GE2025 Uteuzi wa wagombea umekuza au umekanyaga demokrasia ndani ya CCM?

GE2025 Uteuzi wa wagombea umekuza au umekanyaga demokrasia ndani ya CCM?

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

Parabolic

JF-Expert Member
Joined
Dec 3, 2013
Posts
2,922
Reaction score
3,252
Kufuatia Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutoa orodha ya watia nia waliopita kuwa nia Ubunge hatua ya awali katika Majimbo mbalimbali Tanzania Bara na Zanzibar, kumekuwa na sura tofauti za maoni kuhusu demokrasia ndani ya chama hicho kuelekea uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, huku pia ikielezwa kuwa safu inapangwa kuelekea 2030.

Katika orodha hiyo, zaidi ya robo tatu ya makada wake 4,109 waliochukua fomu kuomba ridhaa ya kuwania ubunge katika majimbo 272 ya Tanzania Bara na Zanzibar, wamefyekwa.

Kati ya makada hao waliochukua fomu, Kamati Kuu ya chama hicho iliyoketi Julai 28, 2025, imependekeza majina 1,477 pekee, sawa na asilimia 36, huku 2,632 yakitemwa. Kati ya hayo, yamo ya wabunge zaidi ya 25 waliohudumu kwa zaidi ya muongo mmoja.

Waliopenya

Sura mpya ya vigogo zimetawala katika mchuko huo akiwamo aliyekuwa Mkuu wa Mikoa ya Dar es Salaam na baadaye Arusha, Paul Makonda, Daniel Chongolo, aliyehudumu katika Mkoa wa Songwe na Katibu Mkuu wa CCM, naye ameingia katika orodha hiyo ya wateule, huku Dk Raphael Chegeni akiwa miongoni mwao.

Aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa naye amepenya kwenye mchujo huo na sasa anasubiri kura za wajumbe na uamuzi wa vikao vya kitaifa vya chama hicho ili awe mgombea ubunge au vinginevyo.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, James Ole Millya, ni miongoni mwa makada walioteuliwa kuwania ubunge wa Simanjiro, Mkoa wa Manyara. Millya amewahi kuwa Mbunge wa Simanjiro 2015–2020.

Katika kundi hilo yumo aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (sasa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi), Dk Wilson Mahera, anayetaka kuwawakilisha wananchi wa Butiama, Mkoa wa Mara.

Katika asilimia 36 ya waliopendekezwa, wamo baadhi ya waliokuwa wabunge 19 wa viti maalumu wa Chama cha Domokrasia na Maendeleo (Chadema) waliohamia CCM dakika za mwisho, wakiwemo Esther Bulaya, Esther Matiko, Nusrat Hanje, Grace Tendega, Jesca Kishoa, Kunti Majala na Hawa Mwaifunga.

Wanahabari nao hawakubaki nyuma, kwani wapo kina Baruan Muhuza (Kigoma Mjini), Salim Kikeke (Moshi Vijijini), Hamis Mkotya na Juma Nkamia (Chemba), Hashim Ibwe (Mwanga) na Manyerere Jackton (Butiama).

Kwa mujibu wa ratiba ya CCM, waliopita katika mchujo huo sasa watakwenda kupigiwa kura na wajumbe Agosti 4, 2025, kisha Kamati Kuu itaamua nani kati yao aipeperushe bendera ya CCM jimboni katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025.

Waliofyekwa

Miongoni mwa wabunge na watu mashuhuri waliokumbwa na panga hilo ni Mbunge wa Bumbuli kwa miaka 15, January Makamba na Luhaga Mpina aliyewawakilisha wananchi wa Kisesa kwa miongo miwili.

Wengine waliofyekwa ni Angeline Mabula aliyekuwa Mbunge wa Ilemela tangu 2015 naye ametemwa katika orodha hiyo, licha ya wasifu wake wa kuiongoza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, akianzia kuwa naibu katika wizara hiyo.

Pia, aliyekuwa Mbunge wa Arusha Mjini kwa miaka mitano, Mrisho Gambo naye amekumbana na panga hilo. Historia ya Gambo inabebwa na utumishi wa umma, kuanzia Halmashauri ya Arusha na baadaye kuwa mkuu wa mkoa huo, kisha mbunge

Wengine waliotemwa ni Stephen Byabato (Bukoba Mjini), Ndaisaba Ruholo (Ngara), Mohamed Monni (Chemba), Christopher Sendeka (Simanjiro), Godwin Kunambi (Mlimba), Justin Nyamoga (Kilolo), Shanif Mansoor (Kwimba), Idi Kassim Idi (Msalala) na Mbunge wa Viti Maalum, Shally Raymond.

Wengine ni Pauline Gekul (Babati Mjini), Zubery Kuchauka (Liwale), Emmanuel Ole Shangai (Ngorongoro), Idd Mpakate (Tunduru Kusini), Hasani Kungu (Tunduru Kaskazini), Vedastus Mathayo (Musoma Mjini) na George Mwenisongole (Mbozi).

Kadhalika yumo Nicodemas Maganga (Mbogwe), Twaha Mpembenwe (Kibiti), Shabani Shekilindi (Lushoto), Innocent Kalogeres (Morogoro Kusini), Flatey Maasay (Mbulu Vijijini), Alfred Kimea (Korogwe Mjini) na Taufiq Turkey (Mpendae).

Mbali na waliokuwa wabunge, wapo pia walikuwa matu maarufu akiwamo Rais wa Klabu ya Yanga, Hersi Said, Makamu wake Arafat Haji na mkuu wa wilaya wa zamani wa Hai, Lengai Ole Sabaya.

Akizungumzia uteuzi huo, Mhadhiri wa Sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda amesema mabadiliko ya Katiba ya Katiba ya CCM iliyofanyika Januari 2025 na yaliyofanyika Julai 26, 2025 yameongeza demokrasia ndani ya chama hicho kwa kuongeza majina ya watia nia, lakini pia yameiminya demokrasia hiyo kwa kuipa nafasi Kamati Kuu kuwachagulia wajumbe watia nia wa kuwapigia kura.

“Mabadiliko yameongeza demokrasia kwa kuongeza idadi ya wagombea kutoka watatu hadi watano, kwa sababu watia nia wameongezeka sana, lakini yamepunguza kwa sababu kamati kuu ndio inateua majina ndipo wajumbe waje wapige kura.

“Unajua mtia nia ndio anayejuana na wapiga kura kule jimboni, kwa hiyo ilitakiwa wajumbe ndio wawachague huko chini kabla ya kwenda kamati kuu. Wangewaacha tu, hata wakijitokeza watia nia 40, wapigiwe kura, halafu Kamati kuu iamue mwishoni,” amesema Dk Mbunda.

Ameongeza: “Mwaka 2020 wajumbe ndio walichagua watia nia kisha wakapelekwa kamati kuu. Japo pia kulikuwa na ukandamizwaji wa demokrasia kwa sababu kamati kuu zilichagua mtu bila kujali ameshika nafasi ya ngapi na hivyo kupuuza uamuzi wa wajumbe huko chini,” amesema.

Julai 26 Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan aliitisha Mkutano Mkuu maalum uliofanyika kwa njia ya mtandao Julai 26 ukiwa na ajenda moja tu ya kufanya marekebisho ya Katiba ya CCM ya mwaka 1977 (toleo la Mei 2025).

Kifungu cha Katiba ya CCM kilichofanyiwa marekebisho ni Ibara 105(7) F inayohusu majukumu ya Kamati Kuu katika mchakato wa uteuzi wa wagombea wa CCM ngazi ya Ubunge na Ujumbe Baraza la Wawakilishi. Kifungu hiko kimeongezewa maneno “isipokuwa kama Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itaamua vinginevyo.”

Makundi ya urais

Akizungumzia makundi ya urais ndani ya chama hicho, Dk Mbunda amesema huwa hayakosekani na ni lazima yachezeshe siasa za ndani.

“Ndio maana utashangaa mbona Fulani mwenye ushawishi mkubwa ameachwa na wengine wanaoonekana kutokuwa na nguvu ndio wamewamechukuliwa!”

Waliopita bila kupingwa, familia za marais

Katika uteuzi huo, watia nia watatu wamepita bila kupingwa, akiwamo Waziri wa Nishati na Naibu Waziri Mkuu, Dk Doto Biteko, Ridhiwani Kikwete (Chalinze) na Salma Kikwete (Nchinga), hali iliyozusha gumzo hasa kwa wanafamilia wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Dk Mbunda amesema hatua hiyo ni familia ya Kikwete kujionyesha kwamba bado inakubalika nchini na kwamba, “kuna siasa zinachezwa.”

Kupitishwa kwa wanafamilia hayo kunakuja wakati hivi karibuni Rais mstaafu Kikwete amekuwa akionekana katika shughuli mbalimbali za Rais Samia ikiwamo ya uzinduzi wa Kanisa la Arise and Shine la Mtume na Nabii Boniface Mwamposa Julai 5, 2025 Kawe jijini Dar es Salaam, ambapo Rais alimwita Kikwete kuwa ni bosi wake.
Soma pia: Rais Samia azindua kanisa la Mwamposa

Hata Rais Samia alipozindua Dira ya Taifa uliofanyika jijini Dodoma Julai 16, 2025, Rais mstaafu Kikwete ndiye aliyezungumza kwa niaba ya viongozi wastaafu.

Rais Samia azindua Dira ya Taifa

Ikumbukwe kwamba, Januari 19, 2025 wakati wa kumpitisha Rais Samia kuwa mgombea pekee wa CCM, Rais mstaafu Kikwete ndiye aliyetoa ufafanuzi wa kupitisha azimio la mkutano mkuu baada ya baadhi ya wajumbe kuanza kuhoji mchakato.
Soma pia: Utata Samia kupitishwa kuwa mgombea urais CCM

Pamoja na familia ya Kikwete, familia za marais wastaafu pia zimeng’ara, ambapo kwa Rais mstaafu, Hayati Ali Haasan Mwinyi, mbali na Dk Hussein Mwinyi kuwa mgombea urais wa Zanzibar, wamo pia ndugu zake akiwamo Abdula Ali Mwinyi, Asma Ali Mwinyi na Abbas Ali Mwinyi.

Kwa Hayati John Magufuli, Jesca Magufuli naye amepitishwa, huku kwa Rais Samia, akipitishwa Wanu Hafidh Ameir anayegombea jimbo la Makunduchi.

Bunge la 13 litakuwaje?

Kutokana na uteuzi huo, Dk Mbunda anaona kuna uwekeno wa kuja kuwa na Bunge dhaifu likiwa limejaza wabunge wa CCM wasioibua hoja kali kwa Serikali.

"Rais Samia alifanya kosa kubwa Mei 30, 2025 alipowaambia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kuwa wasi- Gwajimanize chama chao, akionyesha kutofurahishwa na Mbunge wa Kawe, Askofu Josephat Gwajima ambaye ni kiongozi wa kanisa la Glory of Christ (Ufufuo na Uzima)," amesema Dk Mbunda.

Soma: Tusigwamimanize chama.

Juni 2, 2025 Serikali ililifungua kanisa la Ufufuo na Uzima na mpaka sasa halijafunguliwa.

Mbali na Gwajima, Rais Samia alionyesha kutofurahishwa na Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina akisema mbunge huyo anapaswa kuwa wa kitaifa na sio wa jimbo.
Soma pia: Rais Samia amchana Mpina


Kutokana na hali hiyo, Dk Mbunda amesema, “Kwa uchaguzi unaokuja, tusitarajie kuwa na bunge lenye nguvu na hasa kwa kuiwa CHADEMA hawashiriki uchaguzi, basi litakuwa ni bunge lisilo na nguvu. Wewe fikiria Bunge linaloishia limekaa miaka mitano bila kuwa na mbunge yoyote aliyetoa hoja binafsi, kwa hali hii ya sasa ndio litakuwa dhaifu liko la sasa.”

Usawa wa jinsia

Kwa upande mwiingine, akizungumzia usawa na jinsia katika uteuzi huo, mwanasheria Dk Victoria Lihiru, amesema orodha iliyotolewa haionyeshi jinsia za wagombea, jambo linalowapa wakati mgumu watetezi wa haki za kijinsia kupima.

“Kwa kuwa hiki chama kina Umoja wa Wanawake (UWT), tulitarajia kuwa wanapoingia kwenye vikao vya uteuzi wanabainisha ni wanawake wangapi wamepitishwa, ili tuweze kupima jinsia ilivyozingatiwa.

“Kwa hali ilivyo, ni ngumu kujua baadhi ya majina kama ni wanawake au wanaume,” amesema.
 
Back
Top Bottom