Tumaini CN-CNB
Member
- Feb 13, 2021
- 5
- 5
UKUTA MKUU WA CHINA
中国的万里长城
THE GREAT WALL OF CHINA
Kimetungwa na Luo Zhewen (罗哲文)na Zhao Luo (赵洛)
Kimetafsiriwa na Tumaini
UTANGULIZI
中国的万里长城
THE GREAT WALL OF CHINA
Kimetungwa na Luo Zhewen (罗哲文)na Zhao Luo (赵洛)
Kimetafsiriwa na Tumaini
UTANGULIZI
Kwa wageni, “Ukuta Mkuu” hutajwa pamoja na China. Katika kitabu cha jiografia cha shule za msingi, wanafunzi walisoma habari kuhusu Ukuta Mkuu, mmojawapo wa miujiza ya dunia. Usemi wa China husema: “Asiyefika kwenye Ukuta Mkuu si mtu shupavu.” Mgeni ye yote aliyefika China, asipozuru Ukuta Mkuu, bila shaka ni jambo la kusikitisha.
Kwa ajili ya kuthibitisha ukubwa wa mradi wa Ukuta Mkuu, watu husema kuwa Ukuta Mkuu ni jengo kubwa kabisa duniani lililoweza kuonwa na wanaanga kutoka mwezini. Watu walisema ukitumia matofali na mawe ya Ukuta Mkuu kujenga ukuta mkubwa wenye kimo cha mita tano na unene wa mita moja, basi ukuta huo mpya unaweza kuzunguka dunia mara moja na zaidi. Wengine walisema kuwa ungehamisha Ukuta Mkuu hadi Marekani, ukuta huo ungeweza kuenea kutoka Philadelphia hadi Kansas; ungeuhamisha hadi Ulaya, urefu wake ungekuwa sawa na urefu wa kutoka Lisbon hadi Naples n.k..
Historia ndefu ya Ukuta Mkuu vilevile huzungumzwa na watu kwa hamu na furaha. Watu wengi hudhani kuwa Ukuta Mkuu ulijengwa na Qin Shihuang mfalme wa kwanza aliyekuwa na tamaa kubwa ya utawala katika Enzi ya Qin ya karne ya 3 K.K.. Hadithi za mapokeo kuhusu mfalme huyo zimekuwa zikipokezwa kutoka kizazi hadi kizazi mpaka leo. Kwa karne nyingi watu wamekuwa wakibishana kuhusu sifa na makosa ya Qin Shihuang. Jambo hili pia linahusiana na Ukuta Mkuu. Kusema kweli, kati ya masimulizi yaliyotajwa hapo juu, mengi yao hayalingani na hali halisi.
Ukuta Mkuu tunaouona hivi leo, siyo mabaki ya kipindi cha Qin Shihuang, kwa sababu Ukuta Mkuu wa leo una historia ya zaidi ya miaka 600 tu. Lakini Ukuta Mkuu wa kwanza kwa kweli ulijengwa mnamo karne ya 7 K.K.. Baada ya hapo, watawala wa enzi zilizofuata, walijenga makumi ya Kuta Kuu. Mpaka sasa bado yanaonekana magofu ya Ukuta Mkuu wa Dola la Qi uliojengwa mnamo mwaka 555 K.K. katika Jimbo la Shandong. Tukijumlisha urefu wa kuta kuu zote zilizojengwa katika enzi mbali mbali, urefu wao wa jumla unaweza kufikia kilomita 50,000 na zaidi. Katika Mkoa wa Mongolia ya Ndani peke yake kulikuwa na Ukuta Mkuu wa kilomita 15,000.
Ukuta Mkuu ni ushuhuda wa historia ya China. Katika muda mrefu wa zaidi ya karne 20, Ukuta Mkuu uliwahi kustawi kwa kufuata ustawi wa jamii ya kikabaila ya China na ulipoteza manufaa yake hatua kwa hatua kwa kufuata uzorotaji wa jamii ya kikabaila. Ukuta Mkuu ulitoa mchango mkubwa katika kukinga mashambulio ya makabila ya uchungaji yaliyokuwa yakihamahama ya kaskazini, kulinda usalama wa maeneo ya kati ya China na amani ya maisha ya sehemu moja hadi nyingine, kustawisha maeneo ya mipakani na kuhakikisha upitikaji wa “Njia ya Hariri” - njia muhimu ya mawasiliano baina ya China na nchi za maeneo ya magharibi.
Watu wa China huuchukua Ukuta Mkuu kuwa kama roho ya taifa la China. Kuanzia Vita vya Kasumba vya mwaka 1840, watu wa China walikuwa wakipigania uhuru bila ya kulegea. Katika miaka ya 1930, watu wa China waliposhambuliwa na mabeberu wa Japani, wakiimba kwa sauti kubwa wimbo wa Kusonga Mbele kwa Waliojitolea, walipigana dhidi ya maadui kwa ushujaa. Maneno ya wimbo huo yanasema: “Amkeni enyi, msiokubali kuwa watumwa, kwa damu na miili yetu Ukuta Mkuu mpya utajengwa ….” Baada ya kupigana vita kwa muda wa miaka minane, mwishowe wakafanikiwa kuwafukuza washambulizi kutoka China. Mwaka 1949, historia ya miaka 100 ya watu wa China ya kushambuliwa na kukandamizwa na nchi za nje ilimalizika; China Mpya imesimama kwenye upande wa mashariki wa dunia ikiwa kama Ukuta Mkuu adhimu.
Ukuta Mkuu umepoteza uwezo wake katika mambo ya kijeshi tangu zamani, lakini leo umekuwa mahali pazuri pa utalii ambapo watu wengi hutamani kupatembelea. Katika kila majira ya mwaka huonekana watalii wengi kwenye sehemu muhimu na vipito maarufu vya Ukuta Mkuu, kama vile Shanhaiguan iliyoko kwenye Jimbo la Hebei, Jiayuguan iliyoko katika Jimbo la Gansu, Juyongguan iliyoko umbali wa kilomita 50 hivi kaskazini ya Mji wa Beijing na sehemu ya Badaling ya Ukuta Mkuu iliyoko umbali wa kilomita 60 hivi kutoka Mji wa Beijing. Ukuta Mkuu unawavutia wapiga picha na wachoraji na vile vile unawafurahisha watembezi wengi kwa mandhari yake.
Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China inazingatia sana kuhifadhi na kuufanyia utafiti Ukuta Mkuu. Baada ya ukombozi, Shanhaiguan, Jiayuguan na sehemu ya Badaling ya Ukuta Mkuu ziliorodheshwa kuwa kundi la kwanza la majengo muhimu va kale yanayohifadhiwa na serikali. Mwaka 1980 Serikali ya China iliitisha mkutano unaohusu Ukuta Mkuu katika Mji wa Huhhot wa Mkoa Unaojiendesha Wenyewe wa Mongolia ya Ndani. Wasomi walioshiriki katika mkutano huo walitoa makumi ya tasnifu za kutafiti Ukuta Mkuu, pamoja na mapendekezo mengi muhimu kuhusu kuhifadhi Ukuta Mkuu. Serikali za mitaa za ngazi mbali mbali zilizoko kandokando ya Ukuta Mkuu pia ziliamua kuwa vipito, majengo makubwa na madogo na sehemu za Ukuta Mkuu ni majengo muhimu ya kuhifadhiwa katika sehemu zao, na zimekuwa zikituma watu kukagua na kutunza Ukuta Mkuu, kuwaeleza wenyeji umuhimu wa kuhifadhi na kuwaomba watu wote wauhifadhi kwa makini, maana Ukuta Mkuu si wa China tu bali pia ni wa dunia nzima.