China ni nchi kubwa inayoendelea ambayo imekuwa na ushirikiano wa karibu na nchi nyingine zinazoendelea, zikiwemo za Afrika. Ushirikiano huu unajumuisha sekta mbalimbali ikiwemo elimu, uchumi na biashara, utamaduni, ujenzi wa miradi mikubwa ya miundombinu, na pia mabadilishano ya watu na watu.
Katika nchi nyingi za Afrika hivi sasa kuna maendeleo makubwa katika sekta ya miundombinu hususan ya barabara, reli, madaraja, bandari na viwanja vya ndege. Tukitolea mfano ujenzi wa barabara kuu ya Nairobi ama Nairobi Expressway, reli ya SGR kati ya Ethiopia na Djibouti, ambayo ni reli ya kwanza ya kisasa inayounganisha nchi mbili barani Afrika, na pia ukarabati wa bandari ya Lamu nchini Kenya, ambayo imesaidia katika kupunguza msongamano katika bandari ya Mombasa nchini humo.
Nchini Namibia, ushirikiano katika sekta ya baharini kati ya nchi hiyo na China umeendelea kupata matunda makubwa, na kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa nchi hiyo na kuboresha maisha ya watu.
Namibia ina bandari kubwa mbili, ambazo ni Walvis Bay na Luderitz, ambazo zote ziko chini ya Mamlaka ya Bandari ya Namibia, na zinatumika kama malango kwa nchi zisizo na bahari kusini mwa Afrika, hususan Zimbabwe, Botswana, na Zambia.
Akizungumza katika mahojiano na Shirika la Habari la China Xinhua hivi karibuni, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Bandari ya Namibia Andrew Kanime amesema, kituo cha kontena cha bandari ya Walvis Bay, iliyojengwa na Kampuni ya Uhandisi wa Bandari ya China (CHEC) na kuzinduliwa mwaka 2019, kimechukua nafasi muhimu katika mageuzi ya uwezo wa kushughulikia mizigo kwenye Bandari hiyo.
Karime anasema, mradi huo umekuwa na athari chanya sio tu kwa bandari ya Namibia, bali kwa Namibia na kanda hiyo kwa ujumla, kwa sababu kituo hicho kimewezesha bandari hiyo kuongeza uwezo wa kushughulikia mizigo kwa mara mbili zaidi kuliko kipindi cha nyuma.
Mradi huo unatarajiwa kuendelea kuwa na athari chanya kwa cuhumi wa Namibia na maisha ya watu wengi, wakiwemo sio tu wafanyakazi wa bandarini hapo, bali pia wale watakaofaidika kutokana na viwanda vitakavyojengwa kutokana na kuongezeka kidhahiri kwa wingi wa mizigo ambayo inashughulikiwa sasa kupitia Bandari ya Walvis Bay.
Uhamishaji wa ujuzi na teknolojia pia ni jambo lingine ambalo China inafanya katika ushirikiano wake nan chi nyingine zinazoendelea. Karime anasema, ili kuondoa pengo la ujuzi na uwezo katika soko la kazi, jambo muhimu zaidi katika uratibu wa kimataifa ni uhamishaji wa ujuzi. Amesifu mchakato mzima wa uhamishaji wa ujuzi wakati wa ujenzi wa Bandari hiyo kwa kutumia kreni zilizonunuliwa kutoka kampuni ya ZPMC ya Shanghai. Amesema mafundi kutoka kampuni hiyo walitoa mafunzo kwa wazawa nchini Namibia katika kuendesha na kufanya marekebisho ya mashine hizo, na kuongeza kuwa, ingawa mafundi hao wamerejea China, lakini mashine hizo zinaendelea kuendeshwa na kufanyiwa marekebisho na timu za Namibia.
Mambo haya yanaonyesha ushirikiano wa miongo mingi kati ya China na Namibia na China na Afrika, na kuashiria uratibu zaidi kati ya pande hizo mbili katika sekta nyingine.