Rais Kikwete ampongeza Anna Kilango kwa ujasiri dhidi ya ufisadi
Na Leon Bahati,
MWANANCHI, March 29, 2009
RAIS Jakaya Kikwete amempongeza Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango kwa kutunukiwa tuzo ya kimataifa ya Mwanamke Jasiri kwa mwaka 2009 na kwamba, ni ishara ya dunia kuutambua mchango wake katika kupambana na ufisadi nchini.
Taarifa iliyotolewa jana na Ikulu kwa vyombo vya habari, ilielezea kuwa Rais Kikwete alipokea kwa furaha kubwa habari za Kilango kutunukiwa tuzo hiyo.
Wiki hii, Kilango ambaye amekuwa mkali kwa kauli mbalimbali dhidi ya ufisadi, alikabidhiwa tuzo hiyo na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Larry André.
Tuzo hiyo ya mwaka ilianzishwa kwa lengo la kutambua na kuthamini mchango wa mwanamke aliyeonyesha ujasiri wa kiwango cha juu na uongozi mzuri.??Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania ulimteua Kilango kuwa mmojawapo kati ya washiriki waliowania Tuzo ya Kimataifa ya Mwanamke Jasiri ya Mwaka 2009, kutokana na ujasiri aliouonyesha katika kukosoa na kuupa changamoto uongozi wa chama chake ili uweze kushughulikia kikamilifu suala la rushwa. ??Kwa kufanya hivyo alivunja utamaduni wa kisiasa uliokuwa umejengeka bila kujali vitisho kwa usalama wake binafsi. Bila kuchoka wala kutetereka, alishikilia azma yake ya kupiga vita rushwa na kuuliza maswali mazito yaliyoibua mijadala iliyochangia sana katika jitihada za kuongeza uwazi na utawala bora ndani ya chama tawala.
Hatua ya Rais Kikwete kumpongeza Kilango ni pigo kubwa kwa kundi la wana CCM wanaodaiwa kujihusisha na vitendo vya ufisadi na imekuja wakati chama hicho kimegawanyika katika makundi mawili, lile linalotuhumiwa kwa ufisadi na lile la wanaoongoza mapambano dhidi yao, akiwamo mbunge huyo wa Same Mashariki.
Rais Kikwete aliielezea tuzo hiyo kama ni tunda linalotokana na Ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005 kuhusu vita dhidi ya rushwa.
"
CCM na serikali yake, vimetoa fursa pana zaidi kwa wananchi, wanahabari na viongozi, wakiwemo waheshimiwa wabunge, kushiriki kikamilifu zaidi," alisema Rais Kikwete kupitia taarifa hiyo na kuongeza:
"Kutunukiwa kwa tuzo hiyo ni ishara ya kutambua na kuthaminiwa kwa mchango wako katika mapambano dhidi ya rushwa."
Kilango ambaye ni mke wa mwanasiasa mkongwe, John Malecela, alikuwa miongoni mwa wabunge waliosimama kidete bungeni Februari mwaka jana kuhakikisha kuwa viongozi waliohusika katika mkataba tata wa Kampuni ya Richmond na serikali wanaadhibiwa.
Kashfa ya Richmond ilisababisha Waziri Mkuu, Edward Lowassa kujiuzulu na mawaziri wawili, Nazir Karamagi aliyekuwa akishikilia Wizara ya Nishati na Madini na Dk Ibrahim Msabaha aliyekuwa Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.