UTAFITI: Kutolia kunadhoofisha Nguvu za Kiume

UTAFITI: Kutolia kunadhoofisha Nguvu za Kiume

BARD AI

JF-Expert Member
Joined
Jul 24, 2018
Posts
3,591
Reaction score
8,826
Wakati jamii ikitafsiri mwanaume kulia anapopatwa na matatizo ni udhaifu, wataalamu wa saikolojia na viongozi wa dini wanasema ni afya na humpa mhusika faraja ya maumivu anayopitia.

Wameonya kuwa kukaa muda mrefu bila kuonyesha maumivu uliyoyapata kunasababisha kupoteza hamu ya vitu muhimu, ikiwemo kukosa uwezo wa kushiriki tendo la ndoa.

“Kwa asilimia 80 mtu anapofikiri kushiriki tendo la ndoa maamuzi hutokea kichwani, hivyo kama ana mawazo mengi au hana furaha maana yake atashindwa kufanya kazi vile inavyopaswa,” anasema Ramadhani Masenga, mtaalamu wa afya kutoka Mental Hygine Institute.

Hata wakifiwa, Masenga anasema wanaume wengi huambiwa wanyamaze, kwani mwanaume halii au wakitaka kuonyesha hisia zao wananyamazishwa, matokeo yake ni kile ambacho kitaalamu wanakiita unfinished bussines (biashara isiyokamilika).

“Matokeo yake ni kwamba unakuwa umefiwa mwaka juzi lakini una uchungu hadi mwaka huu kwa sababu hukupata nafasi ya kumaliza hasira na maumivu yako. Matatizo mengi ya kijinsia, watu kutokuwa na raha kwenye maisha ni kutokana na vitu vingi walivyofunika kwenye hisia zao,” anasema.

Kinachowaponza wanaume wengi, Masenga anasema ni kutokuwa huru kihisia na kifikra kwa kutakiwa kutoonyesha hisia zao.

Anasema maradhi mengi yanayoathiri moyo kwa wanaume chanzo kikubwa ni kuhifadhi vitu vingi kwenye hisia zake.

“Muda mwingi tunapambana na magumu ndani yetu ambayo kwa uhalisia tunapaswa tuyatoe, kuendelea kukumbatia ndio kunatufanya tupate magonjwa ya moyo. Tunapokuwa na maumivu na kushindwa kuyatoa kuna mambo mawili yanatokea, kwanza mtu anaweza kukerwa au kuumizwa na matukio yako lakini akayahifadhi. Kitakacho kuja kutokea ni baadaye akikerwa na mtu mwingine hasira alizohifadhi zinadhihirika kwa adhabu asiyostahili.

“Ukifanya uchambuzi kwa nini huyu mtu kachukua hatua hii wakati kosa lenyewe limefanyika dogo, utagundua ni yale makwazo ambayo alifanyiwa na akashindwa kuonyesha hisia zake hadharani,” alisema.

Masenga anasema mtu yeyote anapolia humsaidia kuondoa maumivu mwilini na kubainisha kwamba wengine huongea ili kuondoa maumivu hayo.

Kitaalamu anasema inashauriwa mtu kuongea ili kuondoa maumivu, kwani maneno yatakayotoka yatakuwa yameambatana na hisia.

Mwanasaikolojia Charles Muhando anasema moja ya mambo yanayochangia mwanaume kujiua ni kubaki na vitu vingi vinavyowaumiza moyo.

“Hiyo inasababishwa na namna jamii inavyomchukulia mwanaume kuwa anaweza kuvumilia kila jambo hata linalomuumiza. Utasikia jikaze wewe ni mwanaume, jamii imekuwa ikimchukulia kama mtu ambaye hatakiwi kuonyesha udhaifu wa hisia,” anasema Muhando.

Hali hiyo, anasema husababisha mwanaume akilia kutafsiriwa kama mzembe, hivyo wengi kugugumia maumivu moyoni ,

“Hali ya jamii kumchukulia mwanaume kuwa hatakiwi kuonyesha udhaifu humfanya kutokubali kushindwa na jambo na ikitokea ameshindwa kuyafikia matarajio yake kama hana uvumilivu au hayuko na mtu ambaye atampa msaada wa kisaikolojia anaweza akachukua uamuzi wowote hata kujiua,” anasema Muhando.

Viongozi wa dini
Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Richard Hananja anasema mafunzo yaliyotolewa zamani kwamba mwanaume hapaswi kulia yalilenga kumuimarisha, ila akashauri kama mtu anajisikia kulia kulingana na machungu aliyonayo ni muhimu kufanya hivyo ili kulinda afya yake na utimamu wa mwili kufanya mambo mengine.

“Kulia ni faraja, Mungu katuumba hivyo...ukifurahi unacheka na ukiwa na huzuni unaonyesha sura huzuni, hata ukikasirishwa unakasirika na ukiteswa unalia. Ukiumizwa unatakiwa kulia, kulia sio udhaifu, lakini unalia kwenye jambo lipi, sio unakosa hela ya kula unalia pambana,” alisema Hananja.

Hata hivyo, mchungaji huyo anatahadharisha kwamba “yapo mambo mengi unayoweza kulia yakitokea, kwa mfano umefiwa na mtoto au mke ni lazima ulie. Kulia si unyonge bali ni tiba lakini unalia kwenye lipi,’’ alisisitiza.

Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum anasema tafsiri ya watu kuwaita wanaume dhaifu pindi wanapolia si sahihi na utamaduni huu umekuwa ukiwaumiza wengi.

“Kulia ni katika maumbile ya binadamu anapopatwa na jambo la huzuni au anapopata jambo la furaha, lakini akilia anapopata jambo la huzuni ni suala la maumbile. Mungu alitujalia machozi ghali zaidi ambayo Mungu ameyaweka hivyo, mwanamume anapotoa machozi anakamilisha uumbaji wa Mungu kwake kwamba yeye ni binadamu anaweza kutoa machozi,” anasema Sheikh Salum.

Kiongozi huyo wa mkoa alisema kulia ni afya na kwenye maelekezo ya Mtume (S.A.W) alieleza kuwa jicho lenye kulia kwa hofu ya Mungu halitaingia motoni, akiongeza kuwa kulia ni sehemu ya ibada na kama mtu hajisikii kulia anaweza kujiliza.

Jumanne Hussein, mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam anasema ni suala gumu kwake kulia hata anapopatwa jambo lolote, kwani sifa kubwa ya mwanamume ni uvumilivu,.

“Naanzaje kulia, nikilia mimi mwanamke atafanyaje, mwanaume unajikaza unaendelea na mambo mengine, hata nikilia nani atanipa msaada? Kwa hiyo ni suala la kupambana na kuvumilia,’’ alisema.

Mtazamo wa Hussein ni tofauti na Jesca Godfrey, mkazi wa Temeke ambaye alisema mwanamke kulia anapopatwa na tatizo lolote si kwa ajili yake, bali juu ya familia anayoifikiria.

“Kuna mambo unafanyiwa ukiyatafakari unaiwaza familia yako itakuwaje. Kwa mfano, ninapogombana na mwanamume tutatengana, nitakachofikiria ni kuhusu familia yangu tofauti na mwanaume anajifikiria yeye mwenyewe tu,” alisema Jesca.

Source: Mwananchi
 
Sie wenyewe kulia sio kwamba hatupendi lakini issue inakuja hisia za kulia hatuna
 
Back
Top Bottom