Awali ya yote itakuwa mujarabu nikianza kuelezea kwa kifupi maana ya maneno uwajibikaji na utawala bora. Aidha maneno hayo ni kama chanda na pete. Ni kwa nadra sana unaweza kuyatenganisha.
Uwajibikaji ni neno ambalo lipo katika mawanda mapana hususan katika maisha ya mwanaadam. Neno hilo limetamalaki katika maisha ya kifamilia, kijamii, kisiasa na kiroho; ambayo nitayadadavua kwa kifupi kama ifuatavyo:
Kifamilia; uwajibikaji ni ukosaji hiari katika kufanya jambo ama jambo linalomlazimu mtu kulitimiza na hana hiari nalo katika kulifanya. (“Hii ni tafsiri iliyotolewa na kamusi ya Kiswahili sanifu iliyotungwa na kuhaririwa katika sehemu ya kamusi ya Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es salaam.”)
Mathalani katika familia, baba wa familia anawajibika kuitunza familia yake kwa maana ya mke na watoto wake. Kadhalika mama wa familia naye ana majukumu yake yampasayo kuyafanya. Kwa mfano; hapa Tanzania wajibu wao huo umo ndani ya sheria za nchi ambazo zinamlazimisha kila mmoja wao kutekeleza yanayompasa kufanya vinginevyo kwa kawaida sheria huchukua mkondo wake.
Kijamii; uwajibikaji ni hali ya kiongozi na mtendaji kuwa tayari kujibu, kubeba dhamana na kutoa maelezo kwa wananchi juu ya maamuzi au matendo. Utaratibu huo umejidhihirisha katika jamii mbalimbali hususan kama vile wamasai katika utaratibu wao wa maisha.
Kisiasa; aidha uwajibikaji maana yake ni itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani ambayo ni msingi wa kuendesha uchumi wake, utamaduni na mwenendo mzima wa maisha ya jamii hiyo; au mfumo wa mawazo yaongozayo utawala wa Serikali ya Nchi. Kwa mfano siasa ya ubepari au siasa ya ujamaa na kujitegemea.
Maana nyingine ya Siasa ni utaratibu wa utekelezaji au uendeshaji wa jambo kwa kutumia busara na hekima ili kufikia lengo linalotarajiwa. (Tafsiri hiyo inatoka katika kamusi ya Kiswahili Sanifu Taasisi ya uchunguzi wa Kiswahili Chuo Kikuu cha Dar es Salaam).
Kadhalika kutoka “Jamii Forums” imefafanuliwa kwamba, uwajibikaji una maana kadhaa:- Mosi kuwepo mfumo wa udhibiti wa matumizi ya madaraka; Pili kuwepo utaratibu wa kuwalazimisha viongozi kutekeleza yanayowapasa kuyafanya bila kukiuka wajibu wao. Vilevile kuwepo utaratibu wa kuwaadhibu Viongozi wale wanaotumia madaraka yao vibaya au wanashindwa kutekeleza wajibu wao.
Binadamu walio wengi wanaamini katika uwepo wa maisha yanayoonekana na yale yasiyoonekana. Kwa kirefu tumeelezea uwajibikaji katika muktadha wa maisha yanayoonekana. Lakini katika maisha yasiyoonekana ambayo kwa walio wengi wanaamini kuwa yapo; uwajibikaji pia una nafasi yake. Uwajibikaji huo unatambulika kuwa ni wa kiroho unaongozwa na imani ya mtu ambayo hufanya alazimike kutenda kwa kadri ya wajibu wake unavyompasa. Usipotenda kwa kadri unavyotakiwa kuna amri zilizoainishwa kwa kadri ya imani husika ambazo utahukumiwa nazo na Mwenyezi Mungu baada ya kifo chako.
Kwa ujumla itoshe tuu kusema kwamba uwajibikaji ni msukumo wa ndani unaomlazimisha mwanadamu kutenda mambo mema yampasayo kutenda kwa ajili ya wenzake hata bila kulazimishwa na sheria. Lakini kutokana na hulka ya maumbile ya binaadamu kuwa uovu ni sehemu ya maisha yake; uwajibikaji wowote unaomhusu kuutenda aghlabu unaambatana na sheria ambazo zitamlazimisha kutii wajibu wake.
Katika nchi nyingi za “ulimwengu wa kwanza” zinazingatia kwamba uwajibikaji unaomhusu mwanadamu katika masuala yote unatungiwa mifumo mizuri ya sheria ambayo ndiyo inadhibiti uwajibikaji wa aina yoyote katika maisha yao. Na mifumo hiyo kwa hakika inasimamiwa barabara.
Kwa upande mwingine nchi zinazoitwa za “Dunia ya tatu” hazina mifumo mizuri ya sheria inayosimamia uwajibikaji na hivyo kuzifanya ziendeshe mambo yao shaghlabagala katika nyanja nyingi kama vile za uchumi, utamaduni, siasa na kadhalika. Mifano katika kadhia hiyo ipo lukuki katika Nchi yetu ya Tanzania na Nchi nyingine za “dunia inayoitwa ya tatu”. Mathlani tukiongelea maswala ya uchumi nchini Tanzania ni kwamba hali yake imejikita katika msemo usemao “kila mbuzi hula kufuatana na urefu wa kamba yake”. Kutokana na falsafa hiyo, ufisadi umetamalaki katika kila eneo la uchumi. Umeota mizizi ambayo kuing’oa kunahitaji juhudi za ziada.
Katika awamu mbali mbali wametokea viongozi walioonyesha chuki na kujaribu kuutokomeza ufisadi ambao ulikuwa unaitafuna nchi. Kwa mfano kiongozi wa kwanza kabisa wa Tanzania baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere yeye binafsi alikuwa mtu muadilifu sana aliyekuwa na dhamira njema sana na nchi na wananchi wake. Alifanikiwa katika mengi lakini katika ufisadi watu walificha makucha yao tuu.
Alipoondoka tu madarakani nchi ililiwa kama mchwa ulavyo mbao laini. Hali hiyo ya ufisadi imekuwa kama joto la kupanda na kupungua kutegemea kiongozi anayekuwepo madarakani. Kiongozi wa hivi karibuni ambaye alionyesha nia thabiti ya kutaka kutokomeza ufisadi alikuwa ni JOSEPH JOHN POMBE MAGUFULI. Lakini kwa bahati mbaya hakutengeneza mifumo imara ambayo ingelinda uwajibikaji na utawala bora. Alitegemea zaidi usimamizi wa mtu binafsi ambao pindi anapokuwa hayupo ni rahisi kusambaratishwa. Kwahiyo baada ya kufariki kwake polepole nchi ilianza kurudi kwenye lindi la ufisadi. Hata hivyo kifo cha Kiongozi huyo kilizua maneno mengi ikionekana kwamba kifo hicho kilipangwa na maadui ambao hawakupenda mabadiliko ya kuitoa nchi katika lindi la ufisadi. Hali ya namna hiyo ya kuwaua wanamapinduzi imejitokeza pia sehemu nyingine duniani hususani nchi za dunia ya tatu. Mifano ipo mingi kama vile THOMAS SANKARA wa Burkinafaso, MUAMAR GADAFFI wa Libya, SAMORA MACHEL wa Msumbiji, PATRICE LUMUMBA wa Congo aliyeuawa miaka ya mwanzoni kabisa ya uhuru wanchi za kiafrika. Orodha ni ndefu lakini kwa uchache hao wawe ni mfano.
Kama ilivyoelezwa awali kwamba uwajibikaji na utawala bora ni kama vile chanda na pete; basi kunapokuwa na uwajibikaji uliotukuka mahali Fulani, utawala bora hupata njia ya mteremko katika kufanya kazi yake.
Ni vema kabla ya kuendelea ikaeleweka “tawala au utawala maana yake ni nini? Utawala maana yake ni kuwa na amri juu ya matendo na kila sehemu ya maisha ya watu; kuweka nchi au watu chini ya amri (kama vile katiba) mathlani kama vile ambavyo wakoloni walivyotawala Afrika; ijapokuwa haukuwa utawala bora. Ili uwajibikaji na utawala bora ufanye kazi yake kwa ufanisi, dunia inatembea katika mifumo mbalimbali ambayo kila mtawala anajinasibu kwa ufanisi wa mfumo anaotumia. Kwa uchache niainishe mifumo ambayo inatumika kwa sasa. Mfumo unaopigiwa chapuo sana hususan kwa nchi za magharibi ni mfumo wa kidemokrasia. Mifumo mingine ni ile ya kifalme, kikomunisti, kisoshalisti, kibepari, kijeshi na kadhalika.
Iwe iwavyo uwajibikaji ni uti wa mgongo wa mafanikio wa mfumo wowote palipo na uwajibikaji aghlabu na uadilifu huwepo na hivyo kwa pamoja huzaa UWAJIBIKAJI NA UTAWALA BORA.

Upvote
1