Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Mtu mwenye furaha ni yule ambaye kwake hakuna kitu kizuri wala kibaya, bali kuna fikra nzuri na mbaya. Hapa mtu haweki uzuri au ubaya kwenye kile kinachofanyika, bali uzuri au ubaya ni tafsiri ya fikra zake. Hivyo mtu anajijengea maadili mema ambayo yanamwezesha kutafsiri uzuri kwenye kila kinachotokea.
 
Maisha mazuri ni yale ambayo hayaathiriwi na raha wala maumivu. Watu wengi wanasukumwa na nguvu hizo mbili, wanafanya kitu ili kupata raha, au kuepuka maumivu. Lakini raha na maumivu huwa vinakwenda pamoja, kamwe haviachani. Hivyo chochote unachofanya ili kupata raha, baadaye kinazalisha maumivu. Hivyo furaha ya maisha haipaswi kutegemea kwenye kupata raha, kwa kuwa mwisho wa raha ni mwanzo wa maumivu.
 
Ili kuwa huru na kuwa na maisha yenye furaha, unapaswa kujitegemea wewe mwenyewe na kutokutegemea kitu chochote ambacho kipo nje yako. Unapaswa kutumia akili yako kufanya maamuzi na kupokea matokeo yake. Unapaswa kuweka kujiamini kwako kwenye kujifunza na kuendelea kujifunza ili kuwa na maarifa sahihi mara zote.
 
Kuwa na maisha yenye furaha ni kuchagua kuishi kwa msingi wa wema, kuwa na tabia njema kwako na kwa wengine. Kufanya yale ambayo ni sahihi mara zote na kuepuka kufanya vitu kwa kusukumwa na tamaa au kupata raha. Kufanya ubaya ni kwa tamaa ya kupata raha ni kuharibu maisha yako ya furaha.
 
Maisha ya furaha siyo kutokukosolewa na wengine, bali kupuuza wale wanaokukosoa, hasa pale wanapokuonesha kwamba unachofanya ni tofauti na unachosema. Pale watu wanapokuonesha kwamba unaishi kinyume na misingi unayoihubiri. Hilo lisikuondolee furaha ya maisha, kwa sababu unapojiwekea misingi ya maisha haimaanishi ndiyo umeshaweza kuifuata kwa asilimia mia moja, badala yake ni mwongozo wako, ambao kila wakati utajitahidi kuufuata na hata kujipima kwa mwongozo huo. Unapata furaha kila unapokaribia kuishi kulingana na msingi wako. Huku ukijua hujakamilika, hivyo kila siku ni nafasi ya wewe kuwa bora zaidi.
 
Maisha mazuri siyo kuwa na mali na utajiri, wengi hufikiri ukishakuwa na mali na utajiri basi utakuwa na maisha yenye furaha. Lakini wanachokuja kugundua ni kwamba kadiri wanavyopata mali zaidi ndivyo maisha yao yanakosa uhuru zaidi. Maisha yenye furaha ni yale ambayo hata kama una mali nyingi, kama zitapotea zote hautatetereka hata kidogo. Hapa unakuwa umezimiliki mali na siyo mali kukumiliki wewe. Wengi wanaopata mali wanakosa uhuru wa maisha kwa sababu wanahofia kupoteza hata kidogo, na hili linawafanya wawe na maisha yanayoonekana mazuri kwa nje, lakini kwa ndani hawapo huru.
 
Hakuna ubaya wowote kwa mwanafalsafa kuwa na utajiri, wala hakuna ubaya kwa mtu yeyote kuwa na utajiri, kama amepata utajiri huo kwa njia ambazo ni halali, kama hajamwibia yeyote na wala hajamuumiza yeyote kwenye kupata utajiri huo. Kwa kupata utajiri kwa njia sahihi ni kitu kizuri kwa wengine pia kwa sababu utajiri huo utawasaidia na pia wewe utakuwa hamasa kwao kupiga hatua pia.
 
Kipimo cha kujua kama utajiri umepatikana kwa njia sahihi ni pale mtu anapoweza kutangaza hadharani kama kuna yeyote ana kitu anachonidai au nimechukua kwake basi aje kukichukua sasa kutoka kwangu. Kama hakuna anayejitokeza basi utajiri huo umepatikana kwa njia sahihi. Lakini kama watakuja watu, wakiwa na ushahidi sahihi kwamba uliwachukulia vitu vyao kwa njia ambayo siyo sahihi, utajiri ulionao siyo wako, bali umeiba kwa wengine.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…