Mkutano uliopita wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika FOCAC uliofanyika mwezi Septemba mjini Beijing, kaulimbiu ya “Kuungana Mkono ili kuendeleza Usasa na Kujenga Jumuiya yenye mustakabali wa Pamoja ya China na Afrika”, ilifuatiliwa na kuchambuliwa na wataalam na wanazuoni mbalimbali wa ushirikiano wa kimataifa, na hasa wale wa ushirikiano kati ya China na Afrika.
Hoja na maoni mengi kwenye uchambuzi huo, ni kuwa kuna China na Afrika zinashikana mkono kuelekea kwenye mambo ya usasa.
Katika kipindi cha zaidi ya miongo miwili ya ushirikiano kati ya China na Afrika chini ya utaratibu wa FOCAC, na mipango mingine ya ushirikiano wa pande mbili kati ya China na Afrika, ni wazi kuwa eneo la uchumi limekuwa na mafanikio.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kuhusu makadirio ya ongezeko la uchumi duniani kwa mwaka 2024, kati ya nchi na sehemu 20 duniani zinazotajwa kuwa na ongezeko la kasi la uchumi duniani, nchi 11 ni za Afrika, zikiwa ni pamoja na Burundi, Ethiopia, Rwanda na Tanzania, ambazo wastani wa ongezeko lake la uchumi ni kati ya asilimia 6 na 7, juu ya wastani wa dunia wa karibu asilimia 3.
Soma Pia: Ajenda ya mwaka 2063 ya Umoja wa Afrika na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika kuhimiza mafungamano China na Afrika
Kwa wanaofuatilia kwa karibu uhusiano kati ya China na Afrika, huenda ongezeko la uchumi kwa nchi za Afrika kutokana na fursa zinazopatikana kwenye ushirikiano na China pengine si jambo jipya, kwani ni takwimu ambazo zimekuwa zikitajwa mara kwa mara.
Kipengele cha usasa kutokana na ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika ni kitu ambacho hakijatajwa sana, licha ya ukweli kwamba ushirikiano na China umehimiza usasa kwenye nchi za Afrika katika maeneo mengi.
Kwenye suala la miundo mbinu, kwa sasa limekuwa ni jambo la kawaida kuona barabara za kisasa za kiwango cha kimataifa, hospitali za kisasa za kiwango cha kimataifa, hata majumba ya kisasa ya mikutano ya kimataifa, vituo vya kisasa vya kuzalisha umeme kwa nishati mbadala, ambavyo ni matokeo ya ushirikiano kati ya China na Afrika, na visingeweza kujengwa kirahisi kwa muundo au kwa taratibu za ushirikiano zilizopo sasa kati ya Afrika na nchi za magharibi.
Mbali na miradi mikubwa ya kitaifa kama vile miundombinu na majengo makubwa ya kisasa, maisha ya mtu mmoja mmoja wa Afrika sasa yamekuwa yakiendelea kuwa bora, kutokana na ushirikiano wa kibiashara kati ya China na nchi za Afrika.
Kwa sasa limekuwa ni jambo la kawaida kwa watu wa kawaida kabisa wa nchi za Afrika kutumia vifaa vya kisasa vya elektroniki, ambavyo zamani ni wale tu waliokuwa wenye bahati ya kwenda Ulaya na Marekani ndio waliweza kuwa navyo.
Iwe ni simu za mkononi, vifaa vya matumizi ya nyumbani kama televisheni, majiko ya kupikia, Kompyuta na huduma ya internet ya njia pana (broadband), vitu hivi sasa vinaweza kupatikana barani Afrika kwa bei nafuu na ubora unaofaa, kutokana na ushirikiano kati ya China na Afrika.
Dhana ya usasa kwa mujibu wa tafsiri ya kimagharibi, ni dhana ambayo inahitaji muda mrefu sana kufikiwa. Nadharia inayohusu usasa iliyotolewa na mchumi wa Marekani Walt Rostow, inataja njia ndefu yenye hatua tano, inayoanza na jamii ya jadi na kupita hatua nyingine tatu hadi kufikia usasa.
Lakini kufuata njia yake kuna maana kuwa watu wa nchi za dunia ya tatu, wanahitaji mamia ya miaka kuvuka hatua moja, na kama nchi hizo zikifuata nadharia yake, basi kufikia usasa itakuwa ni ndoto.
Kupitia ushirikiano kati ya China na Afrika, usasa sio ndoto tena, bali ni jambo linalojadilika na kuwekewa mikakati, na tayari dalili zinaonekana, na kwamba kuungana mkono katika kufikia hatua hiyo tayari kunaonesha matokeo.