Shahidi wa kwanza alitoa ushahidi wake katika Mahakama hiyo Alhamisi (12 Februari) ya wiki iliyopita mbele ya Jaji Paulo Kihwelo. Shahidi wa kwanza katika kesi hiyo ni Said Mnunka ambaye ni Ofisa mstaafu wa FFU. Shahidi huyo alidai kuwa hakumtambua aliyedaiwa kufanya mauaji hayo hadi alipotazama picha kwenye gazeti.
"Sikuweza kutambua chochote kuna kitu kilitokea, lakini kama Septemba 3, niliona gazeti ofisini kwa RPC wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, ndipo nilibaini kuwa kuna kitu kilitokea jana yake (Septemba 2) baadaye ndipo tulizifuatilia kwa mtu mmoja mmoja kuanzia kwa wale askari walionekana kwenye ile picha hadi kumbaini mtuhumiwa," alidai Mnunka.
Shahidi wa pili alitoa ushahidi wake katika Mahakama hiyo Ijumaa ya wiki iliyopita. Shahidi huyo ni Mkuu wa Kituo cha Polisi Wilaya (OCD) cha Mufindi mkoani Iringa, Assel Mwampamba. Alidai kuwa Septemba 1, mwaka 2012, alipigiwa simu na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, na kumuamuru aandae kikosi kwenda Kijiji cha Nyololo kuzuia maandamano na mkutano wa Chama cha Demokraasia na Maendeleo (Chadema).
"Siku hiyo nilitekeleza maagizo kama nilivyoagizwa na RPC kesho (Septemba 2) tulielekea Nyololo nikiwa na kikosi changu, gari la mkoa moja, magari mawili ya askari wa FFU kutoka mjini Dodoma," alidai.
OCD Mwampamba aliendelea kudai kuwa walipofika Mufindi walikutana na magari mawili ya polisi kutoka Wilaya ya Mufindi na kuelekea kwenye eneo la tukio. Alidai walipofika Kijiji cha Nyololo walikuta Chadema wamefunga vinasa sauti kwa ajili ya kuanza mkutano wao na kwamba aliteremka kwenye gari na kuongea na viongozi wa chama hicho, lakini walikaidi na kutamka kuwa liwalo na liwe lazima wafanye mkutano wao.
Alidai kuwa aliamriwa kuzuia maandamano hayo ili kutekeleza amri ya Serikali baada ya kutangaza kuzuia vyama vyote vya siasa visiendelee na mikutano kutokana na zoezi la sensa ya watu na makazi. Aliendelea kudai kuwa baada ya kuona fujo zimetulia, ndipo waliamriwa kuingia kwenye magari kwa ajili ya kurudi kwenye kambi zao.
Hata hivyo, alidai kabla hawajaondoka, alishtukia Mwangosi ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa, amemkamata mikono bila kujua sababu, ndipo alipoamua kupiga yowe kuomba msaada.
Alidai wakati askari wakienda kumsaidia, alisikia mlipuko wa kishindo na kupoteza fahamu. Alidai alipozinduka alijikuta amelazwa Hospitali ya Wilaya Mufindi akipatiwa matibabu bila kujua kilichotokea Septemba 2, mwaka 2012.
Alidai baadae aliambiwa kuwa Mwangosi alifariki dunia. "Sikujua mwandishi huyo alikuwa na dhumuni gani, ndiyo maana nikaamua kuomba msaada kutoka kwa askari wenzangu ili waweze kunisaidia, " alidai Mwampamba.
Jaji Kihwelo aliahirisha kesi hiyo hadi February 16. 2015 atakapoendelea kusikiliza ushahidi huo. Jaji Kihwelo alisema kuwa mashahidi hao wawili watahitajika tena mahakamani hapo kama ushahidi walioutoa haujakamilika. Baada ya shahidi wa pili kumaliza kutoa ushahidi, Jaji Kihwelo alisema kuwa shauri hilo limehairishwa na hakumtaja ni shahidi yupi atatoa ushahidi February 16.
NIPASHE