PostGE2025 Uongozi unaweza kuwa halali Kisheria, lakini ukakosa uhalali wa kijamii

PostGE2025 Uongozi unaweza kuwa halali Kisheria, lakini ukakosa uhalali wa kijamii

Conversations and stories after Tanzania's 2025 General Elections
Joined
Dec 1, 2025
Posts
7
Reaction score
3
file_00000000dca8722fb004a365cf577a2d.png

Historia inaonesha uongozi unaweza kuwa halali Kisheria lakini ukakosa uhalali wa kijamii

Takribani miezi minne baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, Tanzania inakabiliana na kipimo halisi cha demokrasia yake na uwezo wa upinzani kuwakilisha sauti za wananchi.

Kwa mujibu wa utafiti wa Shirika la Kimataifa la Utafiti na Sera inayojikita katika kukuza Demokrasia (IDEA) na ripoti za Afrobarometer, ushindi wa kura pekee haujengi uhalali wa kidemokrasia bali ni jinsi mfumo wa kisiasa unavyoshughulikia tofauti za maoni, kudhibiti migogoro, na kuimarisha imani ya umma baada ya matokeo.

Ni katika kipindi hiki ambapo sauti za wananchi, hoja za upinzani, na vitendo vya Serikali huamua hatma ya demokrasia kwa kuimarika au kudhoofika kimyakimya.

Hata hivyo, kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa na wanazuoni wa utawala wa kidemokrasia, hatua hiyo ni mwanzo tu wa kipimo muhimu je, mfumo wa kisiasa unaweza kuhimili tofauti za maoni, kuponya migawanyiko na kujenga uongozi unaokubalika zaidi ya ushindi wa kura?

Mtaalam wa masuala ya Siasa, John Mkumbo anasema kura ni mwanzo, sio hatima na kwamba katika nadharia za demokrasia, uhalali wa uongozi haupimwi kwa idadi ya kura pekee.

"Uhalali huo una nguzo mbili kuu ambazo ni uhalali wa kisheria na uhalali wa kijamii, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, uongozi hupata uhalali wa kisheria pale uchaguzi unapofanyika kwa kuzingatia sheria, haki, usawa na taratibu zilizowekwa, "anasema na kuongeza:

"Historia ya mifumo ya kisiasa nchini inaonyesha ukweli mmoja usiopingika kwamba uongozi unaweza kuwa halali kisheria lakini ukakosa uhalali wa kijamii, hapo ndipo wananchi hubaki na mashaka juu ya uwazi, haki au ushiriki sawa katika mchakato wa maendeleo uhalali wa kisiasa huanza kupasuka kimyakimya,” amesema.

Ameenda mbali zaidi kueleza kwamba ni katika mpasuko huo ndipo migogoro ya kisiasa huota mizizi sio kwa sababu ya nani alishinda, bali kwa sababu ya nani alihisi kutosikilizwa na kuongeza kuwa imani ya umma ni mtaji muhimu zaidi wa kiutawala na inapoyumba, hata Serikali iliyo halali hukabili ugumu wa kutawala kwa ufanisi na kwa amani.

Serikali baada ya Uchaguzi

Kipimo cha uongozi wa kidemokrasia baada ya uchaguzi, Serikali iliingia katika awamu nyeti ya kile wanazuoni hukiita democratic consolidation kipindi cha kuimarisha maridhiano, kurejesha imani ya umma na kuthibitisha kuwa mamlaka yaliyopo yanatumika kwa maslahi ya wote.

Katika kipindi hiki, kauli na vitendo vya Serikali imekuwa na uzito mkubwa kuliko hotuba za kampeni.

Screenshot_20260227-130949~2.jpg

Asasi za kiraia, ikiwemo Legal and Human Rights Centre (LHRC), zimekuwa zikisisitiza kuwa kuheshimu haki za kisiasa, uhuru wa maoni, mikutano ya amani na utawala wa sheria si zawadi bali ni wajibu wa kikatiba.

Mwanazuoni wa siasa Freddy Wailes ameonya kuwa pale Serikali inapochagua nguvu badala ya mazungumzo, au udhibiti badala ya uwajibikaji, huongeza ufa kati ya dola na raia.

Anasema "Ufa huu, ukiachwa bila kushughulikiwa, hujenga mazingira ya sintofahamu, hofu na hatimaye kudhoofisha mshikamano wa kitaifa, Serikali inayojali demokrasia haitakiwi kuonekana kama mshindi wa uchaguzi pekee, bali kama msimamizi wa maslahi ya taifa zima ikiwemo sauti za waliopinga au kukosoa,"anasiaitiza.

Upinzani: Kati ya uwakilishi na uwajibikaji

Katika demokrasia ya vyama vingi nchini Tanzania upinzani unachukuliwa kama zaidi ya kundi la waliopoteza uchaguzi.

Mtaalamu wa mifumo ya kisiasa wa nchini India, Profesa Prabhat Patnik anaaeleza kuwa licha ya upinzani kupotezewa bado una jukumu la kuhoji sera za Serikali, kutoa mbadala wa sera na kusimamia matumizi ya rasilimali za umma kwa niaba ya wananchi.

Hata hivyo, anaeleza demokrasia ya baada ya uchaguzi huuweka upinzani katika mizani nyeti.

"Kwa upande mmoja, upinzani unabeba matumaini ya wale ambao hawakuridhika na matokeo,kwa upande mwingine, una wajibu wa kulinda amani, mshikamano na misingi ya kikatiba,

"Siasa za jazba, uchochezi au kuvunja misingi ya sheria huweza kugeuka mzigo kwa taifa na hatimaye kuumiza demokrasia yenyewe. Katika muktadha huu, ukomavu wa kisiasa hupimwa si kwa ukubwa wa sauti, bali kwa uzito wa hoja," anasema.

Anasema Serikali inayowajibika na upinzani unaojenga hoja na wananchi ndizo nguzo za kulinda demokrasia endelevu.

Kipindi hiki nyeti, mustakabali wa demokrasia ya Tanzania hauko mikononi mwa mshindi pekee, bali uko katika namna taifa linavyoshughulikia tofauti zake kwa busara, haki na mazungumzo.

Kwa mtazamo wa ndani ya Tanzania, mchambuzi huru wa masuala ya siasa na utawala Hanifa Ramadhan anaeleza kuwa upinzani una nafasi ya kipekee katika kulinda uhalali wa mfumo wa kisiasa, hasa pale ambapo Serikali iliyopo inapokosa ridhaa pana ya kijamii.

Anasema katika mazingira ya baada ya uchaguzi yenye mashaka, upinzani hubeba jukumu la kuibua hoja za wananchi waliokatishwa tamaa, si kwa lengo la kuvunja dola, bali kulazimisha uwajibikaji wa kisera na kurejesha mizani ya madaraka.

"Upinzani unaponyamazishwa au kupuuzwa, mfumo mzima wa demokrasia hudhoofika kwa sababu sauti mbadala hufutwa katika mjadala wa kitaifa," anaeleza.

Amegusia kuwa demokrasia ya baada ya uchaguzi hupimwa kwa namna Serikali inavyovumilia ukosoaji na upinzani halali.

Anaeleza pale ambapo upinzani unachukuliwa kama tishio badala ya mshirika wa kikatiba katika kusimamia Serikali, hujenga mazingira ya hofu na ukimya wa kisiasa miongoni mwa wananchi.

“Upinzani imara na huru ni kioo kinachoonesha kiwango cha uhalali wa Serikali; kadri kioo hicho kinavyovunjwa, ndivyo taswira ya uhalali inavyozidi kufifia,” anasisitiza.

Serikali bila Uhalali wa Kidemokrasia

Kwa kuzingatia hali ilivyo sasa ni dhahiri kwamba uhalali wa Serikali ya Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, hauwezi kufungwa kwa hoja ya ushindi wa kura pekee.

Kwa mujibu wa Mwandishi wa Habari mashuhuri hapa nchini Jenerali Ulimwengu anasema kwa misingi ya nadharia za demokrasia, ushindi wa uchaguzi hauhalalishi uongozi endapo uhalali wa kijamii na kisiasa haukujengwa baada ya matokeo.

Anasema katika muktadha wa Tanzania, dalili nyingi zinaonyesha kuwa Serikali iliyopo ina uhalali wa kisheria tu, lakini inakosa uhalali wa kidemokrasia.

“Mashaka yanayoendelea baada ya uchaguzi, malalamiko ya upinzani, ukimya wa wananchi unaotokana na hofu, pamoja na vikwazo dhidi ya uhuru wa kisiasa vinaashiria kuvunjika kwa mkataba wa kijamii kati ya dola na raia;

Kwa mantiki hiyo, hoja kwamba Serikali “ni halali kwa sababu ilishinda uchaguzi” inakuwa dhaifu pale ambapo wananchi wanahisi kutosikilizwa, upinzani unazuiwa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba, na haki za kisiasa zinachukuliwa kama fadhila badala ya haki,"anasisitiza.

Kwa mantiki hiyo Serikali iliyopo haina uhalali wa kidemokrasia, kwa kuwa imeshindwa kujenga maridhiano ya kijamii, kurejesha imani ya umma na kuhakikisha mazingira huru ya kisiasa baada ya uchaguzi.

Serikali inapaswa kuelewa kuwa Demokrasia si tukio la siku ya kupiga kura, bali ni mchakato endelevu wa kuongoza kwa ridhaa ya wananchi, si kwa hofu au ukimya wa kulazimishwa.

Hali iliyopo, hatari kubwa si upinzani wala ukosoaji, bali ni kuendelea kwa mfumo unaotawala bila ridhaa ya wananchi wala mabadiliko ya msingi.

Kwa jicho la tatu naiona Tanzania inahatarisha demokrasia yake na kubaki jina tupu, huku mamlaka yakibaki mikononi mwa dola badala ya wananchi.

Screenshot_20260227-131046~2.jpg

file_000000003dc071f5b214e7a1a41932d7.png
 
Back
Top Bottom