Hivi karibuni Mbunge wa Kigoma Kaskazini Mhe. ZITTO KABWE wakati akiwa katika chakuka cha jioni alichoandaliwa na Watanzania waishio katika Jimbo la Michigan (Marekani) aliwaeleza Watanzania hao kuwa Sheria ya uundwaji wa Idara ya Usalama wa Taifa Na. 15 ya mwaka 1996 imeifanya Idara hiyo kuwa butu na kwa hiyo ipo haja na ulazima wa kuipitia na kuifanyia marekebisho. Kauli ya Mbunge huyo ililenga kuonyesha kwamba ubutu wa Idara ya Usalama wa Taifa ni ule wa kushindwa kukabiliana na vitendo vya kifisadi.
Kauli hiyo ya ZITTO ilinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari likiwemo gazeti la Tanzania Daima la tarehe 8 Mei, 2008. Kimsingi, shutuma za namna hiyo kwa Idara ya Usalama wa Taifa zimekuwa zikitolewa mara nyingi hasa tangu vitendo vya kifisadi kuanza kuitikisa nchi.
Kauli hiyo ya Mhe. ZITTO KABWE pamoja na lawama zinazotolewa kwa Idara ya Usalama wa Taifa zinapaswa kuangaliwa kwa mapana hasa kwa kuzingatia kuwa nchi yetu ya Tanzania inafuata mfumo wa utawala unaoitwa Parliamentary system of government ambao chimbuko lake ni Uingereza. Ndani ya mfumo huo kuna mihimili mitatu ya dola yaani Serikali (executive), Bunge na Mahakama. Katika mfumo huo Serikali inakuwa moja kwa moja ni sehemu ya Bunge, lengo likiwa ni kulifanya Bunge na Serikali kuwa ni vyombo vinavyotegemeana na kwa hiyo vinapaswa kufanya kazi zao kwa ushirikiano mzuri ili kuweza kufikia lengo la kuwaletea wananchi maendeleo na ustawi wa jamii.
Ni vyema pia tutambue kuwa wajibu wa Bunge ni kuisimamia na kuishauri Serikali na vyombo vyake vyote katika utekelezaji wa majukumu yake kama Ibara ya 63(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inavyoeleza. Kwa mujibu wa masharti ya Ibara ya 63(3) ya Katiba hiyo, Bunge linasimamia utekelezaji unaofanywa na Serikali kwa kutumia njia ya kuwauliza Mawaziri maswali Bungeni kuhusu utekelezaji unaofanywa na Wizara, halikadhalika kujadili utekelezaji wa kila wizara uliofanywa katika mwaka uliotangulia pamoja na kutoa ushauri unaofaa kuzingatiwa katika mwaka wa fedha unaofuata.
Aidha, ni wajibu wa Bunge kuiwezesha Serikali kutekeleza wajibu wake kwa wananchi kwa kutunga Sheria na kupitisha bajeti. Hatua hiyo ndiyo inayoiwezesha au kuirahisishia Serikali kutekeleza majukumu yake.
Vivyo hivyo, kwa upande wa Mahakama kama muhimili wa tatu, majukumu yake yemeelezwa bayana katika Ibara ya 107 A na 107 B ya Katiba. Kwa mujibu wa Ibara hiyo, mamlaka ya utoaji wa haki katika Jamhuri ya Muungano itakuwa mikononi mwa Idara ya Mahakama na katika kutekeleza mamlaka ya utoaji haki Mahakama zote zitakuwa huru na zitalazimika kuzingatia tu masharti ya Katiba na Sheria za nchi. Kwa maneno mengine Bunge ni chombo cha uwezeshaji kwa Mahakama. Kwamba, Bunge linao wajibu kutunga Sheria zitakazowezesha Mahakama kutekeleza ipasavyo shughuli zake za utoaji haki, kwani bila Bunge kutunga Sheria mbali mbali Mahakama haitaweza kutimiza wajibu wake wa utoaji haki.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa hapo juu ni kwamba, Bunge ni chombo cha uwezeshaji kwa Serikali na kwa Mahakama. Dhana ya utengano wa madaraka baina ya mihimili hiyo mitatu ya Dola, haipo kikamilifu katika mfumo wa utawala unaitwa Parliamentary System of Government:, badala yake kuna maingiliano na ushirikiano mkubwa wa kimadaraka miongoni mwa mihimili hiyo.
Kwa kuzingatia ukweli huo, je, ni sahihi kuilaumu serikali (executive) peke yake au Idara ya Usalama wa Taifa kwa kushindwa kukabiliana na vitendo vya kifisadi? Kwa nini watu wamekuwa wepesi kuilaumu Serikali (executive) na wamekuwa bubu kwa mihimili mingine ya dola? Je, Bunge pamoja na wabunge wake akiwemo ZITTO KABWE ambao wanailaumu serikali hasa Idara ya Usalama wa Taifa walikuwa wakifanya nini katika kuisimamia serikali vizuri ili kuweza kuondokana na vitendo vya kifisadi? Mbunge ZITTO KABWE anaposema Idara ya Usalama wa Taifa ni butu kutokana na sheria iliyoiunda, anategemea nani atarekebisha sheria hiyo? Sambamba na hilo, sheria hiyo ni ya mwaka 1996, kwa kipindi hicho chote ZITTO KABWE hakutambua kasoro ya sheria hiyo hadi leo mwaka 2008? Je ni kweli anatimiza ipasavyo wajibu wake kama Mbunge?
Kwa maoni yangu, mihimili yote mitatu inapaswa kushutumiwa na kunyoshewa vidole vya lawama kutokana na kukithiri kwa vitendo vya kifisadi na siyo serikali (executive) au Idara ya Usalama wa Taifa peke yake. Ni ukweli usiopingika kwamba kushindwa kuwajibika ipasavyo kwa mihimili hiyo mitatu ndiko kulikotufikisha hapa tulipo.
Wanasiasa (Wabunge) akiwemo ZITTO KABWE wasikwepe lawama wanazopaswa kuzibeba kwa uzembe walioufanya. Kama kweli wanathamini dhamana waliyoibeba wanapaswa kwenda kwa wananchi na kuomba radhi (msamaha) kwa uzembe waliofanya ambao umesababisha kukithiri kwa vitendo vya kifisadi ambavyo vimesababisha maisha magumu kwa wananchi waliowachagua. Wabunge hawana haki ya kuilaumu serikali au Idara ya Usalama wa Taifa peke yake, bali wao pia pamoja na Idara ya Mahakama wanapaswa kulaumiwa. Kuilaumu Idara ya Usalama wa Taifa au sheria inayoiunda ni kuitoa kafara kwa makosa ambayo si yake.