Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Afya ya Kinywa Kwa Watu Wazima Chini Ya Miaka 45


Sasa uko kwenye kipindi kizuri na muhimu zaidi cha maisha yako katika kutumia muda wako mwingi kwa shughuli za kimaendeleo ni vizuri kuzingatia afya ya kinywa chako kwa faida ya afya ya mwili wako wote
 
Unaweza kufikiria kuwa kutoboka na kuoza meno ni suala la watoto tu, lakini je unajua kuwa hata wewe uko kwenye mazingira hatarishi maisha yako yote linapokuja suala la magonjwa ya kinywa na meno? Magonjwa ya meno yasipotiliwa maanani na kutibiwa huweza kupelekea matatizo makubwa zaidi kama vile maambukizi, madhara kwenye taya na hata mishipa ya fahamu kwa uchache. Wakati mwingine maambukizi yatokanayo na jino huweza kusambaa sehemu nyingine za mwili na hata kuhatarisha maisha
 
Magonjwa Ya Kinywa Na Meno Yanazuilika
Habari njema ni kwamba magonjwa ya kinywa yanazuilika tena kwa urahisi tu. Na unaweza kuzuia magonjwa ya kinywa na meno kwa kufanya tabia rafiki za afya ya kinywa na meno:
 
Mara zote Kumbuka kupiga mswaki mara mbili kwa siku
Fanya flosi mara moja kwa siku
Kula mlo kamili
Jizuie na milo isiyo na lazima kati ya mlo mmoja na mwingine
Usisahau kuwa na ratiba ya kumuona daktari wa meno mara kwa mara
Kwa kufuatisha tabia hizo rafiki na rahisi unaweza kupunguza uwezekano wa kupata magonjwa ya meno
 
Tabia Na Matendo Mazuri Kwa Afya ya Kinywa
Kupiga mswaki ndio msingi wa afya bora ya kinywa iliyo endelevu. Kutunza meno yako na fizi zako katika hali ya afya, hakikisha mara zote unapiga mswaki mara mbili kwa siku ukitumia dawa ya meno yenye madini ya floridi na mswaki ambao haukuumizi.
 
Ukubwa na umbile la mswaki wako ni lile ambalo litaruhusu mswaki wako kuweza kufika sehemu zote za kinywa kiurahisi. Halikadhalika, usisahau kubadilisha mswaki wako kila baada ya miezi mitatu ama minne au pungufu ya hapo mara tu uonapo kuwa visafishio (brashi) vyake vimehabika. Mara zote mswaki ambao visafishio vyake vimeharibika hauwezi kusafisha meno kwa ukamilifu.
 
Kufanya Flosi
Kufanya flosi inaendana pamoja na kupiga mswaki. Kwa kufanya flosi mara moja kwa siku itasaidia kusafisha vizuri kwenye sehemu finyu kati ya meno ambapo mswaki huwa hauwezi kufika. Ni muhimu sana kufanya flosi kwasababu mara inaposhindikana kusafisha sehemu hizo huweza kutengeneza ugaga (calcus). Ugaga ni utando mgumu sana ambao ili utolewe ni lazima uende kwa daktari wa kinywa na meno kwa ajili ya kusafisha meno yako
 
Matatizo Unayoweza Kuyapata Katika Umri Wako Huu
Ugonjwa wa Fizi
Huu ni ugonjwa unaohusisha fizi ambazo ndio zimeshikilia jino mahali baada ya mfupi ulio chini yake. Ugonjwa huu Unapozidi sana huweza kuathiri mfupi wa taya hali ambayo huweza kusababishwa jino au meno yalioathirika kung’oka. Ugonjwa huu husababishwa na uwepo wa utando mlaini (plaque) unaoundwa na bakteria katika sehemu ambazo meno yanakutana na ufizi.
 
Utando huu usipoondolewa kwa kupiga mswaki huweza kukomaa na kuwa mgumu uitwao ugaga (calculus) kiasi cha kushindwa kuondolewa na mswaki mpaka uende hospitali. Pindi ugaga unapojitengeneza huwa ni vigumu kusafisha kati ya meno. Kujijenga huku kwa utando mlaini (plaque) na kisha ugaga (calculus) ndio hupelekea ugonjwa wa fizi zitoazo damu wakati ama wa kupiga mswaki ama hata wakati unang’ata kitu kuacha alama ya damu.
 
Habari njema ni kwamba mwanzoni kabisa ugonjwa huu hutibika na kisha kabisa, lakini kadiri unavyochelewa kuripotiwa kwa daktari huwa ni vigumu kupona
Ugonjwa huu wa fizi wa zilizovimba na hatimaye kutoa damu usipotibiwa hupelekea ugonjwa mbaya unaohusisha mfupi wa taya linaloshikilia jino ama meno husika (Periodontitis)
 
Inawezekana mtu kuwa na Periodontitis pasi na kujijua kwani mara nyingi ugonjwa huu hauna alama za tahadhari (warning signs. Ndio maana kwenda kwa daktari wa kinywa na meno na kufanyiwa uchunguzi wa ugonjwa huu ni muhimu. Matibabu yake hutegemea ugonjwa wa muhusika ni umefikia kiwango gani. Kimsingi usafi wa kinywa unabakia kuwa ndio njia kuu ya kuzuia ugonjwa huu kukupata, kujirudiarudia ama kukupata na madhara makubwa zaidi
 
Kusaga Meno (Teeth Grinding)
Kusaga meno mara nyingi hutokea wakati ukiwa umelala na huwa muhusika hawezi kujua kama tabia hiyo. Hali hii huweza kuleta matatizo kwenye meno na taya. Ingawa hali hii mara nyingi husababishwa na msongo wa mawazo, pia magonjwa ya usingizi (Sleeping disorders) huweza kuwa sababu. Ni vizuri kumuona daktari wa meno ili kupata msaada zaidi.
 
Maungio Ya Taya (Temporomandibular Joint)
Maungio ya taya ni moja kati ya maungio yenye changamoto zaidi katika mwili wako. Tatizo lolote ambalo linaweza kupata maungio haya huweza kufanya yasifanye kazi vizuri. Mpaka sasa imekuwa ni vigumu sana kujua sababu hasa ya chanzo halisi cha magonjwa yanayoyapata maungio haya
 
Baadhi Ya Dalili Za Ugonjwa Wa Maungio Ya Taya:
Maumivu kwenye ama karibu na sikio
Maumivu kwenye taya
Sauti wakati wa kufungua kinywa
Maumuvu ya kichwa
Kama mara kwa mara una dalili hizo ni vizuri kumuona daktari wa kinywa na meno kwa uchunguzi zaidi.
 
Matibabu Ya Mzizi Wa Jino (Root Canals)
Wakati mwingine jino lako limetoboka kiasi kwamba ni vigumu kuliziba kwa matibabu ya kawaida, mpaka lifanyiwe matibabu ya mzizi wa jino. Matibabu haya hufanywa kwa meno ambayo yametoboka na tundu husika limefika mpaka kwenye sehemu za ndani kabisa ambazo ni laini na zina mishipa ya fahamu na damu
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…