Utu uzima umebadili mtazamo wangu kuhusu mafanikio

Utu uzima umebadili mtazamo wangu kuhusu mafanikio

Peter Mwaihola

JF-Expert Member
Joined
Jun 23, 2022
Posts
276
Reaction score
460
Nikiwa chini ya miaka 20 nilikuwa nawaza sana mambo makubwa makubwa umasikini na shida niliona kama vitu vya kupita.
Nilikuwa najiuliza na kushangaa sana inakuwaje mtu anaishi mpaka anafika miaka 30 hana nyumba, hajaoa hata hawazi kununua gari? Huo ni uzembe bwana nilijijibu mwenyewe.

Sikuwahi kufikiria kuwa watu wazima walio masikini wana juhudi kwenye maisha yao lakini hawafanikiwi tu, wote niliwaona kama wavivu wa maisha.

Nilikuwa naamini kuwa baada ya kumaliza masomo nitakuwa na maisha yangu na nitaweza kufanikisha mambo mengi kabla hata ya umri wa miaka 35.
Akili yangu haikuwekeza sana kufikiria nini kitatokea, niliwaza tu kuwa nisome kwa bidii, nimalize masomo mambo mengine yatafuata.

Hata hivyo baada ya miaka 20 hali ikaanza kubadilika, nikaanza kuona giza, ukungu ukatanda mbele ya matarajio yangu, nikaanza kuhisi kuwa huenda kuwa mtu mzima sio kazi nyepesi.

Kuna wakati ukafika nikaanza kuona aibu kuomba hela kwa watu niliowategemea hapo awali licha ya kwamba wao waliendelea kunijali na hawakuonyesha kubadilika.

Nikaanza kugundua kuwa zama zimebadilika napaswa kusimama mwenyewe kabla ya kutafuta pa kuegemea.

Mtazamo wangu ukazidi kubadilika siku hadi siku, nikaanza kuwaheshimu wakubwa wanaopambana kila siku hata kama wanaonekana hawapati chochote.

Kuna siku nilistahajabu sana, ilikuwa ni msimu wa kuwapokea wanafunzi wa mwaka wa kwanza chuoni kwetu nikiwa mwanafunzi wa chuo hicho wa mwaka wa tatu.
Baada ya wiki mbili w niliwasikia wanafunzi wa kiume watatu wanapanga kutembelea eneo la nje ya mji kutoka chuoni kwetu ili wakaangalie viwanja vinavyowafaa ili pesa ya kujikimu ikitoka watumie pesa hiyo kununua viwanja hivyo wajenge nyumba.

Sikutaka kuwashauri kitu, niliwaacha wafunzwe na ulimwengu kwakuwa nilijua wazi kuwa mimi mwenyewe nilikuwa na mawazo kama yao miaka kadhaa iliyopita.

Baada ya mwezi kupita niliwarudia na kuwauliza mliishia wapi lile jambo? hakuna aliyenijibu nyuso zao ndizo zilisadifu kuwa vichwa vyao vimejaa mambo mengi ambayo hayakidhi bajeti ya mifuko yao.

Kadri ninavyosogea mbele napata funzo jipya, kuwa urahisi wa safari hautazamwi kwa kuangalia ulikotoka bali uendako.

Sasa nimekuwa mtu mzima, naheshimu jitihada za kila mtu.

Ukioa nakupongeza, ukinunua baiskeli nakupongeza, ukijenga nyumba chumba kimoja nakupongeza ukibarikiwa kufanya mambo makubwa kama kumiliki biashara na magari ya kifahari nakupongeza kwakuwa sio kazi rahisi kupiga hatua kwenye maisha.

Wapambanaji ni wengi Ila wanaofanikiwa ni wachache, ziheshimiwe jitihada za mwanadamu.

© Peter Mwaihola
1736577613089.jpg
 
Back
Top Bottom