Kwenye maisha kuna nyakati huwa zinatufikia ambazo zinakuwa ni kipimo ambacho kinaonyesha ukweli wa makusudi yetu kwa yale tuliyokuwa tunataka au tayari tunafanya. Unaweza kukutana na changamoto kubwa kiasi kwamba ukafikia hatua za kusema kama hali ni hii basi sifanyi tena hiki kitu.
Lakini ukweli unabaki pale pale kwanini uliamua kufanya? Kabla hujakata tamaa ni vyema ukaanza tena kujiuliza ni kitu gani hasa kilikusuma wewe kuamua kuanza hiyo biashara? Hicho kipaji chako? Hilo kusudi lako?
Kuna nyakati utakuja kugundua hata wale watu wako wa karibu sana hawaamini hata kidogo kwenye ndoto zako tena wanakusema kwa pembeni huyu jamaa na ndoto zake.
Kwenye chochote kile ambacho unakitegemea katika kukuletea pesa iwe ni biashara au ajira ni vyema kujiuliza swali hili kwamba, kutokana na mabadiliko yanayokuja kila wakati hasa ya kiteknolojia je nitabaki salama kwa muda gani?
Kama ni biashara basi angalia jinsi unavyoiendesha biashara yako sasa hivi na namna ambavyo mambo yanabadilika je unabadilika au unaendelea kutumia mifumo ya zamani?
Unatakiwa ujue kwamba kila siku kuna binadamu wanawaza namna gani wanaweza kuyafanya maisha yawe marahisi kwa kurahisisha upatikanaji wa vitu na huduma mbalimbali. Mojawapo ya vitu vinavyoangaliwa ni biashara yako pia.
Ni vyema ukajitengenezea tabia au mfumo wa kutotegemea aina moja ya uendeshaji ili usije kuanguka kibiashara. Kwasababu mabadiliko yakija hayakuhurumia kama ulijiandaa au hukujiandaa. Kama utatokea mfumo rahisi wa wateja wako kupata huduma au bidhaa unayoiuza halafu wewe pekee ukawa ndio hauna huo mfumo ujue unaweza kuangushwa kibiashara.
Lazima uangali mbele uone ni mabadiliko gani yanakuja na yanawezaje kuathiri kile unachokifanya. Ukiweza kutazama mbele vizuri unaweza kuwa na maandalizi ili lolote linaweza kutokea likuletee athari chanya kwenye biashara yako.
Ni hatari sana kubaki kwenye mfumo wa zamani huku ukidharau mabadiliko madogo madogo yanayokuja. Ni sawa na wale ambao walibaki na farasi zao wakadharau waliokuwa wanatengeneza magari mwisho wa siku unabaki na farasi wako wengi na hakuna wa kumuuzia maana wote wanataka magari.