Moaz
Member
- Apr 6, 2018
- 88
- 127
Ndugu Wadau wa Soka Tanzania,
Napenda kuchukua fursa hii kuwakaribisha katika mchakato muhimu kuhusu maendeleo ya mpira wa miguu nchini Tanzania kupitia mradi wa SAMTA (Sauti ya Mpira Tanzania).
UTAMBULISHO WA SAMTA
SAMTA ni jukwaa linalokusudia kuwakutanisha wadau wote wa mpira wa miguu nchini Tanzania, wakiwemo makocha, wachezaji, mashabiki, wachambuzi, waandishi wa habari, viongozi, wawekezaji, taasisi, na wadau wengine wa mpira. Lengo kuu la SAMTA ni kukuza na kuendeleza mchezo wa mpira wa miguu nchini kwa kutumia maarifa ya kisasa, mijadala ya kitaalam, na ushirikiano wa wadau mbalimbali.
MALENGO YA SAMTA
1. Elimu ya Kisasa ya Mpira wa Miguu: Kuandaa programu za elimu kwa makocha, wachezaji, wachambuzi wa soka, waandishi wa habari na wadau wengine wa mpira.
2. Majadiliano ya Kitaalamu: Kutoa fursa kwa makocha na wataalam wa mpira wa miguu kujadiliana kuhusu mbinu mpya za soka, mifumo ya uchezaji, na maendeleo ya soka la kisasa.
3. Uchambuzi wa Kina: Kuhamasisha uchambuzi wa kisayansi wa mechi, wachezaji, na timu ili kusaidia kuboresha kiwango cha mchezo nchini.
4. Uhifadhi wa Historia ya Mpira wa Miguu Tanzania: Kukusanya na kuhifadhi kumbukumbu za kihistoria za mpira wa miguu nchini ili kuhakikisha historia ya soka haipotei.
5. Kuhamasisha Uwekezaji: Kuwahamasisha wawekezaji wa ndani na nje kuwekeza kwenye mpira wa miguu Tanzania kwa kutengeneza mazingira bora ya biashara ya michezo.
6. Kuleta Mashabiki Karibu: Kuwajumuisha mashabiki wa soka kwenye majadiliano yenye tija, mijadala ya kina, na programu maalum za mashabiki kupitia jukwaa la "Benchi la Mashabiki."
DIRA NA DHAMIRA YA SAMTA
Dira: "Kuitambulisha Tanzania kama kitovu cha elimu ya soka, maendeleo, ushiriki wa mpira wa miguu na ubunifu katika Afrika Mashariki kwa kuunganisha maarifa ya ndani na viwango vya kimataifa"
Dhamira: "Kusasaisha na kuleta weledi katika tasnia ya mpira wa miguu wa Tanzania kwa kutoa elimu rahisi kufikiwa, kukuza ubunifu, kuwahusisha mashabiki na kuunda mazingira endelevu na jumuishi kwa wadau wote wa soka"
KWANINI SAMTA NI HATUA MUHIMU?
Mpira wa miguu ni zaidi ya burudani; ni sekta inayoweza kuleta ajira, maendeleo ya kijamii, na kuimarisha utambulisho wa taifa kimataifa. Hata hivyo, maendeleo ya mpira nchini yanakabiliwa na changamoto kadhaa, ikiwemo ukosefu wa elimu sahihi kwa wadau, ukosefu wa mijadala ya kitaalam kuhusu maendeleo ya soka nchini, na uhaba wa fursa za uwekezaji katika sekta ya mpira wa miguu. SAMTA inaleta suluhisho kwa kuunganisha wadau, ili waweze kushirikiana kwa kushare elimu sahihi miongoni mwao na kuhamasisha uwekezaji kwenye sekta hii muhimu.
HATUA AMBAZO SAMTA IMEFIKIA KWA SASA
- Tumeshakamilisha mchakato wa awali wa kuunda jukwaa la kidigitali la SAMTA. (Documents and Business Plan)
- Tumeshafikia makocha, wachambuzi, na mashabiki wa soka ili kujadili umuhimu wa mradi huu.
- Tumeshafanya majaribio ya majadiliano ya kitaalam miongoni mwa wadau wa mpira wa miguu.
- Tunapanga kuanza kuandaa na kutengeneza Progam ya SAMTA
MSAADA UNAOHITAJIKA ILI KUFANIKISHA MRADI HUU
Ili kufanikisha SAMTA, tunahitaji ushirikiano wa wadau wa mpira wa miguu katika maeneo yafuatayo:
1. Mchango wa Mawazo: Tunahitaji maoni na mapendekezo ya wadau kuhusu namna bora ya kuimarisha SAMTA .
2. Uwekezaji: Tunakaribisha wadau na wawekezaji wanaoweza kusaidia kifedha katika kutengeneza jukwaa la SAMTA na kuwezesha programu zake.
3. Ushirikiano na Taasisi: Tunahitaji ushirikiano na taasisi za soka, mashirika, na vyombo vya habari ili kueneza dhamira ya SAMTA.
4. Teknolojia: Tunahitaji wataalam wa teknolojia kusaidia katika uundaji na usimamizi wa jukwaa la kidijitali la SAMTA.
5. Uhamasishaji: Tunahitaji mashabiki wa soka na wadau wa mpira kushiriki kikamilifu katika jukwaa la SAMTA na kusambaza taarifa zake kwa wengine.
HITIMISHO
SAMTA ni jukwaa la mabadiliko katika mpira wa miguu Tanzania, lenye lengo la kuleta maendeleo ya kweli kwa kupitia elimu, mijadala ya kitaalam, na ushirikiano wa wadau wote wa mpira. Tunawakaribisha wadau wote kushiriki katika safari hii muhimu ili kwa pamoja tufanikishe maendeleo ya mpira wa miguu Tanzania.
Tunaomba ushirikiano wako katika kufanikisha mpango huu muhimu. Tafadhali wasiliana nasi kwa maelezo zaidi na jinsi unavyoweza kushiriki.
Kwa mawasiliano:
Email: sautiyampirawatanzania@gmail.com
Phone 📞: +255789574411
Kwa pamoja, tunaweza kuleta mapinduzi katika mpira wa miguu Tanzania!
Wanzilishi wa SAMTA