Ukitaka kutambua kwa usahihi siku ambazo mwili wa Yesu Kristo ulikaa kaburini ni vyema uchunguze kwanza maandiko yanasemaje kuhusu msingi uliowekwa wa maadhimisho ya sikukuu za,
a) Sabato ya kila mwisho wa juma,
b) Pasaka,
c) Pamoja na siku 7 zinazoambatana na Sabato ndogo mbili za maadhimisho ya sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu.
Wayahudi walikuwa na sikukuu ya Sabato kubwa ambayo iliadhimishwa kila siku ya 7 ya juma. Katika sikukuu hii iliwalazimu kustarehe kabisa bila ya kufanya kazi yoyote ile, na pia kushiriki katika kusanyiko takatifu. Katika Sabato hii hawakutakiwa kufanya kazi yoyote ile, iwe ya utumishi ama kazi nyingine ya nyumbani isiyokuwa ya utumishi.
Aidha kulikuwa na sikukuu za sabato ndogo ambazo ziliadhimishwa mara moja kwa mwaka kama vile zilivyoainishwa ndani ya vitabu vya Torati, hazikupaswa kuadhimishwa kila juma kama ilivyo Sabato kubwa, masharti pekee ilikuwa wafanye kusanyiko takatifu na kutokufanya kazi za utumishi tu. Hivyo Torati haikuwalazimisha kustarehe kabisa na kuacha kufanya kazi zingine zisizokuwa za utumishi. Ebu kwanza tuirejee nukuu ifuatayo kutoka katika maandiko matakatifu,
MAMBO YA WALAWI 23
1 Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Sikukuu za BWANA, ambazo mtazitangaza kuwa ni makusanyiko matakatifu; hizi ni sikukuu zangu.
3 Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yoyote; ni Sabato kwa BWANA katika makao yenu yote.
4 Sikukuu za BWANA ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo
5 Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni Pasaka ya BWANA.
6 Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa BWANA ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba.
7 Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yoyote ya utumishi.
8 Lakini mtasongeza sadaka kwa BWANA kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yoyote ya utumishi.
Yesu Kristo alikula sikukuu ya Pasaka na wanafunzi wake jioni ya siku ya 14 ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa Kiyahudi (Walawi 23:5). Ambapo baada ya hapo alikwenda nao bustani ya Gethsemane. Kutokana na juma letu hii ilikuwa ni siku ya Jumanne. Nukuu kutoka katika kipande cha Neno la Injili kinasema,
LUKA 22
7 Basi, siku ya mikate isiyotiwa chachu ikafika. Hiyo ndiyo siku ambayo mwanakondoo wa Pasaka huchinjwa.
8 Hivyo Yesu akawatuma Petro na Yohane, akawaambia, “Nendeni mkatuandalie karamu ili tupate kula Pasaka.”
Siku ya 15, yaani siku ya Jumatano ilikuwa sikukuu ya mikate isiyotiwa chachu (Walawi 23:6), siku ambayo aliteswa na kufa msalabani muda wa saa 9 alasiri. Nukuu ya kipande cha Neno la Injili kinasema,
MATHAYO 27
45 Tangu saa sita mchana mpaka saa tisa, nchi nzima ilikuwa giza.
46 Mnamo saa tisa Yesu akalia kwa sauti kuu, “Eli, Eli lama sabakthani?” Yaani, “Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha?”
47 Baadhi ya watu waliokuwa wamesimama hapo waliposikia haya walisema, “Anamwita Eliya!”
48 Mmoja wao akaenda mbio akaleta sponji akaichovya kwenye siki akaiinua kwa mwanzi akamwekea mdomoni.
49 Lakini wengine wakasema, “Hebu tuone kama Eliya ata kuja kumwokoa.”
50 Yesu akalia tena kwa sauti kuu, kisha akakata roho.
Siku ya 16, yaani Alhamisi, ilikuwa ni sikukuu ya sabato ndogo (Walawi 23:7), kwa kuwa ilikuwa ni siku ya kusanyiko takatifu ambapo Wayahudi hawakupaswa kufanya kazi za utumishi. Hii ilikuwa siku ya kwanza kwa mwili wake kukaa kaburini chini ya moyo wa nchi. Nukuu kutoka katika kipande cha Neno la Injili kinasema,
LUKA 23
50 Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yusufu mwenyeji wa mji wa Arimathaya, ambaye alikuwa anautazamia Ufalme wa Mungu. Yeye alikuwa mjumbe wa Baraza na pia alikuwa mtu mwema na mwenye kuheshimika.
51 Lakini yeye hakukubaliana na wajumbe wenzake katika uamuzi wao na kitendo cha kumsulubisha Yesu.
52 Basi, Yusufu alikwenda kwa Pilato akaomba apewe mwili wa Yesu.
53 Akaushusha kutoka msalabani, akauzungushia sanda, akauhifadhi katika kaburi lililochongwa kwenye mwamba. Kaburi hilo lilikuwa halijatumika bado.
54 Siku hiyo ilikuwa ni siku ya Maandalio, na sabato ilikuwa karibu ianze.
55 Wale wanawake waliokuwa wamefuatana na Yesu kutoka Galilaya wakamfuata Yusufu, wakaliona kaburi na jinsi mwili wa Yesu ulivyolazwa humo.
56 Kisha wakarudi nyumbani wakaandaa marashi na manukato ya kuupaka huo mwili. Lakini waka pumzika siku ya sabato kama ilivyoamriwa.
Siku ya 17 ya mwezi huu wa Kiyahudi, yaani siku ya Ijumaa, ilikuwa ni siku ya maandalizi ya sikukuu ya Sabato kubwa ya kila juma. Hii ilikuwa ni siku ya pili kwa mwili wake kukaa kaburini. Nukuu kutoka katika kipande cha Neno la Injili kinasema,
MATHAYO 27
62 Hata siku ya pili, yaani ndiyo iliyo baada ya Maandalio, makuhani wakuu na Mafarisayo walimwendea Pilato
63 wakamwambia, “Tunakumbuka kwamba yule mwongo alisema, ‘Baada ya siku tatu nitafufuka.’
64 Tunaomba uamuru kwamba kabu ri liwekewe ulinzi hadi siku ya tatu. Vinginevyo wanafunzi wake wanaweza wakaja wakauiba mwili wake na kuwaambia watu kwamba amefufuka. Jambo hili likitokea uongo huu wa mwisho utakuwa mbaya zaidi ya ule wa kwanza.”
65 Pilato akawaambia, “Ninyi mnao askari. Nendeni mkaweke ulinzi, mhakikishe pamekuwa salama kama mpendavyo.”
66 Wakaenda wakaweka ulinzi kaburini, wakaliwekea lile jiwe mhuri na kuwaweka askari walinzi.
Na hatimaye Bwana Yesu Kristo alifufuka kutoka katika wafu siku ya 18 ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa Kiyahudi, yaani siku ya Jumamosi, saa 9 alasiri, baada ya kutimia kwa siku tatu kamili za mwili wake wa awali wa kibinadamu kukakaa kaburini kama vile yeye mwenyewe alivyonena kuhusu jambo hilo.
Tukio hili lilitokea siku ya Sabato kubwa ambayo Wayahudi walipaswa kustarehe kabisa na hawakutakiwa kufanya kazi za namna yoyote ile. Ndiyo maana wakuu wa makuhani walikwenda kumuomba Pilato ulinzi wa kaburi ufanywe na askari wa Kirumi.
Ikawa jioni, ikawa asubuhi siku ya 19 ya mwezi wa kwanza wa mwaka wa Kiyahudi, yaani siku ya Jumapili alfajiri na mapema, ndipo taarifa za kufufuka kwake zilipoanza kusambaa. Lakini tukio la kufufuka kwake na kuondoka kwake kaburini lilidhihirika na kuwa bayana kabisa kwa wale askari wa Kirumi waliokuwa na jukumu ya kulilinda kaburi lake, nao walikwenda kutoa ushuhuda wao kwa wakuu wa makuhani na Mafarisayo. Nao waliwahonga kwa fedha kuuficha ukweli huo. Nukuu ya kipande cha Neno la injili kinasema,
MATHAYO 28
11 Wakati wale wanawake walipokuwa wanakwenda, baadhi ya wale askari waliokuwa wanalinda kaburi, wakaenda mjini kuwaeleza makuhani wakuu yote yaliyotokea.
12 Baada ya kufanya mkutano na wazee na kushauriana, waliwapa wale askari kiasi fulani cha fedha na
13 kuwaambia, “Semeni, ‘Wanafunzi wake walikuja wakamwiba usiku sisi tukiwa tumelala.’
14 Kama habari hizi zikimfikia gavana, sisi tutamridhisha na hamtapata shida yo yote.”
15 Kwa hiyo wale askari wakazipokea hizo fedha wakafanya kama walivyoagizwa. Na habari hii imeenea kwa Wayahudi mpaka leo.
Hakuna utata wowote ule katika hesabu za siku 3 za mwili wa Yesu Kristo kukaa kaburini. Maandiko matakatifu yanahitaji hekima kubwa sana kupitia karama za Roho wa Kristo, ili kuweza kuyapatanisha vyema na kuleta maana sahihi iliyokusudiwa kwa kuzingatia misingi iliyojengeka kupiria katika Neno hilo hilo.
Ukiyasoma pasipo kuwa na hekima hii utaishia kujichanganya wewe mwenyewe na kisha kuishia kuleta tafsiri potofu sana. Neno la Mungu hujisimamia na kujitetea lenyewe, halihitaji falsafa, dhana, elimu wala simulizi za mapokeo ya kibinadamu ili kujenga mantiki. Jambo la msingi ni kuzipatanisha aya sahihi ili zitupe kwa usahihi ujumbe uliokusudiwa.
Mbarikiwe sana kupitia Jina lipitalo majina yote duniani na mbinguni, Jina la BWANA YESU KRISTO.