyingi na wakati mwingine kuwabambikia kesi za hovyo, hakuna mazingira rafiki kati ya Mabenki wa wananchi yanayowawezesha kupata mikopo matokeo yake wananchi wanaogopa benki kama vituo vya polisi, riba za mikopo ni kubwa, tozo ni nyingi, uonevu ni mkubwa, hakuna sehemu rasmi zilizoandaliwa kwa ajili ya biashara ndogondogo katika maeneo mabalimbali nchini, bado kuna mambo mengi yanayohitaji usaidizi wa wataalamu ili tuweze kusasimisha hizi biashara na kuwajengea wananchi mazingira mazuri na salama ya kujipatia kipato.

Tukija kwenye MKUKUTA bado ni kitendawili kile kile, tunasema tunapunguza umaskini wa kipato lakini kipato cha wananchi tunakipokonya kupitia tozo, tunasema tunaboresha utawala wa sheria na uwajibikaji lakini hali inazidi kuwa mbaya

Kimsingi tunahitaji kuweka nguvu kubwa kuhakikisha dira inatekelezwa kama ilivyopangwa kwa usaidizi wa wataalamu wetu pamoja na usimamizi thabiti.
 
Mzigo mkubwa wa kodi unaua biashara na maendeleo ya wananchi, kuendelea mzigo wa kodi lazima upungue
Ni kweli mkuu, serikali haijajenga mazingira rafiki ya kufanya biashara badala yake wametengeneza mianya ya unyonyaji na uonevu dhidi ya hawa wafanyabiashara
 
TASAF imekuwa sehemu ya watu wasiostahili kupata fedha, tofauti na malengo yaliyokusudiwa.
Kwa sasa inafanya kazi kinyume na lengo kwa sababu kaya zinazopewa hizi fedha ukiziangalia kiundani utagundua kwamba zina watu wanaojiweza na hazistahili kupata msaada, badala yake fedha hizi zingeelekezwa kutekeleza shughuli zingine za maendeleo na kuzalisha ajira kwa ajili ya hawa wanaopewa misaada ili waweze kumudu maisha yao pasipo kutegemea pesa hizo
 
Hili ni pendekezo zuri Abrianna. Wapenda maendeleo wote watakubaliana na wewe kuwa bila katiba imara basi hatutaweza kutoka hapa tulipo.
Asante sana mkuu kenshi Ni kweli katiba ni priority kwa sasa na ndio itatusaidia kutatua vitendawili vingine vyote katika nchi hii
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…