DEEP GREEN FINANCE COMPANY LIMITED
Mnamo tarehe 18 Machi 2004 ilianzishwa kampuni iitwayo Deep Green Finance Co. Ltd. kwa madhumuni ya, pamoja na mengine, kufanya biashara kama mabepari na wakopeshaji fedha! Kufuatana na taarifa za Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), wakurugenzi wa Deep Green Finance walikuwa ni mabwana Mark Ross Weston wa New Zealand; Anton Taljaard wa Afrika Kusini; na Rudolph van Schalkwyk pia wa Afrika Kusini. Wote watatu ni wakazi wa Afrika Kusini na wanaelekea kuwa ni maafisa na/au wafanyakazi wa Nedbank Ltd. ya Afrika Kusini. Kufuatana na taarifa za BRELA, wanahisa wa awali wa Deep Green Finance walikuwa ni mawakili Protase R.G. Ishengoma na Stella Ndikimi wa kampuni ya mawakili ya IMMMA Advocates; Nedbank Ltd., Nedbank Africa Investments Ltd. na SBM Nedcor Holdings Ltd. Tarehe 15 Aprili 2005 mawakili Ishengoma na Ndikimi walihamisha hisa zao kwa Nedbank Ltd. na Nedbank Africa Investments Ltd. IMMMA Advocates vile vile ni mawakili wa Tangold Ltd. ambayo imehusishwa na ufisadi tuliouelezea katika Orodha ya Mafisadi.
Taarifa za kibenki tulizonazo zinaonyesha kwamba tarehe 1 Mei 2004, Deep Green Finance ilifungua Akaunti Na. 011103024840 katika tawi la Corporate la Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), Dar es Salaam. Kitu cha kwanza cha kushangaza ni kwamba siku hiyo ilikuwa ni Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi) na ilikuwa siku ya mapumziko. Kitu cha pili cha kushangaza ni kwamba kampuni hii iliruhusiwa kufungua na kuendesha akaunti hiyo bila ya kuingiza wala kutoa fedha yoyote kwa zaidi ya mwaka mmoja kuanzia tarehe 1 Mei 2004 hadi tarehe 31 Julai 2005. Kitu cha tatu cha kushangaza ni kwamba pamoja jina la Deep Green Finance kuashiria kwamba kampuni hii ni taasisi ya kifedha, orodha ya taasisi za kifedha iliyotolewa na BOT tarehe 21 Agosti 2007 haionyeshi kwamba kampuni hii imewahi kusajiliwa na BOT kama taasisi ya kifedha!
Hata hivyo, kwa kipindi kifupi cha miezi minne kati ya Agosti 1 na Desemba 1, 2005 kampuni hii ilipokea jumla ya shilingi 10,484,005,815.39 kutoka Wizara ya Fedha na/au BOT. Fedha hizo zilitolewa kwa utaratibu ufuatao:
(a) Tarehe 1 Agosti 2005 BOT, kwa kutumia hundi Na. 241740, ilihamisha dola za Marekani 1,354,167.26 au shilingi za Tanzania 1,546,778,770.92 kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Siku hiyo hiyo fedha hizo zote zilichukuliwa kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwa utaratibu maalum wa haraka (special clearance) na kupelekwa mahali kusikojulikana na kwa madhumuni yasiyofahamika;
(b) Tarehe 1 Septemba 2005 BOT, kwa kutumia hundi Na. 015558, ilihamisha dola za Marekani 1,827,137.44 au shilingi za Tanzania 2,083,255,881.60 kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Siku hiyo hiyo jumla ya shilingi 2,083,333,333.33 zilichukuliwa kwa mara nyingine tena kwa kutumia utaratibu huo huo maalum wa haraka na kupelekwa kusikojulikana;
(c) Tarehe 8 Septemba 2005 Tangold Ltd. ilihamisha dola za Marekani 100,256.62 au shilingi za Tanzania 114,611,746.80 kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Itakumbukwa kwamba Tangold Ltd. ni kampuni ya kigeni iliyoandikishwa nchini Mauritius tarehe 5 Aprili 2005 na kupewa Cheti cha Kutimiza masharti ya Tanzania tarehe 20 Februari 2006. Hata hivyo, mawaziri kadhaa wa Serikali ya Rais Jakaya Kikwete wameendelea kudai kuwa kampuni hiyo inamilikiwa kwa asilimia mia moja na Serikali ya Tanzania. Wakurugenzi wa Tangold Ltd. ni Gavana Daudi Balali, Waziri wa Miundombinu Andrew Chenge, Katibu Mkuu (Fedha) Gray Mgonja, Katibu Mkuu (Maji) Patrick Rutabanzibwa na Katibu Mkuu (Ofisi ya Waziri Mkuu) Vincent Mrisho. Kufuatana na barua ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa BOT ya tarehe 21 Desemba 2006, Tangold Ltd. ililipwa na BOT dola za Marekani 13,736,628.73 kwa kupitia akaunti isiyojulikana ya Nedbank Ltd. ya Afrika Kusini na kwa madhumuni yasiyojulikana;
(d) Tarehe 16 Septemba 2005 jumla ya shilingi 129,000,000.00 zilitolewa kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance na kuwekwa kwenye akaunti ya muda maalum (FDR);
(e) Tarehe 3 Oktoba 2005 jumla ya shilingi 2,083,333,333.33 za Wizara ya Fedha zililipwa kwa utaratibu maalum wa haraka kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Inaelekea fedha hizo zililipwa kabla BOT haijaingiza fedha yoyote kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwa vile tarehe 4 Oktoba 2005 BOT ilihamisha dola za Marekani 1,789,075.89 au shilingi 2,083,891,765.35 kwenda kwenye akaunti hiyo;
(f) Tarehe 8 Oktoba 2005 jumla ya shilingi 39,761,397.98 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwenda Tangold Ltd.;
(g) Tarehe 31 Oktoba 2005 jumla ya shilingi za Tanzania 2,083,333,333.33 fedha za Wizara ya Fedha zilihamishiwa kwenye akaunti ya Deep Green Finance;
(h) Tarehe 2 Novemba 2005 dola za Marekani 1,821,095.57 au shilingi za Tanzania 2,083,653,279.68 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwenda kusikojulikana;
(i) Tarehe 30 Novemba 2005 BOT ilihamisha shilingi za Tanzania 2,083,333,333.33 zikiwa fedha za Wizara ya Fedha kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Siku moja baadaye, dola za Marekani 1,817,199.52 au shilingi za Tanzania 2,184,610,383.04 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwenda kusikojulikana;
(j) Tarehe 10 Desemba 2005 shilingi 100,940,489.71 zilihamishwa kutoka Tangold Ltd. kwenda kwenye akaunti ya Deep Green Finance. Hii ilikuwa ni siku nne tu kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Desemba 14, 2005 kufanyika nchini kote;
(k) Tarehe 19 Desemba 2005, siku tano baada ya Uchaguzi Mkuu kufanyika, dola za Marekani 88,722.17 au shilingi za Tanzania 104,755,554.09 zilihamishwa kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance kwenda kusikojulikana;
(l) Tarehe 9 Februari 2006 shilingi 3,836,800.00 zilihamishwa kwenda akaunti ya mawakili wa Deep Green Finance, IMMMA Advocates, iliyoko benki ya Standard Chartered. Haijulikani kama fedha hizi zilikuwa ni kwa ajili ya malipo ya mawakili hao au la;
(m) Malipo ya mwisho kutoka kwenye akaunti ya Deep Green Finance yalifanywa tarehe 22 Novemba 2006 ambapo jumla ya shilingi 14,465,000.00 zilihamishiwa katika akaunti isiyojulikana ya benki ya Standard Chartered na kwa matumizi yasiyojulikana;
Kutokana na rekodi za kibenki zilizoonyeshwa hapo juu, jumla ya shilingi 10,484,005.39 ziliingizwa katika akaunti ya Deep Green Finance katika kipindi cha miezi minne tu kati ya tarehe 1 Agosti na 10 Desemba 2005. Hiki kilikuwa ni kipindi cha mchakato na/au kampeni za Uchaguzi Mkuu uliofanyika tarehe 14 Desemba 2005. Aidha, kuanzia tarehe 11 Desemba 2005 hakuna fedha yoyote iliyoingizwa katika akaunti hiyo hadi tarehe 27 Februari 2007 kampuni hiyo ilipovunjwa kwa hiari ya wanahisa wake. Ni muhimu kurudia kwamba, kwa ushahidi huu wa nyaraka za kibenki, kampuni ya Deep Green Finance haikuwa na hata senti moja kabla ya tarehe 1 Agosti 2005 na wala haikupokea hata thumni mara baada ya tarehe 10 Desemba 2005 na mara baada ya Uchaguzi Mkuu.
Kwa taarifa za sasa hivi, inafahamika kwamba faili la Deep Green Finance lililotakiwa kuwa BRELA limetoweka. Tuna kila sababu ya kuamini kwamba hii ilikuwa ni kampuni hewa (shell company) iliyoundwa kwa ajili tu ya kupitishia fedha za umma kutoka Benki Kuu kwenda kusikojulikana wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2005. Ndio maana kampuni hiyo haikuwa na fedha zozote benki kutokea tarehe 1 Mei 2004 hadi tarehe 1 Agosti 2005, wiki tatu kabla ya kuanza kwa kampeni za Uchaguzi Mkuu. Na ndio maana mabilioni iliyolipwa na Benki Kuu yalilipwa wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu na mara baada ya Uchaguzi Mkuu kupita malipo hayo ya fedha za umma yalikoma.