Naandika nikiamini kwa namna moja au nyingine ushauri huu utamfikia huyu kijana Diamond. Yeyote asiye na maelewano na wazazi/mzazi wake pia inamuhusu. Na wazazi wanaotelekeza vizazi vyao pia wanaweza kujifunza jambo.
Mimi ni mmoja kati ya watu wanaopenda namna Diamond anavyojituma katika kazi pamoja na ubunifu katika muziki na biashara ya muziki. Pia amekuwa mstari wa mbele kusaidia vijana wenzake, hususan waliotoka katika hali duni kimaisha kama ilivyokuwa kwake, kupata maendeleo kupitia sanaa. Tumeshuhudia hali kadhalika mara kadhaa akirudi maskani Tandale na kuwasaidia wakazi wa huko, kidogo alicho jaaliwa, na mengine mengi mazuri.
Yapo pia mambo kadhaa ambayo sifurahishwi nayo kuhusu yeye, lakini nitalizungumzia hili la kumtelekeza Baba yake. Nimeona mahojiano ambayo baba Diamond amefanya na online TV moja. Ni wazi kwamba huyu mzee alitibuana na demu wake Sandra - mama Diamond, akatimka nyumbani na kutelekeza familia. Anasema wakati huo Diamond alikuwa na akili yake nzuri tu, hivyo huenda Diamond aliathirika sana kisaikolojia kwa Baba yake kutokomea kusikojulikana na kuwaacha yeye na mama yake hawana hata unga robo. Kutokana na maelezo yake aliyotoa na mazingira ya nyumbani kwake, huyu mzee ana hali ngumu. Baba Diamond sasa hivi anafanya biashara ya kukopa viatu vya mtumba Ilala, anarudi kwake magomeni anaviosha na kung'arisha kisha anatembeza mtaani, yaani Mmachinga typical. Anapoumwa kwa mfano, anakuwa hana hata fedha ya matibabu, hivyo kugeuka ombaomba. Kutokana na maelezo ya Mzee mwenyewe, majirani na mdogo wake Diamond anayeishi na baba yake, Diamond kufika kwa mzee wake ni tokea yuko na Wema!
Kilichonifanya kuandika huu uzi ni kwamba Baba Diamond ameomba msamaha kwa makosa aliyoyafanya. Tena amesema kwa uchungu kabisa, kwamba hata Mwenyezi Mungu husamehe. Kwa nini , yeye asisamehewe?. Binafsi naona imefika wakati Diamond akunjue moyo wake na kumsaidia Baba yake. Katika Qur'an, ipo wazi kabisa, kwamba baada ya Mwenyezi Mungu, wanafuata wazazi. "Be grateful to Me and to your parents; to Me is the [final] destination." (
Quran 31:14). Mzee Abdul alikosea kumtelekeza mtoto Diamond, haijalishi walitibuana nini na mama Diamond. Diamond hajui nini hasa kilitokea. Mzee ameomba msamaha, anapaswa kusamehewa na maisha yaendelee.
Diamond rudisha maelewano na umsaidie baba yako. Amejutia na ameomba msamaha. Kwa sasa haikupunguzii chochote kumsaidia mzee wako aishi maisha ya kawaida, ya angalau ajue familia yake itakula nini jioni. Utakuwa na amani, Itakuongezea heshima katika jamii, na zaidi utapata credit kwenye daftari lako la Akhera. Maisha yenyewe ndiyo haya. Ukiishi sana 80. Ukiishi zaidi ya 80 ni maumivu tu, uwe na hela au huna. Akifa huyu mzee katika hali hii, Diamond utaaibika Duniani na akhera.