Na Kizitto Noya
UMOJA wa Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA), kwa kushirikiano na taasisi mbalimbali za kijamii na za Kutetea Haki za Binadamu, umepinga ziara ya Rais George Bush wa Marekani aliyewasili jana nchini.
Umoja huo ulieleza kutoridhika kwake na ziara ya rais huyo jana katika mdahalo wao ulioandaliwa kwa kushirikiana na wanaharakati hao kwenye Ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam sehemu ya Mlimani.
Akisoma tamko la pamoja, Mwenyekiti wa UDASA, Datmas Nyaoro, alisema Umoja wa Wanataaluma chuoni hapo unaamini kuwa kidemokrasia Tanzania haina jambo lolote jema la kujifunza kutokana na kuwa rafiki wa karibu wa rais huyo wa Marekani.
"Hii inatokana na ukweli kwamba, chini ya utawala wa Rais Bush, haki za Wamarekani weusi zimeendelea kuvunjwa, idadi ya wafungwa kutoka katika jamii za Wamarekani weusi imeongezeka huku huduma za kijamii hasa afya na elimu zikidorora," alisema.
Kwa mujibu wa UDASA, Tanzania haiwezi kuendelea kwa kutegemea ufadhili kutoka nchi zinazotoa misaada yenye masharti kandamizi kama Marekani, hivyo mkataba wa dola za Marekani 608 milioni unaotarajiwa kusainiwa kati ya Rais Bush na Tanzania akiwa nchini, hauna maana yoyote zaidi ya kuendeleza ukandamizaji huo.
"Tunaamini pia katika kujitegemea na kujitawala wenyewe. Kuongezeka kwa kiwango cha misaada kutoka Marekani katika kipindi hiki ambacho uchumi wake umedhoofika na upinzani dhidi ya ubabe wake umeongezeka, kunatufanya tuamini kwamba ufadhili huu una agenda ya siri ambayo ni Africom," aliendelea kusema Nyaoro.
UDASA ilitoa wito kwa Watanzania kulinda misingi ya uhuru na utaifa, kulinda na kutetea utu, haki, usawa, amani na umoja wa Afrika badala ya kuendelea kuikumbatia Marekani na kupoteza misingi iliyojengwa tangu enzi za mababu.
Awali wakizungumza katika mdahalo huo, baadhi ya wanaharakati na wawakilishi wa taasisi za kijamii walisema kuwa ziara ya Rais Bush nchini haina manufaa kwa Tanzania isipokuwa kwake binafsi na taifa lake la Marekani.
Kwa upande wake, Amiri wa Shura ya Maimam, Sheikh Ponda Issa Ponda, alisema ziara ya Bush nchini haina manufaa kwa Tanzania zaidi ya taifa kujitengenezea maadui kwa kuunga mkono sera ya ugaidi.
Alisema sheria ya ugaidi nchini inapaswa kuangaliwa upya kwani inapingana na sheria za nchi na ndiyo inayosababisha mapigano katika mataifa mengi duniani.
Hussein Mmasi wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema Bush hana utaratibu wa kufanya ziara zenye manufaa kwa nchi wenyeji na kuwa ziara hii ni mwendelezo wa utaratibu huo wenye misingi ya kuzinyonya nchi maskini.
Profesa Azaveli Lwaitama, Mhadhiri wa UDSM, aliitaka serikali kuchagua marafiki wa kweli wanaoweza kutoa ushauri wa haki kuhusu maendeleo yake badala ya marafiki wanafiki kama taifa la Marekani.
Alisema Rais Bush amekuja nchini kwa kivuli cha misaada, lakini ukweli ni kwamba ana agenda kubwa yenye masilahi binafsi na taifa lake.
Ndani ya ukumbi kulikofanyika mdahalo huo kulikuwa na mabango kadhaa yaliyoelezea hisia za wanaharakati hao juu ya ziara ya kiongozi huyo wa taifa kubwa duniani.
Baadhi ya mabango hayo yalisomeka 'Mfumo tulionao wa demokrasia wakilishi haufai, tunadai demokrasia shirikishi... Bush sitisha vita Iraq, Amani na Haki siyo vita'.