- Source #1
- View Source #1
- Source #2
- View Source #2
Nimekuwa ni mtumiaji wa panadol katika kusafisha pasi yangu inapochafuka, lakini nimepigwa na butwaa na kupata wasiwasi baada ya kukutana na post mtandaoni kuwa matumizi hayo ya panadol ni hatari kwa afya ya binadamu kutokana na kuzalisha sumu kali, hili uhalisia wake ni upi?
- Tunachokijua
- Tovuti ya health direct ya nchini Australia inafafanua kuwa Paracetamol ni dawa ambayo inatumika kushusha nguvu ya homa, maumivu madogo hadi ya kati mathalani maumivu ya kichwa, maumivu wakati wa hedhi, mafua nk, lakini pia huweza kutumika mtu apatapo homa ya mwili, maumivu makubwa na kadhalika. Watu wengi hufikiri wanapotumia paracetamol na maumivu kupungua au kuisha hudhani wamepona la hasha kwani haitibu chanzo cha maumivu bali kazi yake ni kupunguza maumivu.
Matumizi yaliyopitiliza kiwango ni hatari kwa afya ya binadamu kwani huweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo kuharibiwa kwa ini na hata kusababisha kifo.
Licha ya kutumiwa kama dawa inayopunguza maumivu kwa binadamu, lakini baadhi ya watu wamekuwa wakitumia Paracetamol ya ajili ya kusafishia pasi ya kunyooshea nguo baada ya kuchafuka kutokana na nguo zilizoungua na kushikilia sehemu ya pasi, ambapo usafishaji huo huhusisha pasi iliyounganishwa na umeme na kupata joto kali na hapo ndipo vidonge hivyo vinahusika kusugua sehemu ya pasi iliyochafuka.
Matumizi hayo ya paracetamol katika kusafisha pasi yameibua wasiwasi kwa baadhi ya watu kutokana na uwepo wa hoja kuwa unapotumia kusafisha pasi kwa kutumia vidonge hivyo husababisha kuzalishwa kwa kemikali inayotoka kwa njia ya mvuke na kuhatarisha afya ya binadamu.
Je, ni upi uhalisia wa hoja hiyo?
JamiiCheck imepitia tafiti na vyanzo mbalimbali vya kuaminika ambapo imebaini kuwa utumiaji wa vidonge vya Paracetamol ni si salama kwa afya ya binadamu kwani kitendo hicho huzalisha kemikali ambayo ni hatari inapoingia kwenye mwili wa binadamu kwa njia ya hewa.
Kwanza katika kutafuta uhalisia wa jambo hili JamiiCheck ilianza kwa kutaka kubaini kama matumizi ya paracetamol yana madhara kwa binadamu ikitumiwa katika chakula ambapo, tovuti ya science direct ikieleza juu ya matumizi ya kemikali inayojulikana kama ‘acetaminophen’ inayopatikana kwenye paracetamol katika kupikia nyama ili ilainike inabainishwa kuwa inapotumiwa kupikia huvunjika na kuyeyuka na kutengeneza sumu inayojulikana kama ‘4-aminophenol’ ambayo huweza kupelekea kuharibiwa kwa ini na figo na hata kushindwa kufanya kazi kabisa.
Maktaba ya tiba ya taifa ya nchini Marekani (National Library of Medicine) inaweka bayana kuwa Kemikali hiyo ya 4-Aminophenol huweza kusababisha madhara kwenye ngozi ya binadamu, pia ikivutwa kwa njia ya hewa inaweza kusababisha Methemoglobinemia ambapo hupelekea kukosekana kwa oksijeni kwenye damu, lakini pia inaweza kuchochea Bronchial asthma ambao ni ugonjwa unaosababisha njia za hewa kufunguka na kufungwa, hivyo kuleta ugumu wa kupumua na kikohozi ambapo dalili zake zinaweza kuwa maumivu ya kichwa, kupumua kwa shida, kuchoka nk.
Kemikali za Aminophenols zinaweza kufyonzwa kwa urahisi kupitia ngozi na kuleta madhara kwenye mapafu, lakini pia kemikali hizi hushusha uwezo wa damu kubeba hewa ya oksijeni, matatizo ya ngozi, na uharibifu wa ini, figo, na ubongo pamoja na mabadiliko ya genetiki.
Aidha Kwa mujibu taarifa iliyochapishwa katika tovuti ya premium times ya nchini Nigeria, inayohusu matumizi ya vidonge vya paracetamol kwenye chakula, inabainisha kuwa Paracetamol ikichomwa kwa namna yoyote kwa kutumia moto huvunjikavunjika, kuyeyuka na kuzalisha kemikali ijulikanayo kama ‘four-amino phenol’ ambayo inaweza kusababisha kufeli kwa figo na hata ini kuathirika.
Ili kulinda uimara wa afya zetu ni muhimu kuepuka matumizi yasiyofaa dhidi ya paracetamol jambo ambalo linaweza kusaidia kuondoka na gharama ambazo zingesababishwa kutokana na madhara husika.
Njia salama kusafishia pasi
Pasi ni kifaa muhimu katika maisha ya kila siku kutokana na namna ambavyo imekuwa na mchango mkubwa kwenye unadhifu wa mavazi hasa kwa kuondoa mikunjo ya nguo. Mara pasi ichafukapo kwa kunasa mabaki ya nguo yaliyoungua huleta changamoto katika unyoshaji wa nguo kutokana na kuacha madoa kwenye nguo kutokana na uchafu huo.
Watu wengi wamekuwa wakitumia vidonge vya Paracetamol kusafishia pasi njia ambayo inaonekana kuwa ni hatari kwa afya ya binadamu.
Tovuti ya kampuni ya teknolojia ya Phillipes inasisitiza Wakati wa kusafisha pasi kwanza hakikisha pasi hiyo haijaunganishwa na umeme huku ikiwa imepoa kabisa. Kwa pasi ambayo imechafuka kwa kiwango kidogo unaweza kutumia maji ya vuguvugu yenye sabuni ambapo kwa kutumia sponji unaweza kusugua taratibu ili kuondoa uchafu huo.
Endapo bado pasi haijasafishika baada ya kutumia maji yenye sabuni hakikisha pasi hiyo imekauka, ambapo badala yake unaweza kutumia dawa ya meno, ukitumia kitambaa kizito kidogo na kuweka dawa ya meno juu yake au kwa kupaka sehemu iliyochafuka kisha kusugua vizuri madoa hayo.
Pia, unaweza kutumia Vinegar ambapo unachanganya Vinegar na chumvi kiasi kisha upashe moto mchanganyiko huo, epuka kuchemsha kabisa huku ukihakikisha unaikinga mikono yako kwa kuvaa ‘gloves’ na kupitia mchanganyiko huo tumia sponji au kitambaa laini kusugua vizuri sehemu ya pasi iliyochafuka.
Pia sehemu unayotumia kusafishia unaweza kutanguliza kitu kwa chini ili kukinga majimaji yanayodondoka wakati wa kusafisha. Kumbuka, njia zote hapo juu unatakiwa kuhakikisha pasi haiko kwenye umeme na iwe imepoa kabisa.