Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Kuna majina kibao ya makocha wanaohusishwa na kibarua hicho kuanzia Mauricio Pochettino, Zinedine Zidane, Antonio Conte, Laurent Blanc na wengine kibao, lakini yote kwa yote ni nani atakayekuja kuchukua mikoba hiyo?

Huko nyuma, Mourinho alishawahi kuzinoa timu kadhaa na kuondoka, lakini unafahamu ni kitu gani kilichokuja kutokea kwa makocha wote wa kudumu waliokuja kurithi timu za Mourinho. Cheki hapa kilichotokea kwa makocha hao waliomrithi Mourinho kwenye timu alizopita.
 
Victor Fernandez (Porto)

Baada ya Mourinho kuondoka Porto na kutimkia zake Chelsea mwaka 2004, klabu hiyo ya Ureno kwanza ilimchukua Luigi Delneri kuwa kocha wake mpya kabla ya kumfuta kazi siku chache tu na hivyo kumchukua Victor Fernandez kuwa kocha wake wa kudumu mwanzoni mwa msimu mpya. Lakini, kilichomkuta Mhispaniola huyo ni kwamba aliishia kuinoa FC Porto kwa miezi sita tu, akafutwa kazi baada ya kushindwa kufanya kile alichofanya Mourinho katika msimu wake wa mwisho klabuni hapo.
 
Kumbuka Mourinho aliondoka na kuiacha FC Porto ikiwa bingwa wa Ulaya na jambo hilo liliifanya timu hiyo kuwa mfupa mgumu kuutafuna kwa makocha waliokuja badala yake. Fernandez alifutwa kazi Januari 2005, huku FC Porto ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo baada ya kuchapwa 3-1 na Braga. Rekodi zake ni kwamba alicheza mechi 29, alishinda 12, sare 10 na vichapo saba.
 
Avram Grant (Chelsea)

Baada ya mafanikio ya miaka mitatu huko Chelsea, Mourinho alifutwa kazi Septemba 2007 baada ya kuanza hovyo kwenye msimu wake wa nne na nafasi yake ilikuja kuchukuliwa na Avram Grant, akiwa kocha wa kipindi cha mpito kwanza kabla ya kusaini mkataba wa miaka minne akiwa kocha wa kudumu, baada ya kuonyesha ubora wake kwa miezi mitatu tu. Hakika mashabiki wa Chelsea hawakumkubali kabisa Grant, ambao wengi walikuwa wameshazoea yale maneno ya shombo ya kocha wao aliyetangulia, Mourinho.
 
Grant alianza kwa kupoteza dhidi ya Manchester United, lakini baada ya hapo aliitengeneza Chelsea yake na kuwa moto na ilikuwa ikishindana kwenye mataji matatu kati ya manne yaliyokuwa yakishindaniwa kwa msimu huo. Kwa bahati mbaya Grant hakuwa na bahati ya mataji, kwani alifungwa kwenye fainali ya Kombe la Ligi na Tottenham Hotspur na fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akichapwa na Man United, huku kwenye Kombe la FA alitolewa kwenye hatua ya robo fainali na Barnsley.
 
Rafael Benitez (Inter Milan)

Mourinho alidumu kwa miaka miwili kwenye kikosi cha Inter Milan kutoka 2008 hadi 2010, akishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya na mataji mawili ya Serie A kabla ya kutimkia zake Real Madrid. Baada ya kuondoka kwenye kikosi hicho, Mourinho alikuja kurithiwa na adui yake mkubwa, Kocha Rafael Benitez, ambaye alikuwa ametoka zake Liverpool na Inter alikwenda kusaini mkataba wa miaka miwili.
 
Benitez alishinda taji lake la kwanza na Inter, Agosti 2010 baada ya kuichapa AS Roma kwenye Italian Super Cup na huo ulikuwa mwanzo mzuri kwa Mhispaniola huyo. Mechi ya kwanza kwenye Serie A ilikuwa sare dhidi ya Bologna, hivyo ilimfanya Benitez kusubiri hadi Septemba 11, 2010 kupata ushindi wake wa kwanza baada ya kuichapa Udinese uwanjani San Siro. Baadaye, Inter ikakumbana tu na vichapo kwenye Serie A na kujikuta ikishuka hadi nafasi ya sita huku akienda kuchapwa na Tottenham kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Desemba 23 mwaka huo huo, Benitez alifutwa kazi, akiwa na rekodi ya kucheza mechi 25, akishinda 12, sare sita na vichapo saba.
 
Carlo Ancelotti (Real Madrid)

Wakati Mourinho alipoondoka Real Madrid kwenda kujiunga tena na Chelsea, mabosi wa Los Blancos iliamua kumpa ajira Mtaliano, Carlo Ancelotti kuja kuinoa timu yao. Kocha Ancelotti baada ya kutua Bernabeu alishuhudia kuondoka kwa wachezaji wenye majina makubwa kama Mesut Ozil na Gonzalo Higuain, lakini akifanya usajili wa mastaa Isco na Gareth Bale kutua kwenye kikosi hicho. Ancelotti alikuja kubadili hadi mfumo wa kuichezaji, timu ikianza kutumia 4-3-3 na kufanikiwa kushinda taji la Copa del Rey ikiifunga Barcelona 3-1 kwenye fainali.
 
Mafanikio makubwa ya Ancelotti kwenye kikosi cha Madrid yalikuja kwenye msimu wa 2013/14, ambapo alishinda taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini mambo hayakuwa mazuri kwenye La Liga na baada ya kushindwa kubeba ubingwa, mabosi waliamua kumfuta kazi Ancelotti, Mei 2015, huku bosi Florentino Perez akisema ulikuwa uamuzi mgumu sana kuwahi kufanya wakati anamfuta kazi Mtaliano huyo.
 
Antonio Conte (Chelsea)

Licha ya kuipa Chelsea ubingwa wa Ligi Kuu England katika msimu wa 2014/15, Mourinho alikumbana na wakati mgumu msimu uliofuatia na Chelsea ilijikuta ikishuka hadi nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi na Desemba 2015 tu, akafutwa kazi huko Stamford Bridge.

Baada ya Guus Hiddink kuja kuwa kocha wa muda, Chelsea iliamua kumpa kazi Mtaliano, Antonio Conte kwenye majira ya kiangazi ya 2016, ambako kocha huyo alitoka kuiongoza Italia kufika robo fainali kwenye Euro 2016, ambapo walifungwa kwa penalti na Ujerumani.
 
Baada ya kuanza hovyo, akikumbana na vipigo viwili mfululizo kutoka kwa Liverpool na Arsenal, Conte alikitengeneza kikosi chake cha Chelsea na kuwa moto kabisa, akiwatumia Marcos Alonso na Victor Moses kuwa wing-backs huku akitumia mabeki wa kati watatu.

Chelsea ikashinda mechi 13 mfululizo na kikosi kikaa vyema, kikimaliza msimu huo kwa kubeba Ligi Kuu England, wakiweka rekodi ya kushinda mechi 30 katika msimu mmoja. Wangebeba Kombe la FA pia, lakini alichapwa na Arsenal kwenye mechi ya fainali.

Msimu uliofuatia mambo yalikuwa magumu kwa Conte na matokeo yake, akafutwa kazi na Chelsea baada ya timu hiyo kumaliza ligi ikiwa kwenye nafasi ya tano, licha ya kwamba ilishinda ubingwa wa Kombe la FA.

Kwa sasa Chelsea inanolewa na Mtaliano mwingine, Maurizio Sarri.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…