Ini ndiyo kiungo pekee cha mwili kinachoweza kujiunda upya. Kwa mfano, unaweza ukapoteza asilimia 50 ya ini lako na baada ya wiki mbili ukawa na ini jingine lililokamilika kabisa.
Ini ni kiungo muhimu kwa maeneo mengi ya siha. Chochote kinachoingia mwilini kabla ya kufika kwenye ngazi ya seli hupitia kwenye ini kwanza. Hii ina maana kuwa ini lako ndiyo ngome ya kwanza ya mwili wako dhidi ya sumu mbalimbali zinazoingia mwilini mwako kwa njia ya chakula au vinywaji.
Ini ni kiungo cha ajabu kabisa ambacho ni cha lazima kabisa kwa utendaji kazi wa mwili. Sehemu kubwa ya wataalamu bobezi wa kiungo hiki wanaamini kwamba ini lina zaidi ya majukumu 500 ndani ya mwili.
Ukiondoa jukumu la kuchuja sumu kutoka kwenye vitu mbalimbali tunavyokula na kunywa, kuwepo kwa ini pia ni lazima kwa sababu ya kuhifadhi viinilishe, kuondoa sumu kwenye uchafu unaozalishwa mwilini kutokana na majukumu mbalimbali ya viungo vya mwili.
Kazi nyingine ni kuratibu na kuhifadhi nishati mwilini, kuratibu utendaji kazi wa homoni, kusasambua (digest) mafuta yanayoingia mwilini kwa njia ya lishe, uundwaji wa protini ndani ya mwili, uundwaji wa lehemu (cholesterol) ndani ya mwili na kuratibu sukari ya damu.
Kazi ya kwanza na ya msingi ya ini ni kuchuja na kudhibiti sumu zinazoingia mwilini na zile zinazozalishwa ndani ya mwili. Bila kiungo hiki muhimu miili yetu itazidiwa na mzigo mkubwa wa sumu na itashindwa kuishi.
Ni kazi ya ini kupambana na kemikali mbalimbali kutoka kwenye mazingira zinazoingia mwilini kwa njia ya kula au kunywa. Ini linafanya kazi kama chujio ambalo huchuja damu inayozunguka mwilini.
Ni kazi ya ini kupambana na kemikali mbalimbali kutoka kwenye mazingira zinazoingia mwilini kwa njia ya kula au kunywa. Ini linafanya kazi kama chujio ambalo huchuja damu inayozunguka mwilini.
Chujio hili huondoa sumu zilizopo kwenye damu. Baadhi ya sumu hizi ni mabaki ya chembe nyekundu za damu zilizochakaa (Bilirubin) yaliyochakatuliwa kwenye wengu, kemikali ya ammonia kutoka kwenye protini zilizotumika mwilini, madawa mbalimbali, hasa yale ya kifamasia, pombe, sumu kutoka katika vyakula na vinywaji mbalimbali tunavyokula na kunywa.
Nyingine ni sumu kutoka matumboni; mathalan mabaki ya pembejeo za kilimo, viambata vilivyoongezwa kwenye chakula, na sumu zinazozalishwa na bakteria, fangasi na vimelea vingine vinavyoishi matumboni.
Magonjwa ya ini
Matatizo mbalimbali yanaweza yakalikabili ini na kulifanya lishindwe kufanya kazi inavyopasa, au lishindwe kabisa kufanya kazi.
Miongoni mwa matatizo haya ni pamoja na mwili kuzidiwa na mzigo mkubwa wa sumu mbambali.
Ini kujikuta likikabiliana na kemikali moja au zaidi ambazo ni sumu kali, kwa mara moja, au kwa vipindi tofauti, maambukizi ya vimelea mbalimbali vya maradhi. Kila moja kati ya matatizo haya, au yote kwa pamoja, huzaa magonjwa mbalimbali ya ini.
Dalili za magonjwa ya ini ni pamoja na maumivu, tumbo kujaa (bloating), ini kuongezeka ukubwa, mabadiliko katika haja kubwa na ngozi kugeuka kuwa rangi ya njano.
Hata hivyo, haina maana kuwa dalili hizi zinapokosekana, basi ini lako liko salama. Kipimo cha uhakika zaidi cha usalama wa ini lako ni upimaji wa kiwango cha vimeng’enya (enzymes) vinavyozalishwa na ini ndani ya damu. Kuwepo kwa vimeng’enya hivi ni kiashiria kuwa seli za ini zilizoharibiwa zinavuja kuingia katika mzunguko wa damu.
Kadri kiwango cha vimeng’enya hivi kinavyokuwa kikubwa ndiyo ukubwa wa uharibifu wa seli za ini unavyokua. Kuna vitu kadhaa vinavyoweza kusababisha kuongezeka kwa vimeng’anya vya ini kwenye damu, ikiwamo sumu na maambukizi ya vijidudu kwenye ini.
Sababu kuu inayochangia ini kushindwa kufanya kazi kutokana na sumu zinazotokana na matumizi ya dawa mbalimbali za kifamasia ni dawa inayoitwa Acetaminophen (Tylenol/Panadol).
Dawa hiyo siyo sumu. Inakuwa sumu kwa sababu ini linaibadilisha na kuwa kemikali ya aina nyingine inayoitwa napqi. Hivyo, husababisha kifo cha haraka kwa seli za ini.