Nikiwa nimeishi nchini China kwa miaka mingi sana tangu mwaka 2008, na kushuhudia nchi hii ambayo sasa ni ya pili kwa uchumi mkubwa duniani inavyobadilika hatua kwa hatua, chini ya muongozo wa chama tawala cha Kikomunisti cha China yaani CPC, na kwa ushirikiano mkubwa wa vyama vingine vidogo, inanikumbusha jinsi vyama vya siasa vya nyumbani kwetu Tanzania, vinavyopaswa kushirikiana pamoja kuwajali zaidi wananchi na maslahi ya taifa, badala ya kila chama kufanya kazi peke yake, huku kikisubiri chama kimoja kiteleze kisha kianze kukikosoa hadharani.
Katika kipindi chote nilichopo hapa, somo kubwa ambalo nimelipata kupitia uongozi imara wa chama cha CPC na serikali yake ni kwamba, hakuna muda wa kupoteza katika kuwatumikia wananchi. Na jambo linalonigusa zaidi katika miaka yote hii hadi kunipa hamasa ya kuandika haya, ni kuona nchi ikifanya kazi zake kwa kufuata maadili, kuheshimu wakati, na kuwa na kiwango kikubwa cha utaratibu na mipango kabambe inayowekwa katika kila ngazi ya jamii.
Mfano mzuri ni Mpango wa 14 wa Miaka Mitano wa China (2021-2025) ambao unahitimisha utekelezaji wake mwaka huu wa 2025. Kama taasisi muhimu yenye tija kubwa katika mfumo wa utawala wa taifa la China, mipango ya miaka mitano imekuwa muhimu katika kusukuma mbele maendeleo ya nchi katika sekta zote kwa miongo kadhaa iliyopita. Pia mipango hii inatanguliza mbele maendeleo ya hali ya juu na kuonesha vipaumbele vya nchi.
Kufuatia kukamilika kwa utekelezaji wa Mpango wa 14 wa Miaka Mitano wa China (2021-2025), mwezi Oktoba mwaka huu Chama cha CPC kitafanya mkutano wake mkuu, ili kuainisha mipango yake ya maendeleo ya taifa kwa miaka mitano ijayo (2026 hadi 2031) huku kikizingatia hatari za kiuchumi za ndani na nje ya nchi.
Mipango hii inayowekwa na chama tawala kwa ajili ya kuwaneemesha na kuwaletea maisha bora wananchi, inazidi kuongeza uelewa wangu juu ya itikadi za watu wa China. Mipango hii imepata mafanikio makubwa kwani imeitoa nchi kwenye jamii ya kilimo pekee hadi kuwa nchi ya pili kwa uchumi mkubwa duniani, ikipata faida mbili kubwa ambazo ni ukuaji wa haraka wa uchumi na utulivu wa muda mrefu wa kijamii.
China haikuinuka kirahisi tu. Ilipanda kwa sababu CPC inatawala vyema kimkakati, kimbinu, na kuwa na kiwango kikubwa cha uwajibikaji na nidhamu ndani ya chama, jambo ambalo mara nyingi limekuwa likiwashangaza wakosoaji wake wa nchi za Magharibi. Chama kimejenga utamaduni kwa maafisa kuwa na sifa, watendaji kazi, na kufuata sera za chama, na sio kuchaguliwa kutokana na umaarufu wao au kwa upendeleo. Mwenendo huu mzuri umewezesha China kuwa na mwelekeo thabiti na wa muda mrefu wa sera zake.
Nchi nyingi zinazoendelea, zikisukumwa na mafanikio ya China, zimefuata nyayo za China kwa kuanzisha mikakati ya muda mrefu hadi ya muda wa kati, huku nchi kadhaa zikiwa ni pamoja na Ethiopia na Tanzania zimekaribisha taasisi za China kusaidia katika mashauriano yao ya kuweka mipango yao.
Tunafahamu kuwa Chama cha CPC na CCM cha Tanzania vimekuwa na uhusiano wa kisiasa wa muda mrefu na vimechangia kwa kiasi kikubwa mafanikio ya nchi zote mbili katika nyanja mbalimbali. Kwa minajili hii, na kwa mifano kadhaa ambayo tayari nimeshailezea kuhusu namna CPC inavyowapigania wananchi wake, si vibaya kwa vyama vya siasa vya Afrika hususan CCM ya Tanzania, kuendelea kuchota maarifa haya, kwani wahenga hawakukosea waliposema ukiwa karibu na muwaridi lazima nawe utanukia.
Wakati uchaguzi mkuu unakaribia nchini Tanzania, vyama vya siasa vya nchi hiyo sasa ni wakati wao wa kuonesha mshikamano, na kutambua kuwa tofauti za kisiasa hazipaswi kutumika kama sababu ya kuharibu umoja, amani na mshikamano wa kitaifa uliojengwa kwa muda mrefu. Badala yake sasa hivi ni muda wa kunadi sera ambazo zitakuwa na maslahi kwa wananchi, na kuweka mipango ya kuinyanyua nchi kiuchumi, kama inavyofanya CPC.
Tutambue kuwa kwa nchi, amani ina thamani kuliko hata dhahabu. Unaweza kuondoa amani kirahisi sana, lakini kuirejesha, ni lazima kuwe na gharama ya mali na maisha ya watu. Na hii inatufanya turejee kwa wahenga pale wanaposema amani haiji ila kwa nja ya upanga.