Upendo ni silaha isiyojeruhi

Upendo ni silaha isiyojeruhi

GoldDhahabu

JF-Expert Member
Joined
Apr 29, 2023
Posts
7,189
Reaction score
10,375
Kama ambavyo hakuna mkate mgumu mbele ya chai, kadhalika, hakuna mfupa mbishi mbele ya upendo. Upendo huusaga hata mfupa uliomshinda fisi.

Ukimwi ni "ugonjwa" hatari, lakini aliye na upungufu wa upendo moyoni yupo hatarini zaidi kuliko mwenye virusi vya ukimwi.

Upungufu wa upendo, umesababisha ndoa nyingi kuvunjika.

Upungufu wa upendo, umesababisha maafa mengi, hata kupelekea wengine kupoteza maisha.

Lakini kwa upendo, mambo mengi mema yamefanyika.

Kama ni msomaji wa vitabu, huenda ulishakisoma kitabu chenye ushuhuda ninaoenda kuusimulia sasa.

Dada mmoja, baada ya kukwazwa sana na mume wake, tena mara nyingi, alifikia uamuzi kuwa ni bora ndoa ivunjike.

Lakini kabla ya kutekeleza uamuzi wake, alimshirikisha kaka yake. Kwa bahati nzuri, kaka yake alikuwa ni "mtaalam" wa Saikolojia, hivyo akaamua kumsaidia dada yake bila dada mtu kufahamu kuwa ushauri aliopewa ni wa kuiponya ndoa yake.

Kwanza, alimwuliza sababu ya kutaka kuachana na mume wake. Alipomwambia ni kwa sababu ameshaujeruhi moyo wake mara nyingi, alimwelekeza cha kufanya ili naye amjeruhi kisawasawa.

Alimwambia kuwa kuanzia siku hiyo, ajitahidi kuwa mnyenyekevu kwa mumewe, na kumwonesha upendo wa hali ya juu, hata kama ni kwa kuigiza. Alimwambia afanye hivyo kwa miezi kadhaa, halafu mume wake atakapobaini kuwa anampenda, ndipo amwache.

Dada mtu alichukua ushauri wa kakaye kama ulivyo.

Na kama ilivyo ada, matendo ni mbegu. Atendacho mtu ndicho avunacho.

Baada ya dada mtu kuanza kutekeleza agenda upendo kwa mume wake, muda si mrefu, mumewe naye alianza kurudisha mapigo.

Ndoa ikageuka fujo, safari hii, si fujo za kuumizana. Yalizaliwa mashindano ya kutendeana mema. Ilimpelekea kila mmoja akawa anavizia nafasi ya kumtendea mwenzake jema. Hakukuweko na aliyekuwa tayari kushindwa.

Mashindano ya upendo yalipokuwa yamepamba moto, siku moja, dada mtu alimpigia kakaye simu na kumjulisha hali ya ndoa yake. Alimweleza kuwa mume wake amekuwa mume mwenye upendo mno.

Naam, kakaye alivyosikia hivyo, alimwambia dadaye kuwa huo ndiyo wakati sahihi wa kuachana na mumewe.

Jibu lake? "Nitampata wapi tena mwanaume kama huyu?"

Upendo ulibadilisha hali ya mambo. Upendo haushindwi.

Unaweza kuthubutu kumpenda hata asiyekupenda?

Unaweza kumsema vizuri hata anayekusema vibaya?

Unaweza kumpelekea zawadi nzuri, au kumtendea jambo jema hata ambaye unafahamu kuwa anakuchukia?

Watu wengi wanaweza kuwatendea mema wale wanaowatendea mema, ila ni watu wenye upendo pekee wanaoweza kuwatendea mema "wabaya" wao.

Anayetawaliwa na upendo ana afya nzuri kiroho na kiakili. Kumbatia upendo, hautajutia.

Imeandikwa,WAPENDENI MAADUI ZENU!

Imeagizwa, MPENDE JIRANI YAKO KAMA NAFSI YAKO.

Kupendwa ni jambo jema, lakini anayependa anafaidi zaidi kuliko hata anayependwa.

Mtu anaweza asijue wewe ni nani kwake, lakini wewe usiache kutambua yeye ni nani kwako. Mpende, bila kujali kama anastahili au hastahili.

Mpende, isipokuwa na manufaa kwake itakuwa na manufaa kwa moyo wako.

Upendo haujawahi kushindwa! Maisha ya upendo ni maisha ya ushindi.

Wapende wote.
 
Back
Top Bottom