Hili suala naona linazungumziwa kiutani lakini kwa taratibu za FIFA zilivyo iwapo uongozi wa Yanga hautachukulia suala la kuvunja mikataba na wachezaji/makocha wake kwa makubaliano ya maridhiano ya pande mbili na wachezaji hao wakaenda kushtaki TFF and then madai yakafika FIFA na ikaonekana madai yao ni ya kweli na Yanga haina uwezo wa kuwalipa basi usishangae kuikuta Yanga mwakani inapambana na Mawenzi market, Ihefu, Green warriors n.k.
Kimsingi uongozi wa Dk. Msola unapaswa kutumia busara na maridhiano na wachezaji/makocha wanaovunja mikataba yao na si watumie mihemuko ili kila mtu aende zake kwa amani ya bwana akiwa ameridhika. Ni busara zaidi kwa uongozi kufanya makubaliano na wachezaji/makocha wanaowaacha kuwa siri badala ya kuwatuma wasemaji wa klabu kwenye vyombo vya habari kubwabwaja kuwa mchezaji fulani hana kiwango tumeamua kumuacha. Kwa mchezaji/kocha ambaye anaona kabisa hali ya kiuchumi ya klabu sio nzuri akielezwa vizuri na makubaliano yakawa siri ni rahisi sana kuvunja mkataba na akasamehe baadhi ya madai yake.
Kuvunja mikataba na wachezaji/makocha ni jambo la kawaida duniani kote na Yanga si wa kwanza wala hatakuwa wa mwisho. Kimsingi wawatumie wanasheria ambao ni mashabiki wa Yanga ambao wapo wengi tu nchini ili wawasaidie katika hili tena bila hata malipo ili klabu isiingie katika migogoro isiyo na tija na kuiingiza taasisi kubwa kama hii kwenye matatizo ambayo yanaweza kuzuilika.