Punguza ulaji wa nyama nyekundu kama vile nyama ya ng’ombe, mbuzi, kondoo na badala yake kula nyama ya kuku. Kula zaidi kuku wa kienyeji na wapike au wachome ili wasiwe na mafuta mengi. Kwa kuku wa kisasa hakikisha hauvunji na kutafuna mifupa yao maana mabaki mengi ya dawa huachwa huko, utakuwa unakula na dawa zilizotumika kuwakuzia na kuwatibia.
Sote tunakula mafuta. Na sote tupo katika hatari ya kupata au kuendelea kuwa na matatizo yanayosababishwa na mafuta mengi mwilini. Tunajua kwamba mafuta mengi ni mabaya mwilini na tunapenda kupunguza kula mafuta. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mafuta mengi huleta matatizo na kumuweka mtu katika hatari ya kuwa na unene na uzito mkubwa na uliopitiliza, kupata na shinikizo kubwa la damu, kupata kisukari, kupata magonjwa ya moyo na kadhalika. Yote hayo unaweza kuyaepuka au kusaidia kuyatibu kwa kupunguza mafuta mwilini.
Njia nzuri zaidi ya kudhibiti mafuta ni kujizuia usile mafuta mengi. Unaweza kufanya hivyo kwa
Kutumia maziwa yaliyopunguzwa au kuondolewa mafuta
Kutumia kiasi kidogo tu cha mafuta katika mapishi
Kuepuka kukaanga vyakula kwa mafuta, na badala yake kutumia njia zingine za kuandaa vyakula kama vile kuchemsha, kuchoma, kuoka, kupika kwa mvuke nk
Toa mafuta yanayoonekana kwenye vyakula na mboga
Punguza ulaji wa vyakula vilivyokaangwa kwa mafuta na vile vyenye mafuta mengi kama vile soseji, nyama ya kusaga, keki, vitumbua, chipsi, nyama za kukaanga nk
Kula zaidi kuku (Ondoa ngozi ya nje) na samaki
Kupunguza mafuta kutakusaidia kufanikisha mambo yafuatayo
Kukukinga dhidi ya hatari zinazoletwa na mrundikano wa mafuta mengi mwilini
Hatari za mrundikano wa mafuta mengi mwilini ni pamoja na kuganda kwenye mishipa ya damu na moyo na kupelekea kupungua kwa njia ya kupita damu na moyo kutumia nguvu nyingi sana kusukuma damu. Hatima yake ni magonjwa ya moyo, presha na magonjwa mengine ya mishipa ya damu.
Pia mafuta mengi humfanya mtu kuwa na uzito mkubwa na unene uliopitiliza, kuweza kupata magonjwa mbalimbali kama vile kisukari, shida katika upumuaji, mwili kuwa mvivu na kushindwa kufanya kazi vizuri, matatizo ya miguu na kadhalika