Endapo mafuta hayo yataongezeka zaidi huathiri mfumo wa damu kwa kuziba mishipa hivyo kuinyima nafasi ya kutosha kupita na kusababisha shinikizo la damu,” anasema.
Anaeleza kuwa ili kuepukana na matatizo hayo ni vema mtu akafanya mazoezi kila wakati ili kujiweka sawa na kupunguza mafuta mwilini. Mazoezi hayo yanaweza kuwa ni kukimbia, kukata tumbo na mengine ambayo husaidia kupunguza mwili.
Mbali na mazoezi ameshauri kuwa makini na matumizi au ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi kama nyama na kupendekeza matumizi ya mafuta ya mimea.
Daktari mwingine, Eliza Wampembe wa Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili (Muhas) anasema mbali na sababu hizo, kisukari kinaweza kurithiwa kutoka kwa wazazi au wanafamilia wengine ambao walikuwa na ugonjwa huo ndani ya ukoo.
Dk Eliza anabainisha kuwa mgonjwa wa moyo na kisukari yupo hatarini kuathirika na maambukizi mengine kwani huathiri figo na kongosho, hivyo kupunguza kinga za mwili.
“Miongoni mwa athari za kisukari ni miguu kuwa na vidonda visivyopona kwa urahisi kiasi cha kukatwa kwa baadhi ya wagonjwana kusababisha ulemavu ambao hawakuzaliwa nao,” anasema.
Pia, shinikizo la damu husababisha matatizo ya figo, macho, kiharusi, misuli ya tumbo na kutosikia vizuri.
Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2015 ya Shirikisho la Kisukari (IDF) Afrika, zaidi ya watu milioni 14 barani humo wana ugonjwa huo na idadi inaweza kuongezeka hadi kufikia milioni 34 mwaka 2040 endapo jitihada za dhati za kukabiliana nao hazitachukuliwa.
Ripoti hiyo inasema asilimia 66.7 ya watu wote barani Afrika wana kisukari, kati yao asilimia 79 ni wenye umri zaidi ya miaka 60.