USIMAMIZI WA HAKI ZA DIJITI/DIGITALI; NINI KIFANYIKE?
Ni ukweli usiofichika teknolojia imekuza uchumi wa nchi hii kwa kasi mno. Kampuni na watu binafsi hasa wafanyabiashara hutumia ulimwengu wa elektroniki (e-world) kama nyanja yao kuu ya mawasiliano na wateja wao. Katika mawasiliano yao, wafanyabiashara hawa huwa na haki zao za kidijiti ambazo zinatambulika ulimwenguni na hulindwa kwa sheria mbalimbali za nchi husika.
Haki za dijiti ama digitali ni mfumo mzima wa kuzuia utumiaji, utengenezaji au uboreshaji na usambazaji wa kazi zenye hakimiliki kwenye mtandao au ulimwengu wa elektroniki bila ya kibali au ruhusu kutoka kwa wamiliki wa kazi hizo. Katika nchi hii, Tanzania, haki hizi za dijiti hutambulika na hulindwa chini ya sheria yetu ya hakimiliki “Copyrights and Neighbouring Rights Act” iliyofanyiwa maboresho mwaka 2019. Hivyo, kwa kupitia sheria hiyo wamiliki wa hakimiliki kwenye ulimwengu wa digitali hupata haki zao zote; iwe haki za kimaslahi ama haki za kimaadili.
Hata hivyo, ni watanzania wachache sana wenye uwelewa au hata ufahamu juu ya haki hizi za dijiti. Kampuni na wafanyabiashara wa mitandaoni wanapoteza haki zao za msingi za dijiti bila ya wao kujua. Wengine huchochea uvunjifu wa haki hizi wakiamini kwa usambazaji wa kazi zao bila hata ruhusu zao ndiyo wanakua kibiashara bila kujali kwamba kwa kufanya hivyo wanapoteza haki zao na hata mamilioni ya pesa. Mfano wa hali hii unachorwa dhahiri kwa wafanyabiashara wetu wa mtandaoni, unaweza kuta mchoraji anatangaza na kuuza biashara yake kwenye mitandao ya kijamii. Anakuja mfanyabiashara mwingine anachukua picha za mchoraji kutoka ukurasa wa mchoraji na anatangaza katika kurasa yake, mwisho wa siku hupelekea uvunjifu wa haki za mchoraji.
Ni kwa ushauri wangu, mitandao ya kijamii, digitali na ulimwengu wa kijitali uheshimike na haki za wamiliki wa hakimiliki zilindwe kwa namna zinavyotakiwa. Kwa dhumuni ya kufanikisha ushauri huu, COSOTA (chombo cha usimamizi wa hakimiliki) itoe elimu juu ya haki za dijiti kwa washikadau wake na kwa umma kiujumla. Ni vyema pia, serikali izingatie umuhimu wa haki hizi kwani, ni nyanja mojawapo ya kuongeza kipato cha taifa.
Hivyo basi,kuna uhitaji mkubwa wa kuunda mamlaka ya utawala kusimamia haki dijiti za watengeneza programu, waandishi na watumiaji wa dijiti.
Upvote
2