Kusaidia maskini ni kutoa sadaka na kwa wengine ni ibada. Hivyo si rahisi kwa mtu kufuatilia alichokitoa kinatumikaje au kinakwenda wapi kwa kuwa jukumu lake lilikuwa ni kutoa sadaka au kufanya ibada.
Lakini kwa sababu za kijamii, ni muhimu kuangalia kwa kina mfumo mzima wa watu wanaoomba mitaani, hasa wenye ulemavu unaowafanya wasiweze kabisa kujishughulisha na kazi za uzalishaji.
Umeshawahi kujiuliuliza wale ombaomba walemavu wanaotumia viti vya magurudumu wana uhusiano gani na vijana wanaowasukuma? Je, ni ndugu au vijana tu walioamua kuwasaidia?
Wengi hujiuliza, hawa wanaowasukuma ombaomba walemavu ni vijana wenye afya njema na nguvu. Kwa nini basi wasijihusishe na shughuli za uzalishaji au biashara ili wawasaidie hao ndugu zao badala ya kufanya kazi nzito ya kuwasukuma kutwa nzima na kutembea sehemu kubwa?