Nikijuwa kwamba kwa vile alikuwa mpinzani kutoka Libya lazima alikuwa anachukua hadhari yasije yakamfika yaliyowafika wapinzani wengine wa kiongozi wa Libya, Muammar Qadhafi. Nikikumbuka ya alasiri ya Ijumaa ya Aprili 11, 1980, pale Yusuf Hassan, mtangazaji wa BBC, ambaye kwa sasa ni mbunge wa Kamukunji, Nairobi, Kenya, aliponipigia simu ofisini mwangu na kunipa pole.
Siku hizo nilikuwa mhariri wa Afrika na Mashariki ya Kati kwenye jarida la Index on Censorship. Nilimuuliza Yusuf pole za nini? Akanijibu: “Kwani hujasikia? Rafiki yako Ramadan amepigwa risasi punde hivi msikitini na amekufa.”