Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Kipimo cha kujua kama utajiri umepatikana kwa njia sahihi ni pale mtu anapoweza kutangaza hadharani kama kuna yeyote ana kitu anachonidai au nimechukua kwake basi aje kukichukua sasa kutoka kwangu. Kama hakuna anayejitokeza basi utajiri huo umepatikana kwa njia sahihi. Lakini kama watakuja watu, wakiwa na ushahidi sahihi kwamba uliwachukulia vitu vyao kwa njia ambayo siyo sahihi, utajiri ulionao siyo wako, bali umeiba kwa wengine.
 
Tofauti ya utajiri kwa mwanafalsafa na kwa mtu wa kawaida ni hii; mwanafalsafa anamiliki utajiri na kuutumia kwa njia sahihi, na unapoondoka, hakuna kinachobadilika kwenye maisha yake. Lakini kwa watu wa kawaida, wanamilikiwa na utajiri, utajiri unawatumia kufanya yale ambayo siyo sahihi na wanapopoteza utajiri huo maisha yanavurugika sana, wengine wanakuwa tayari hata kukatisha maisha yao. Kwa mwanafalsafa utajiri ni kitu ambacho ni kizuri kuwa nacho, lakini hata kisipokuwepo maisha yanaendelea, kwa mtu wa kawaida utajiri ndiyo maisha yenyewe, na usipokuwepo basi hakuna maisha.
 
Usipoteze muda wako kwenye kuhukumu wengine, hasa kwenye kutafuta makosa kwenye maisha yao, badala yake angalia kipi kizuri ambacho mtu anafanya na unaweza kujifunza kwake. Kwenye maisha watu wengi wamekuwa wanapenda kuangalia makosa ya wengine ili kujidhibitishia kwamba licha ya watu hao kupiga hatua, wana mapungufu makubwa, lakini hilo halitakuwa na msaada kwako. Kila aliyepiga hatua kuna vitu vizuri anavyofanya, ambavyo unaweza kujifunza na wewe ukawa bora sana. Jifunze mazuri ya wengine na yatumie kupiga hatua zaidi.
 
Maisha yenye furaha ni maisha yenye maandalizi wakati wote, wanajeshi huwa wanafanya maandalizi ya vita wakati ambapo kuna amani. Hivyo na wewe unapaswa kufanya maandalizi ya hali ngumu wakati ambapo una hali nzuri. Mfano licha ya kuwa na mali na kuweza kupata chochote unachotaka, mara kwa mara ishi kama mtu asiyeweza kupata kile anachotaka. Licha ya kuwa na kitanda kizuri, mara kwa mara unaweza kuchagua kulala chini. Licha ya kuwa na gari binafsi, mara kwa mara unaweza kuchagua kutumia usafiri wa uma au hata kutembea kwa miguu kama wasioweza kumudu hata usafiri wa uma. Kufanya mazoezi ya aina hii siyo tu utakuweka imara pale unapopoteza unachomiliki, bali pia itakufanya uthamini zaidi kile unachomiliki. Unaweza kuwa umeshazoea sana kitanda chako, lakini siku moja ukilala chini, siku unapolala tena kwenye kitanda chako utashukuru mno.
 
Maisha ya furaha ni matokeo ya mtu kuyaelewa maisha yako na kuishi kwa asili yake, kujijua wewe mwenyewe kwa uwezo ulionao na kujua wapi unataka kufika, kisha kukaa kwenye njia sahihi ya kufika unakotaka kufika. Baada ya kuwa kwenye njia sahihi, unachopaswa kuweka ni juhudi na kujifunza kwa waliokutangulia, huku ukiutumia utajiri na siyo utajiri kukutumia. Na kutokupoteza muda wako kuhukumu maisha ya wengine, badala yake kujifunza kutoka kwenye mazuri ya wengine. Na kwa kila unachopata kwenye maisha, kujua unaweza kukipoteza wakati wowote na hivyo kutokung’ang’ana na chochote. Hivi ndivyo unavyoweza kuwa na maisha yenye furaha, kitu ambacho kinawezekana kwa kila mmoja wetu. Chagua leo kuishi maisha ya furaha.
 
Ubarikiwe mpenzi
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…