Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

IMG-20180102-WA0484.jpg
 
Kuna ugonjwa wa moyo unaoitwa Atherosklerosisi (Atherosclerosis). Hali hii ni kitendo cha mafutamafuta kuganda kwenye mishipa ya ateri. Kuganda kwa mafutamafuta huko, kunaweza kuchukua miaka mingi. Kadri miaka inavyosonga mbele, ndivyo mafutamafuta haya yanazidi kuwa magumu na kuzuia msukumo wa damu yenye oksijeni kwenye moyo.
 
Ikiwa mafutamafuta yataziba kabisa kwenye ateri koronari na kusababisha misuli ya moyo kukosa damu yenye oksijeni, huweza kumsababishia mtu maradhi mengine yanayoitwa Anjina (Angina), kwa maana ya maumivu makali ya kifua na Mshtuko wa Moyo (Myocardia Infarction/Heart Attack).
 
Anyurismu (Aneurysm) ni aina nyingine ya magonjwa ya moyo. Hiki ni kitendo cha mishipa ya ateri kuvimba kama puto kutokana na kuharibika kwa mishipa au kudhoofika kwa kuta za mishipa. Ikitokea mishipa hii ya ateri ikapasuka, husababisha damu kuvuja kwenye ubongo,
 
hivyo kumsababishia mtu kukumbwa na Kiharusi (Stroke). Kiharusi ni ugonjwa wa kupooza unaotokana na kuingiliwa au kupungua kwa usambazaji wa damu kwenye ubongo hali inayosababisha seli za ubongo kukosa oksijeni na virutubishi.
 
Ugonjwa mwingine wa moyo hujulikana kwa jina la Rhumatiki ya Moyo (Rheumatic Heart Disease). Huu ni ugonjwa unasababisha kupungua utendaji kazi wa moyo kutokana na moyo kuwa na vivimbe tangu mtoto anapozaliwa (Congenital Heart Diseases), na mara nyingi huweza kusababisha vifo wakati wa utotoni.
 
Peripheral Vascular Disease ni ugonjwa mwingine wa moyo kwenye mishipa ya damu. Ugonjwa huu hutokea kwenye mfumo wa usambazaji wa damu nje ya ubongo na moyo. Mara nyingi, ugonjwa huu huwapata watu wenye umri wa kuanzia miaka 50 na kuendelea, hasa wavutaji wa sigara na wenye kisukari
 
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), magonjwa yasiyoambukiza kama yalivyo magonjwa ya moyo, kila mwaka huuwa watu milioni 38 duniani. Vifo vingi kati ya hivyo, hutokana na magonjwa ya moyo.
 
Inakadiriwa kwamba watu takriban milioni 17.5 hufariki dunia kila mwaka kwa magonjwa hayo ya moyo, ikifuatiwa na magonjwa ya Saratani yanayouwa watu takriban milioni 8.2 kwa mwaka, wakati magonjwa ya njia ya hewa yanauwa watu milioni nne na Kisukari watu milioni 1.5 kila mwaka.
 
Kwa upande wa Tanzania, takwimu kutoka Chama cha Madaktari wa Watoto nchini (PAT), zinaonyesha kwamba takriban watoto 13, 600 huzaliwa kila mwaka wakiwa na magonjwa aina mbalimbali ya moyo, huku watoto takriban 3, 400 kati yao, wakihitaji kupatiwa matibabu kwa kufanyiwa upasuaji.
 
Ni nini chanzo cha magonjwa ya moyo?

Kutozingatia kanuni za ulaji bora, ni moja ya mambo yanayoongeza uwezekano wa mtu kupata magonjwa ya moyo. Kwa mfano, ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi, vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi nyingi na lehemu nyingi, huku ulaji wa mbogamboga na matunda ukiwa ni wa kiwango cha chini, huongeza uwezekano wa kupatwa na magonjwa ya moyo.
 
Aidha, hali ya kuwa na uzito uliozidi kiasi au kuwa na unene uliopitiliza pamoja na kutofanya mazoezi ya mwili na viungo mara kwa mara, huchochea pia uwezekano wa magonjwa ya moyo.
 
Wakati mwingine magonjwa ya moyo huweza kutokana na historia ya ugonjwa huo katika familia. Umri unapozidi miaka 50 kuna uwezekano pia wa kupatwa na magonjwa haya ya moyo, huku wanaume wakiwa kwenye hatari zaidi ya kupatwa na tatizo hili mapema zaidi ikilinganishwa na wanawake.
 
Tafiti mbalimbali ambazo FikraPevu inazo zinaonyesha kuwa magonjwa ya moyo huanza kumwandama mtu pale mambo fulani yanaposababisha sehemu ya ndani ya kuta za mishipa ya damu kuharibiwa.
 
Back
Top Bottom