S3 epi 21
Kiutani utani ndani ya selo Sasa, kachumba kenyewe kadogo watu wamejaa balaa, wengine majeruhi mtu ana majeraha mabichi kabisa yupo ndani kule, nikatafuta angle Moja nikawa nimetulia, dah hapo nawaza Sana Leo hii nimekua mtu wa selo tena, sikukaa Sana Kuna jamaa nae akaingizwa hapo selo, Sasa sijui ni nini ye tangia aingie anapiga kelele tu anaita askari kule kaunta, aisee jamaa wakaanza kumpiga Sasa, jamaa anapigwa damu zinatiririka tu mpaka askari wakaja wakamchukua, jamaa kule ndani wanalalamika " huyu mrembo kaja kutupigia kelele hapa" Sasa hapo ndo nikapata akili huku sio kukaa kilele mama, muda wowote unaweza kuchezea kichapo....
Hapo Sasa nawaza jamaa niliyekuja nae atafanya mambo ntatoka, usiku ushaingia hapo, badae naskia naitwa nikasema afadhali hapa nifanye mpango nitoke tu Sasa, kufika pale counter nashangaa jamaa kaniletea chakula pale, nikachoka!!! Huyu badala ya kuja kunitoa ndo kwanza ananiletea chakula mbona kazi ipo hapa, jamaa wakamuamuru aonje kile chakula kwanza, badae kuna askari wa kike pale akaniambia kula harakaharaka kijeshi ukienda nacho kula kule hataambulia kitu, hapo Sasa hata hamu ya kula ninayo basi, nikamuuliza jamaa vipi hujafanya mpango wa kunitoa? Jamaa ndo ananiambia ameambiwa afande mwenye faili langu Wala hata hayupo na mkuu wa kituo hayupo ngoma mpaka kesho hio, nikavuta pumzi pale nikasema kazi ipo
Nikachukua ule msosi hata sikula nikarudi nao tu selo nikasema acha jamaa wakale, kufika Sasa chakula kiligombaniwa zaidi ya mpira wa kona dakika si nyingi hola, nimekaa zangu pembeni tu pale Kuna jamaa akanifata
Jamaa: " mwamba una ishu gani?"
Sasa sikutaka story nyingi na mtu nikamuambia Kuna mtu tu tumetofautiana nimemuumiza kidogo, akawa ananipa moyo we utatoka tu hata kesho sisi wengine tuna ishu nzito na Hawa jamaa hata mahakamani hawatupeleki..... Aisee mbu wa selo sio wa kawaida.... Wale ni kama walitengenezwa maabara flani wakapewa mafunzo ndo wakatupiwa kule selo, huo usiku sikulala ulikua wa mateso makubwa, nawaza nisingefanya upumbavu kule dar Leo hii nisingekua hata hapa, basi tu
Usiku ukawa kama wiki vile hatimae pakapambazuka, mida ya saa 4 akaja yule jamaa Sasa na mfanyakazi mwingine yeye alikua mkubwa kwetu kikazi, nikaja kuitwa, nikatolewa kule Sasa nikajua hapa nishatoka, kumbe ngoma Bado mbichi, jamaa nadhani Kuna Hela walitoa nikahamishwa tu selo, nikapelekwa selo za kule nyuma nadhani wanaita vip, kule kweupe hakuna mtu Wala nini, nikaingizwa kule jamaa nikawa naongea nao kupitia grill zile, basi kula nikakataa nikanywa maji tu pale.....
Jamaa nauliza nini kinaendelea wanasema Kila wanayemfata wanaelekezwa faili lipo Kwa afande flani, wakimpigia anasema anakuja ila ndo hivo hata hafiki, tukakaa pale yule afande akaja, wakawa Sasa wanamuambia waniwekee mdhamana pale, jamaa akaanza kufoka " hivi nyie mmemuona Binti alivyoumia au mnachukulia mambo kirahisi tu"
Yule jamaa mwingine wa kazini akawa anamuambia huyo Binti yupo wapi tuongee nae, wakamuita Rachel pale kweli alikua kaumia Kuna upande juu ya jicho alikua kapasuka.... Hapo tunaangaliana tu mie basi Nina hasira zangu, jamaa wakatoka nae wakaenda kuongea nje huko..... Badae wanarudi wanasema Binti haelewi, anasema ukae tu huko ndani mpaka ajiangalie Hali yake ikoje ndo atoe maamuzi, hapo nina hasira nawaambia msimbembeleze kama vipi nyie niacheni tu huku, jamaa wakarudi ongea Sana na yule afande wapi bana wanazungushwa tu, mpaka wakaenda Kwa mkuu wa kituo sijakaa sawa naona wamekuja nae, mkuu wa kituo ananiuliza una shida gani nikamuelezea pale akasema subiri.....
Kama ilivyo ada pale jamaa wakatoa 'chochote kitu' mmoja wao akanidhamini pale, ila Kwa masharti Sasa haya
i) nimlipe Rachel gharama alizotumia kujitibisha, hapo pia nitaendelea kumtibisha mpaka apone kabisa
ii) nikae nae chini tuone namna gani tunaweza kumaliza hio kesi Ili yeye ndo aje aifute, tofauti na hapo kesi inaenda mahakamani
Nikatoka pale nina hasira kichizi, nikajua hapa ndo nimemaliza huyu acha nikampe hio pesa mengine tutajua mbele Kwa mbele, kumbe bana ngoma Bado mbichi, natoka pale mara naitwa Kuna kitengo Cha ustawi wa jamii walikua na jengo pembeni pale, kule Nakuta madai Rachel anataka Sasa mtoto, nikasema huyu kaniamulia Leo, yeye hapo kashajieleza alafu wale watu walikua wadada tu, nikaanza kuchambwa Sasa kule ndani mada kubwa wanaongelea nimezaa na mdogo wake Rachel, hapo Nina hasira nataka kuharibu tu kule ndani maana naona Hawa wananifanya kama mtoto mdogo, ila nikiwawaza wale mbu nikasema acha niwe mpole, wakachukua maelezo pale wakasema msipoelewana mtaenda mahakamani wataamua kule kule....wale watu wa ustawi wakachukua namba zangu tukaruhusiwa
Tukatoka pale Kuna pesa Rachel aliandikisha ametumia nikaongea na jamaa yangu akawa amempa tukaondoka, mimi hapo sitaki hata kuongea nae, jamaa yule tuliyekuja nae siku Ile tukaongozana mpaka home, yule mwingine akaondoka zake, Sasa hapo jamaa Simu aliweka ndege, so hakuna anayejua Nina msala gani, Rachel nadhani alimwambia mama mkwe ila G Hajui chochote hapo...
Nafika home Sasa Nakuta G hapo alikua kajiandaa, akapanic ananiuliza "kuna nini hupatkani ulikua wapi? Hapa nilikua nasubiri usafari Nije kukuangalia kazini" nikamuambia acha tu Jana nimelala kituoni ila tutaongea badae, maswali yakawa mengi Sasa ikabidi niweke tu ukauzu nikamwambia nishakuambia tutaongea hebu niache, uzuri huyu Binti alikua ananiheshimu Sana na ka uoga flani akaniambia sawa hakuna shida.....
Sasa sijui ni Imani gani yule jamaa wangu akanitolea sijui ni magadi sijui chumvi ya mawe akaniambia kaogee hii mwanangu, selo Pana mikosi Sana, mimi hata bila kuelewa nikaenda oga na Yale madude, kurudi jamaa alishaomba zile nguo nilizovaa na viatu Nakuta kashazitia kiberiti hapo nabaki nashangaa tu sielewi....
Imefika jioni Sasa wale wadada wa ustawi wakancheki, wakaniambia niwakute Kuna baa ipo karibu na pale pale polisi, nikaenda mshkaji tukawa tumeachana nae, nafika kule wale wadada wanakula zao bia pale Ile nafika tu wananiambia hebu nunua bia kwanza, nikawaongeza bia pale na mimi nikachukua yangu Kali tukaanza pale mazungumzo, aisee hakuna watu Wana midomo mchafu kama Hawa wadada, yaani hawana hata aibu, wakawa wananishauri Sasa " kaka unafeli wapi, yule mlishavuliana nguo, ukitaka suluhu ya haraka muite mahali Mt**mbe tu Wala hatakua na jipya, wanawake tunajijua udhaifu wetu"
Sasa tumekaa pale naona hakuna hata la maana walioniitia, mara yule afande aliyekua na faili langu akawa kama anapita akaniona, jamaa hata aibu Hana akifika pale anajichekesha tu kaagiza kinywaji anamuambia mhudumu jamaa atalipa, basi akawa analalamika tumemzunguka Kwa bosi wake, hapo mi namchora tu, basi at least Sasa huyu jamaa akanishauri Sana nifanye mpango nimalizane na Rachel maana mambo ya mahakamani ni kupoteza muda alafu kule hawana mzaha mnaweza kwenda siku hakimu akawa anagawa dozi(vifungo tu) hio siku.... Nikawaza Sana nikasema hapa inabidi niwe mpole maana Rachel Nina misala nae miwili, hili la kesi Bado Kuna mambo ya mtoto hapo
Nikanyanyua Simu, hapo sitaki kumshirikisha mtu yoyote, nikamtoa kwanza Rachel blacklist kule, nikampigia hapo nimekua mpole kweli, akaanza kujichekesha tu ananiambia naona Leo umenikumbuka.... Nikawa namsihi pale tuangalie namna ya kumaliza haya mambo Kwa amani maana tukiendelea kugombana mtoto ndo atakuja kupata shida , akanikatisha pale anasema "wee, hayo sio mambo ya kuongea kwenye Simu, tafuta muda tukutane tuongee"