SoC01 Uwekezaji wa Vijiji vya kisasa katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja

SoC01 Uwekezaji wa Vijiji vya kisasa katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja

Stories of Change - 2021 Competition

Valentine Bon

New Member
Joined
Jul 14, 2021
Posts
2
Reaction score
2
Utangulizi
Tanzania kiuhalisia bado ni nchi ambayo inategemea uchumi wake kukua kupitia vijiji vyake ambavyo shughuli za watu wake wengi hutegemea kilimo. Mbali na kutegemea kilimo zaidi na shughuli zingine, lakini bado vijiji vingine viko nyuma zaidi katika nyanja za kijamii, kiuchumi na tekinolojia. Hivyo ni kusema kwamba hakuna uwekezaji mkubwa katika nyanja hizo.

Ni kweli kwamba takribani asilimia 75 ya watanzania wote kwamujibu wa sensa ya 2012 hukaa vijijini na idadi ndogo hupatikana mjini ambapo wao shughuli zao kubwa ni kazi za maofisini, kazi za viwandani na biashara kwa ukubwa wake. Bado hoja inabaki kuwa ni sehemu gani zaidi huzalisha malighafi za viwandani, mazao ya biashara. Ni kweli ni vijijini. Hapo ndipo swali juu ya uwekezaji wa vijiji vya kisasa linaibuka. Kwa nini uwekezaji vijijini usipewe nguvu zaidi na kuhakikisha bajeti kubwa inaelekezwa huko ili uzalishaji uwe wa kisasa ambao utachochea kukua kwa uchumi wa nchi na mtu mmoja mmoja?

Dhana vya vijiji vya kisasa
Hii dhana ya vijiji vya kisasa katika nchi hizi zinazoendelea hasa Tanzania katika karne hii ya 21 ambayo ukuwaji wa chumi nyingi duniani hutegemea sayansi na teknolojia. Ni ukweli kwamba Tanzania bado vijiji vyake vingi sekta nyingi ziko nyuma mno.

Kuanzia kanda ya ziwa, kanda ya kaskazini, magharibi, kanda ya kati, kanda ya pwani, nyanda za juu kusini mwa Tanzania bila kusahau Zanzibari; kuna vijiji vingi ambavyo watu wake wanajishughulisha na kazi mbalimbali hasa shughuli za kilimo. Lakini ni kweli kwamba katika vijiji hivyo miundombinu bado ipo chini mno kwa kiasi kikubwa. Miundombinu ya mabarabara, mashule, afya kwa ujumla wake ipo nyuma zaidi. Swali ni kwamba unawezaje kukuza uchumi wa nchi na ustawi wa watu takribani asimilia 75 inayozalisha sana, kama sekta ya afya haiko imara, hakuna shule za kutosha pia kuna upungufu mkubwa wa walimu. Vilevile sekta ya miundombinu na mawasiliano nayo bado duni, na ndiyo ambayo hutumika kupitishia mazao kutoka mashambani kwenda viwandani hasa mijini, ambapo vinapopatikana viwanda vingi? Kwa tafsiri hii ni kweli kwamba inawezekana kuona uchumi unakua, lakini ukuaji wake hauwezi kuakisi hali halisi ya ustawi wa mtu mmoja mmoja na ongezeko la idadi ya watu.

Mamlaka husika yani serikali yenye dhamana inawajibu wa kuhakikisha kuwa inatenga bajeti kubwa ambayo itaelekezwa kuboresha na kuvifanya hivi vijiji kuwa vya kisasa na kuendana na ukuaji wa teknolojia ya karne hii ya 21. Mabarabara ya kisasa ya lami, vivuko, miundombinu ya kimawasiliano ambayo hufika kila kona, sekta ya afya, elimu na sekta nyingine kwa ujumla. Kwa kutekeleza hayo sekta hizo zitachochea mnyororo wa thamani na uchumi kukua. Mfano mazao yanapovunwa itarahisisha kufika masokoni na viwanda vilivyoko huko mijini kwa wepesi na haraka zaidi.

Katika sekta ya afya, ni kweli vijiji vingi Tanzania sekta ya afya inachechemea. Kama wasemavyo afya ni mtaji na ndio mtaji namba moja. Rasilimali watu hutegemea afya imara ili kazi zisisimame. Kwa upande wa vijiji vingi bado sana suala la sekta ya afya lipo nyuma. Serikali bado haijawekeza kiukamilifu katika vituo vya afya kwa wingi, na pia utoaji wa elimu ya afya bado uko nyuma sana, mbali na kuwepo na sekta binafsi zinazojitolea bila malipo na zile za malipo. Kama nguvu kazi ikiwa inauhakika wa huduma ya afya itakuwa ni rahisi kupata matibabu na kurejesha afya imara na kuendelea katika uzalishaji. Hivyo kuzungumzia uwekezaji wa kisasa vijijini una maana pana katika sekta ya afya ambayo itakuwa imara katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi.

Elimu ni suala la msingi zaidi katika karne hii ya 21. Elimu ni sekta mtambuka na ndio uchumi wenyewe. Elimu ni msingi wa kila nyanja hasa karne hii ambayo teknolojia ya mawasiliano ni injini ya uchumi katika mapinduzi ya viwanda vya kisasa. Vijiji vingi Tanzania vinahitaji uwekezaji mkubwa wa elimu isiyo na mabataka. Elimu yenye usawa kwa watoto wote wakitanzania, inayofanana na isiyo na upendeleo kwa wale waishio mjini na vijijini. Shule zinazojengwa vijijini ziwe za kisasa na zijengwe za kutosha zitakazo ondoa tatizo la wanafunzi kutembea umbali mrefu. Pia shule ziwekewe nishati ya umeme na somo la tehama lifundishwe mashuleni hii itawasaidia wanafunzi wanaosoma huko vijijini kuendana na usasa wa ukuaji wa teknolojia ya mawasiliano. Hii itasaidia upatikanaji wa maarifa kuwa bora zaidi.

Mambo mengi yakizingatiwa na kuboreshwa katika elimu, mfano mtoto wa mkulima aishie kijijini atakuwa na uhakika wa kupata elimu bora na si bora elimu. Kwa maana hiyo vijiji vitazalisha wasomi ambao watakuja kusaidia jamii wanazotoka. Mpaka sasa Tanzania haijafikia uwekezaji mkubwa wa sekta ya elimu, na Wataalamu wa uchumi wanasema ili nchi yeyote ikue kiuchumi ni lazima iwekeze katika sekta ya elimu kwa asilimia za juu zaidi. Kwa mfano huwezi kuzungumzia nchi ya Marekani au Uingereza bila kusemea sekta ya elimu jinsi inavochangia pato la taifa lao. Pia mtaala wa elimu ulio bora hasa unaolenga kuwapa maarifa wanafunzi jinsi ya kutatua na kukabiliana na mazingira yanayowazunguka, na si kuwa na mtaala unaompa maarifa mengi yasiyo na mchango mkubwa wa kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Sekta ya mawasiliano, miundombinu na uchukuzi ni muhimu sana. Hasa sekta ya mawasiliano ni nyenzo muhimu muhimu sana katika uchumi wa kisasa. Ni sekta ambayo husisimua uchumi na kufanya nchi husika chumi zake kukua kwa haraka zaidi. Ni kweli kuwa vijiji vya Tanzania sekta ya mawasiliano ipo nyuma mno. Mapinduzi haya ya nne na ya tano ya viwanda ambayo yanategemea zaidi sekta ya mawasiliano na ni sekta mtambuka, ni lazima serikali itazame fursa hii ya kukuza uchumi kwa kuhakikisha uwekezaji vijijini kwenye sekta ya mawasiliano ili nguvu kazi ipate huduma ya mawasiliano ya uhakika. Kuwepo kwa huduma nzuri ya mawasiliano itawasaidia kuwasiliana kwa haraka zaidi hata mauzo ya mazao kurahisishwa kwa njia ya mtandao na biashara kwa ujumla itafanyika kwa njia ya mtandao pale panapohitajika. Hivyo dhana ile ya kutaka kuifanya Tanzania inayostawi kiviwanda ni lazima uwekezaji wa mkubwa wa sekta ya mawasiliano ufanyike kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa malighafi ambapo ni vijijini.

Hudumuma ya maji pia lazima iwe kipaumbele kwenye uwekezaji huu. Tatizo la miundombinu ya maji katika vijiji hivi bado ni kubwa licha ya kuwa na vyanzo asili vya maji ila huduma ya maji safi na salama bado imekuwa duni katika vijiji vingi. Upatikanaji wa maji safi na salama itakuwa ni chachu ya kuboresha afya za watu. Pia mbali na kuanza na visima vya kuchimba lazima usasa ujikite kuwekeza kwenye maji ya bomba ambayo yatasadia kuokoa muda.

Matarajio/Matokeo

Kama uwekezaji ukifanyika vizuri kwenye vijiji na kuwa vya kisasa bila shaka itaongeza mnyororo wa walipa kodi. Tatizo la vijana kutaka kukimbilia mijini kutafuta maisha litapungua maana huduma za msingi zitapatikana hukohuko vijijini walipo. Mbali na hayo hali za maisha ya watu zitaimarika pia. Malighafi zitakuwa za kutosha na kuvutia wawekezaji wa ndani hata wa nje, kutokana na uwepo wa miundombinu iliyo bora na rafiki. Hakika uwekezaji ulio bora ndio shabaha ya uchumi ulio imara.

Hitimisho
Dhana hii ya uwekezaji wa vijiji kuwa vya kisasa bila shaka itaenda kukuza uchumi wa mtu mmoja mmoja na nchi kwa ujumla. Serikali ni lazima ihakikishe inatenga bajeti na sehemu kubwa ya bajeti ilenge kwenda kuimalisha hivi vijiji. Pia serikali ikiimalisha sekta muhimu wawekezaji watavutiwa kuwekeza na hiyo itaisaidia serikali kujikita kwenye sekta mtambuka tu na kutunga sera na sheria zitakazo imalisha ukuaji wa chumi.

Ni kweli kabisa mipango na mikakati inaweza kuwa mizuri, ila isitekelezeke au kwenda kwa kuchechemea kutokana na ubinafi, ufisadi na changamoto nyingi ambazo zinatatulika. Watu huishi kwa tamaduni zao, ila tabia inaweza kuwa si sehemu ya tamaduni hiyo. Hivyo viongozi wanawajibu wa kulinda viapo vyao na usawa katika sheria kwa wote ni jambo la heri. Katiba imara hutengeneza chumi zilizo imara na tamaduni yenye udemokrasia wenye kufuata sheria hujenga taifa imara.
 
Upvote 5
Una wazo zuri sana sana. Ingekuwa vizuri sana ukaboresha kwa kuandika namna vijiji vinavyoweza kugeuzwa vya kisasa. I mean maelezo yako yamekuwa ya jumla sana bila kuainisha kwa undani. Nikupe mfano. Niliwahi kutembelea mkoa wa Kilimanjaro eneo linaitwa Mabogini. Huko wajapani walikuwa wamefanya kazi nzuri sana (sadly haikudumu baada ya mradi kukabidhi ngozi nyeusi waendeshe). Walichofanya ni kuchimba mfereji kutoka kwenye source ya maji ya mto, halafu wakajenga vitalu vikubwa sana vya kulimia mpunga. Vile vitalu vilikabidhiwa kwa wenyeji na walikuwa wanalima mpunga kwa kufuata taratibu na sheria za bodi iliyokuwa inaongoza. Huu mradi uliwasaidia sana wenyewe na kujikwamua kutoka kwenye umaskini. Ndiyo maana nikasema wazo lako ni zuri sana na kwa kuanzia serikali ingeangalia ni mazao gani yanastawi katika kila sehemu halafu wapeleke utaalam kama walivyofanya wajapan.
 
Una wazo zuri sana sana. Ingekuwa vizuri sana ukaboresha kwa kuandika namna vijiji vinavyoweza kugeuzwa vya kisasa. I mean maelezo yako yamekuwa ya jumla sana bila kuainisha kwa undani. Nikupe mfano. Niliwahi kutembelea mkoa wa Kilimanjaro eneo linaitwa Mabogini. Huko wajapani walikuwa wamefanya kazi nzuri sana (sadly haikudumu baada ya mradi kukabidhi ngozi nyeusi waendeshe). Walichofanya ni kuchimba mfereji kutoka kwenye source ya maji ya mto, halafu wakajenga vitalu vikubwa sana vya kulimia mpunga. Vile vitalu vilikabidhiwa kwa wenyeji na walikuwa wanalima mpunga kwa kufuata taratibu na sheria za bodi iliyokuwa inaongoza. Huu mradi uliwasaidia sana wenyewe na kujikwamua kutoka kwenye umaskini. Ndiyo maana nikasema wazo lako ni zuri sana na kwa kuanzia serikali ingeangalia ni mazao gani yanastawi katika kila sehemu halafu wapeleke utaalam kama walivyofanya wajapan.
Shukurani sana kwa wazo zuri
 
Katiba imara hutengeneza chumi zilizo imara na tamaduni yenye udemokrasia wenye kufuata sheria hujenga taifa imara.
Kwa tafsiri isiyo rasmi, mimi naiona katiba kama mpango ama mkataba ambao raia tumekubaliana kuutumia katika kuongoza na kuongozana baina yetu ili tuishi kwa amani, uhuru, haki, na umoja.

Utekelezaji hasi wa mpango huu uathiriwa na yale uliyoyataja ubinafsi, rushwa, na kadhalika. Kwa hiyo, kwa maoni yangu tuondoe vikwazo vya utekelezaji wa mpango/katiba baaada ya hapo tuone kama kweli katiba inashinda. Vinginevyo, tutabadili katiba chungu nzima bila kupata tunavyovihitaji ambavyo ni pamoja na haki, amani, umoja,uhuru, maendeleo ya kijamiii na kiuchumi na mengine kama hayo. Hatuna mfano mzuri ambao umeonyesha kuandika upya katiba ya nchi kumewezesha kupatikana haki, umoja,uhuru maendeleo katika nyanja zote kwa nchi yanazofanana nazo.

Nina simama kukosolewa.
 
Back
Top Bottom