Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

ZHOU ENLAI: MWANADIPLOMASIA MASHUHURI ALIYEMALIZA UHASAMA KATI YA CHINA NA MATAIFA YA ULAYA MAGHARIBI NA KUJENGA MSINGI WA USHIRIKIANO KATI YA CHINA NA MATAIFA YA AFRIKA.

Thursday, September 27, 2018: 06:00AM

Na Masudi Rugombana

“Kwa hakika huyu ni mtu mwenye ubongo bora kuliko watu wote niliowahi kukutana nao katika nyanja ya siasa za kimataifa” Maneno haya aliyatamka Dag Hammarskjöld wakati huo akihudumu katika nafasi ya ukatibu mkuu wa umoja wa mataifa alipokuwa akimzungumzia Zhou Enlai, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa China chini ya Utawala wa Mao Zedong (Mao Tse Tung)
 
Zhou Enlai (tamka Chou En-lai) anatajwa kuwa miongoni mwa wanadiplomasia mashuhuri kabisa kuwahi kutokea nchini China na barani Asia. Alihudumu katika cheo cha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya watu wa china kuanzia Octoba 1949 hadi Januari 1976 na wakati huo huo akitumikia cheo cha Waziri wa mambo ya nchi za nje wa China kati ya mwaka 1949 hadi mwaka 1958.
 
Anaheshimika zaidi nchini mwake kuwa ndiye Muasisi wa diplomasia ya China na Mhamasishaji mkubwa wa amani Duniani. Yeye pamoja na Mao ndio waliosisi na kutekeleza kwa ufanisi mkubwa sera huru ya mambo ya nchi za nje ya China. Ndiye mwanadiplomasia aliyefanya juhudi kubwa za kuondoa uhasama uliokuwepo baina ya Jamhuri ya watu wa China na Mataifa ya Ulaya Magharibi, uhasama uliotokana na vita ya Korea.
 
Ni matokeo ya mkutano huo ndio yaliyoanzisha uhusiano wa kibiashara kati ya Marekani na China ambapo Marekani iliruhusu meli zake kufanya biashara na China huku zikipeperusha bendera za nchi nyingine (under foreign flags) na kuruhusu China kuuza bidhaa zake nchini Marekani kwa mara ya kwanza tokea kumalizika wa vita vya Korea.
 
Juhudi za Mwanadiplomasia Zhou Enlai zilipelekea uhusiano wa kidiplomasia kati ya China na Marekani kuimarika zaidi baada ya kufanikisha ziara ya kihistoria ya rais Richard Nixon mnamo mwaka 1972. Na hatimaye Marekani kutangaza rasmi kuitambua Jamhuri ya Watu wa China kwa kuvunja uhusiano wa moja kwa moja wa kidiplomasia na Kisiwa cha Taiwan mwaka 1979.
 
Pia umahiri wake katika masuala ya diplomasia ndio uliofanikisha kurejesha kiti cha Jamhuri ya Watu wa China katika umoja wa Mataifa mnamo October 25 mwaka 1971, awali ya hapo, Taiwan ndiyo ilikuwa ikitambuliwa rasmi kama Mwakilishi halali wa wananchi wa China katika umoja wa Mataifa.
 
USHIRIKIANO BAINA YA CHINA NA MATAIFA YA AFRIKA.

Ni Zhou Enlai ndiye aliyeasisi Ushirikiano baina ya China na Afrika. Ni baada ya kuhudhuria mkutano wa Bandung ( Bandung Conference), mkutano wa Kwanza mkubwa baina ya Nchi za Afrika na bara la Asia ulifanyika huko nchini Indonesia mwaka 1955 uliohudhuriwa na mataifa 29, sita kutoka Afrika ambayo ni Ethiopia, Misri, Libya, Sudan, Liberia na Guinea.
 
Mkutano huo ulikusudiwa kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya nchi za Asia na Afrika, pia kupinga ukoloni na ukoloni mamboleo. Mkutano wa Bandung ulikuwa ni mojawapo katika hatua muhimu kuelekea kuanzishwa kwa Umoja wa nchi zisizofungamana na upande wowote ( The Non-Aligned Movement ).
 
Ni katika mkutano huo ndipo Zhou Enlai alipofanya majadiliano ya kwanza na nchi za Kiafrika yaliyopelekea kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya China na nchi za kiafrika. Na mwaka ulifuata (Mwezi May, 1956) Misri ikawa taifa la kwanza barani Afrika kuanzisha uhusiano wa kidiplomasia na China. Hadi kufikia mwanzoni mwa miaka ya 1960 nchi kumi za Afrika ikiwa ni pamoja na Morocco, Algeria na Sudan zilikuwa tayari zimeshaanzisha uhusiano wa kidiplomasia na China.
 
Uhusiano baina ya China na Afrika uliimarika zaidi baada ya Ziara ndefu ya siku 51 ya Waziri Mkuu wa China Zhou Enlai kwenye mataifa kumi ya Afrika kati ya December 14, 1963 hadi February 04, 1964, akiweka historia ya kuwa kiongozi wa kwanza wa ngazi ya juu katika Serikali ya China kuzuru bara la Afrika akitembelea mataifa ya Misri, Somalia, Tunisia, Ethiopia, Algeria, Morocco, Ghana, Mali, Guinea na Sudan.

Ziara hiyo inaelezwa kuwa ndio ziara ndefu kuliko zote kuwahi kufanywa na kiongozi wa China barani Afrika.
 
ZHOU ENLAI AITEMBELEA TANZANIA.

Tanganyika ilikuwa ni miongoni mwa nchi alizopanga kutembelea, lakini ziara yake iliahirishwa kutokana na kuingiliana na tukio la kihistoria la mapinduzi ya Zanzibar. Hata hivyo Zhou Enlai alifanya ziara ya kiserikali nchini Tanzania mnamo June 4, 1965 kwa Mwaliko wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hayati Julius Nyerere. Ziara ambayo ilifungua ushirikiano wa kidiplomasia, kisiasa na kiuchumi baina ya China na Tanzania.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…