Rais mteule wa Marekani Donald Trump akiwa sasa yupo kwenye maandilizi ya kurejea tena kushika usukani na kuliongoza taifa la Marekani Januari mwaka 2025, ameanza kujenga uhasama na nchi washirika wake wa kibiashara kwa kutoa vitisho kwa nchi mbalimbali duniani, huku akitilia mkazo sera ya Marekani kwanza lazima iheshimiwe na watu wote duniani.
Kitendo hicho cha Trump kina uwezekano mkubwa wa kuzusha mzozo kuhusu sera ya nje ya Marekani, hasa kutokana na sifa aliyoionesha wakati alipokuwa akiiongoza Marekani katika muhula wake wa kwanza, ambapo alivuruga hali yoyote ya utulivu iliyopo, na sasa ameshaanza tena kuonesha makali na cheche zake.
Ni hivi majuzi tu alianza kutoa vitisho vyake kwa washirika wakubwa wa kibiashara wa Marekani wakiwemo Mexico, Canada na China akisema kwamba atakapoanza kazi rasmi basi atazitoza ushuru mpya nchi hizo kama sehemu ya juhudi zake za kukabiliana na wahamiaji haramu na dawa za kulevya. Alisema atatoza ushuru wa 25% kwa bidhaa zote zinazoingia nchini Marekani kutoka Canada na Mexico, na ushuru wa ziada wa 10% kwa bidhaa kutoka China, kama moja ya maagizo yake ya kwanza ya utendaji.
Hata hivyo anachosahau Trump ni kwamba kama vitisho hivi vikiwa ni vya kweli, basi sio tu nchi alizozilenga ndio zitaathirika, bali hata nchi nyingine duniani ikiwemo na hata Marekani yenyewe. Kwa Marekani athari hii itaonekana kwenye maduka makubwa yanayofika bidhaa hizo zikiwemo Supermarket, migahawa hata makampuni yake ya ndani. Vilevile wateja wa Marekani na wafanyabiashara ambao watalazimika kufuata muswada huo pia watajikuta kwenye wakati mgumu.
Ushuru wa Trump unakusudiwa kuishinikiza Canada na Mexico juu ya sera yake ya mpaka, na kwa upande wa China unalenga kuiporomosha kiuchumi. Lakini matokeo ya kutekeleza sera hiyo ni kwamba Marekani huenda ikaishia kujipiga risasi yenyewe mguuni, kwani kwa sasa China bila shaka tayari imeshinda raundi hii ya kwanza. Ushuru wa ziada wa 10% kwa bidhaa kutoka China ambazo Trump alitishia Jumatatu ni sehemu tu ya ushuru wa 60% aliokuwa akiutaja wakati wa kampeni zake kabla ya kuchaguliwa kuwa rais.
Kwa kuzingatia hilo, ubalozi wa China mjini Washington ulitahadharisha kwamba iwapo kutakuwa na vita vya kibiashara ama vita vya ushuru basi hakuna atakayeshinda. Ukisisitiza kuwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Marekani una manufaa kwa pande zote.
Kama hayo hayatoshi Trump pia ametishia kutoza ushuru wa asilimia 100 kwa kundi la mataifa tisa la BRICS, ikiwa watajaribu kubadilisha dola ya Marekani na kutumia sarafu nyingine. Hatua hii imekosolewa sana na baadhi ya wataalam wa Marekani wakisema tishio la Trump la kuiadhibu BRICS, linaifanya Marekani ionekane dhaifu sana.
Ni kweli tishio hilo halileti sura nzuri hata kidogo, kwani ni sawa na kukiri kwamba dunia sasa imekosa imani na dola ya Marekani, na kwa upande mwingine linafanya nchi za BRICS ambazo sio tishio kwa Marekani wala nchi yoyote ile kuinuka hadhi yake duniani.
Mbali na hapo Marekani ikitekeleza ushuru wa 100% dhidi ya nchi za BRICS kwa hakika hautakuwa na manufaa kwa wateja wa Marekani, matokeo yake ni kwamba gharama za bidhaa kutoka mataifa wanachama wa BRICS zikiwemo kahawa kutoka Brazili, vifaa vya elektroniki na nguo kutoka China, na madini kutoka Afrika Kusini zitaongezeka na hivyo kusababisha mfumuko wa bei kwa watumiaji nchini Marekani.
Ikijibu tamko la Trump kuhusu kuipandishia BRICS ushuru wa asilimia 100 kwa madai ya eti kundi hilo lina mpango wa kuunda sarafu mpya, Afrika Kusini ambayo ni mwanachama wa BRICS imetupilia mbali madai hayo.
Wizara ya Uhusiano wa Kimataifa na Ushirikiano ya Afrika Kusini ilisema ripoti za kupotosha zilizotolewa hivi karibuni zimesababisha maelezo yasiyo sahihi kwamba BRICS inapanga kuunda sarafu mpya, jambo ambalo si kweli. Ukweli ni kwamba mijadala inayofanyika ndani ya BRICS inalenga kukuza na kuendeleza biashara kati ya nchi wanachama kwa kutumia sarafu zao za kitaifa.
Trump asipokuwa makini anaweza kusababisha anguko la dola katika nyingine duniani, hasa kama ataendelea kuishurutisha dunia kutumia dola ilhali kila nchi ina uwezo wa kujiamulia ni sarafu ipi ya kutumia.