Sehemu ya Nne - Legacy inayoweza achwa na Rais ambae awali alikuwa ni Makamu wa Rais kupitia mfumo wa mgombea mwenza.
Je:
- Rais anayepatikana kwa njia ya kurithi nafasi iliyoachwa wazi na Rais aliyefariki akiwa madarakani anaweza kujenga ‘Legacy’ yake tofauti na Rais aliyemtangulia?
Uzoefu wa Taifa la Marekani unaendelea kutupa majibu. Katika sehemu inayofuata tutangalia kwa undani uRais Lyndon B. Johnson.
Lyndon B. Johnson aliteuliwa kuwa mgombea mwenza na mgombea Urais – JF Kennedy katika uchaguzi wa Rais wa mwaka 1960 na hatimaye kuwa makamu wake wa Rais. Sababu kubwa ya JF Kennedy kumteua Lyndon Johnson kuwa mgombea wake mwenza ilikuwa ni kumsaidia JF Kennedy kupata kura za kutosha katika jimbo gumu la Texas. It is such a ‘coincidence’ kwamba miaka mitatu tu baadae (1963), Rais JF Kennedy akauwawa kwa kupigwa risasi akiwa ziarani katika jimbo hilo hilo la Texas.
Lyndon Johnson aliapishwa kuchukua nafasi ya JF Kennedy akiwa angani ndani ya ndege iliyokuwa imebeba mwili wa marehemu John Kennedy kutoka Texas (jimbo alipouwawa JF Kennedy) kuelekea makao makuu ya taifa hilo, Washington D.C, kwa ajili ya shughuli za mazishi ya kitaifa. Ndege ilipofika Washington DC na mwili wa marehemu JF Kennedy muda mfupi baada ya kuondoka Texas, Rais Lyndon Johnson alishuka ndani ya ndege na kuanza shughuli za mazishi akiwa tayari ameshaapishwa kuwa Rais na Amiri Jeshi Mkuu. Hali hii haina tofauti sana na kilichotokea Tanzania kufuatia kiti cha Urais kuwa wazi baada ya Rais John Magufuli kufariki akiwa bado yupo madarakani.
Hata hivyo, Rais Lyndon Johnson aliweza kutumikia nafasi hiyo kwa muhula mmoja tu. Sababu iliyomfanya Lyndon Johnson kuwa Rais wa muhula mmoja haikuwa ni zuio la Kikatiba. Badala yake, kilichomfanya Lyndon B Johnson awe ni Rais wa muhula mmoja ilikuwa ni maaamuzi yake mwenyewe ya kisera akiwa Rais. Ni maamuzi hayo ya kisera ndio yaliyopelekea Rais Johnson apoteze mvuto ndani na nje ya chama chake cha siasa (Chama cha Democrat), hivyo kulazimika kutangaza kutokuwa na nia ya kugombea uchaguzi ili kutumikia awamu ya mbili.
Rais mteule Lyndon Johnson aliapa kuanza kazi kwa kusimamia suala la Haki za Raia – “Civil Rights”. Ikumbukwe kwamba kabla ya kuuwawa kwa risasi, Rais JF Kennedy alijaribu kupeleka muswaada juu ya Haki za Raia bungeni ili uwe sheria lakini alifariki kabla hajafanikiwa. Lakini kufuatia ushawishi na umahiri wake kama Rais, Lyndon Johnson alifanikiwa kuandaa na kupeleka muswada huo bungeni na baadae kupitishwa kuwa sheria – The Civil Rights ACT (1964). Hii lilichangia sana kwa Rais Johnson kupata ushindi mkubwa katika uchaguzi wa Rais November 1964 dhidi ya mgombea wa chama cha upinzani (Republican Party) – Barry Goldwater.
- Legacy ya Rais Lyndon Johnson
Kama tulivyogusia awali, mara tu baada ya kuingia madarakani kufuatia kifo cha Rais JF Kennedy, kipaumbele cha kwanza cha Rais Johnson ilikuwa ni maandalizi ya muswada wa HAKI ZA RAIA (Civil Rights) na kuupeleka bungeni ukawe sheria. Tumeona kwamba mtangulizi wake – JF Kennedy alifariki akiwa bado hajafanikiwa katika hilo.
Katika sehemu inayofuata tutaangalia kwa undani sheria ya haki za raia (1964) pamoja na nyinginezo zilizomsaidia Rais Lyndon Johnson kujenga legacy kubwa na tofauti na ya mtangulizi wake, JF Kennedy.
Sheria ya Haki za Raia (1964) zilipiga marufuku ubaguzi wa rangi katika maeneo yafuatayo:
- ELIMU – Kutoa fursa sawa kielimu kwa raia wote bila ya kujali tofauti za rangi zao.
- MAJENGO NA MAKAZI – Kutoa fursa sawa kwa raia wote kuingia katika maofisi/majengo yote ya umma bila kujali tofauti za rangi zao. Sambamba na hilo - fursa sawa kwa raia wote kuishi sehemu yoyote ya ardhi ya marekani bila ya kujali tofauti za rangi zao.
- AJIRA – Kutoa fursa sawa kwa raia wote kuajiriwa bila ya kujali tofauti zao rangi zao.
Kufuatia ushindi wake mkubwa kwenye uchaguzi wa Rais (1964) dhidi ya mgombea wa Republican (Garry Goldwater), Rais Johnson alitoa hotuba ya kusisimua mbele ya Taifa na kutangaza dhamira yake ya kuendelea kuleta mabadiliko makubwa zaidi. Kwa mfano, Rais Johnson alitangaza kuchukua hatua dhidi ya vikwazo vyote vilivyowanyima Wamarekani weusi kupiga kura. Wamarekani weusi walinyimwa haki kupiga kura kupitia mbinu kama vile:
- Literacy rates tests – yani kuwapa mitihani ya kupima uwezo wao wa kusoma na kuandika kabla ya kuwaruhusu wapige kura. Kwa kipindi kile wengi wao walikuwa bado hawana uwezo wa kusoma na kuandika.
- Kodi ya Kichwa – Kodi hii ilitumika kama ‘voting fee’ kwa wamarekani weusi kupiga kura, huku raia wengine wakipiga kura bila malipo/bure. Kwa kipindi kile Wamarekani weusi wengi hawakuwa na ajira zenye kuwawezesha kuwa na vipato vya kugharamia kodi husika.
Miswada hii miwili - Muswaada juu ya Kodi ya kichwa na ule wa Literacy Rates Tests, ilikuwa ni the ‘most comprehensive’ katika historia ya marekani, suala ambalo liliimarisha legacy ya Rais Lyndon Johson. Kwa mfano, ni kutokana na Sheria hizi mbili sio tu kwamba wamarekani weusi wameendelea kuwa ni ‘base’ kubwa na muhimu ya wapiga kura nchini Marekani, bali pia Marekani kama taifa lilifanikiwa kupata Rais wa kwanza mwenye asili ya watu weusi- Barrack Obama (2008 - 2016); na hata katika uchaguzi mkuu wa Rais (2020) Marekani ilifanikiwa kupata Makamu wa Rais mwanamke na mwenye asili ya watu weusi kwa mara ya kwanza, Makamu wa Rais Kamala Harris.
Tukiendelea kuangalia Legacy za Rais Lyndon Johnson, tunaangazia sheria zifuatazo:
- Sheria ya Kutokomeza Umaskini/Fursa Za Kiuchumi (1965)
- Sheria ya Shule za Msingi na Sekondari (1965)
- Sheria ya Elimu ya juu (1965).
Sheria ya Kutokomeza Umaskini (1965)
Rais Johnson aliendelea kupeleka miswaada mingi bungeni sambamba na kuanzisha programu mbalimbali zilizolenga kuinua maisha ya wanananchi walio wengi. Moja wapo ulikuwa ni ‘Muswada wa Fursa Za Kiuchumi’ ambao ulikuja kuzaa sheria iliyounda Programu ya ‘Job Corps & Community Action. Pamoja na mengineyo, programu hii ililenga kupunguza umaskini wa wananchi kwa kuzalisha ajira sambamba na matumizi ya fedha (kwa njia ya ruzuku) kusaidia ‘local communities’, ikilenga hasa
‘maendeleo ya watoto’. Jukumu hili lilisimamiwa na ofisi maalum iliyoanzishwa na Rais Johnson – Ofisi ya ‘Fursa Za Kiuchumi’. Ofisi hii pia ilipewa jukumu la kuhakikisha kwamba familia maskini zinapata uhakika wa chakula kupitia sheria iliyojulikana kama – the ‘Food Stamp ACT’ (1964).
Sheria ya Elimu Ya Msingi na Sekondari (1965)
Rais Lyndon Johnson pia alifahamu umuhimu na mchango wa sekta ya Elimu katika mapambano dhidi ya umaskini. Kwa mfano kupitia sheria ya Elimu ya Msingi na Sekondari (1965), serikali yake ilitenga jumla ya Dola za kimarekani Billioni Moja kwa ajili ya kuboresha mfumo wa elimu na kuja na programu maalumu ya elimu kwa ajili ya familia zilizokuwa zinaishi katika maeneo ambayo umaskini ulikuwa umekithiri.
Sheria ya Elimu ya Juu (1965)
Rais Johnson alihakikisha kwamba sekta ya elimu ya juu pia inapatiwa fedha za kutosha. Kwa mfano kupitia sheria ya Elimu ya Juu (1965) serikali yake ilitenga fedha nyingi kwa ajili ya ‘scholarship’ ikilenga zaidi familia maskini ili kutoa fursa za elimu ya juu (vyuo vikuu) kwa vijana ngazi ya vyuo vikuu. Sambamba na hilo, sheria ya Elimu ya Juu (1965) pia ilihakikisha kwamba mikopo ya elimu ya juu inapatikana kwa wingi na kwa riba nafuu.
Sekta ya Afya
Sambamba na Elimu, Rais Johnson pia alilenga kuboresha sekta ya Afya kwa kuanzisha ‘Medicare & Medicaid Programmes’, akilenga zaidi huduma bora za afya kwa wananchi maskini na wazee.
Hatima ya Urais Wa Lyndon Johnson
Pamoja na mafanikio makubwa ya urais wake ambayo hadi leo yameendelea kuacha legacy kubwa, urais wa Lyndon Johson uliishia kuwa ni wa muhula mmoja (1963 – 1969). Kama tulivyogusia awali, hilo halikutokana na zuio la kikatiba bali makosa yake mwenyewe ‘kisera’ akiwa Rais.
Makosa ya Kisera yaliyopelekea ndoto ya Lyndon Johnson kuwa Rais wa mihula miwili kuyeyuka yalitokana zaidi na maamuzi aliyochukua wakati wa Vita Vya Marekani nchini Vietnam (1964). Rais Johnson alifanya ‘controversial decisions’ nyingi ambazo zilipelekea taifa la Marekani kuingia kwenye vita ngumu na ndefu, iliyogharimu taifa la marekani maisha mengi na fedha nyingi za walipa kodi. Mbaya zaidi, ilikuja kufahamika kwamba Rais Johnson alidanganya taifa umma kuhusu “uhalisia na ukweli” wa vita vya Vietnam. Hii ndio iliyopelekea ‘approval ratings’ zake kama Rais kushuka kwa kasi, hivyo kupoteza mvuto wake kisiasa ndani na nje ya chama chake cha Democrat.
Kufuatia changamoto hizi, hatimaye Rais Lyndon Johnson akafikia uamuzi wa kutangazia chama chake na umma kwa ujumla kwamba hakuwa na nia ya kugombea kwa muhula wa pili. Ulipofika msimu mwingine wa uchaguzi mkuu wa Rais (1968), chama chake cha Democrat kikamchagua Hubert Humphrey kuwa mgombea urais. Ni chama cha upinzani cha Republican ndicho kilichoibuka mshindi kwa nafasi hiyo ya urais kupitia mgombea wake - Richard Nixon. Hata hivyo Rais Richard Nixxon nae aliishia kutawala kwa muhula mmoja baada ya kujiuzulu kufuatia kashfa ya ‘Watergate’. Kashfa hii ilihusisha wasaidizi wake ndani ya ikulu na pia chama chake cha Republican ambao walishutumiwa kuvamia ofisi za chama cha upinzani – chama cha Democrat, pamoja na kuhujumu viongozi wa chama hicho.
Kufikia hapa tumejifunza mambo makuu menne:
Kwanza tumejifunza kwamba asili ya urais wa Mama Samia Suluhu Hassan ni mfumo wa mgombea mwenza wa Marekani. Hii ni kutokana na mabadiliko ya kumi na moja ya Katiba ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kufuatia kazi ya tume ya Jaji Bomani miaka ya tisini. Tumejifunza mambo makuu matatu:
Pili tumejifunza kwamba Makamu wa Rais anaye rithi kiti cha uRais kufuatia kifo cha Rais aliyepo madarakani ana uwezo mkubwa wa kutengeneza legacy yake tofauti na yenye maslahi mapana kwa nchi na wananchi kwa ujumla. Tuliona hilo kwa kujadili urais wa Lyndon Johnson kufuatia kifo cha Rais JF Kennedy.
Tatu tumejifunza kwamba chini ya mfumo wa mgombea mwenza, makamu wa Rais hausiki moja kwa moja na maamuzi yote yanayofanywa na Rais wa nchi. Tuliona hilo kupitia mjadala wetu wa utawala wa Rais Franklin Roosevelt na Makamu wake Harry Truman.
Nne tumejifunza kwamba - Makamu wa rais anaporithi kiti kilichoachwa wazi na rais aliyefariki dunia ana nafasi ya kuendelea na kumaliza mihula yake miwili Kikatiba. Anaweza pia kukwama katika hilo, sio kutokana na zuio la Kikatiba bali maamuzi mabaya ya “kisera”, suala ambalo linaweza pelekea apoteze mvuto wake kisiasa na kuishia kuwa rais wa muhula mmoja. Tuliona hilo katika mjadala wetu juu ya urais wa Lyndon Johnson.
Katika sehemu inayofuata, tutajaribu kujadili uzoefu wa Marekani katika muktadha wa nchi yetu ya Tanzania. Tutaangazia zaidi utawala wa sasa wa Rais Samia Suluhu Hassan, hasa kwa kuangalia fursa na changamoto zinazomkabili.