Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Hakika nilisangazwa na masuali hayo kwani licha mimi kuwemo na kutokuwemo katika chama hicho, bali hata kupata kukisikia sijapata kukisikia maisha yangu. Nilimjibu kuwa, "Mimi sikijui, wala hao wakubwa wa chama hicho ikiwa wapo, mimi siwajui". Kiasi ya kumwambia hayo tu, nilimuona Mandera amebadilika sura yake na alianza kutumia lugha za ukali na matusi na mwisho aliniambia, "Ikiwa unataka kutuonesha uhodari kwa kukataa kusema kweli, basi na sisi tutakuonesha nini tutakufanya sasa hivi. Utatuambia ukweli au vipi?" Nilimwambia, "Ikiwa unautaka ukweli, huo niliyo kwambia ndio ukweli wala sina ukweli zaidi kuliko huo", "yote haya uyasemayo miye sijui lolote juu yake"
 
Allah Akbar! Alinipiga kibao cha ghafla, kilinitupa mpaka chini. Hapo, aliamrisha nilazwe juu ya meza, sikuwahi hata kupepesa, nilijisitukia nimesha bwagwa juu ya meza kama gunia la chumvi na nimelazwa kifudifudi. Naam, Mandera hakupoteza wakati, alianza kunicharaza kwa fimbo za mipera na huku akinitukana kwa matusi mabaya mabaya. Nilikuwa siwezi hata kufurukuta kwani hao wasaidizi wake walinidhibiti mikono na miguu, mradi nilikuwa taaban! Tokea nilikuwa nikihisi maumivu ya kupigwa mpaka mwili ulikufa ganzi nikawa sihisi chochote. Tokea nikiweza kupiga makelele na kuyayatika mpaka nilikuwa siwezi hata kuguna. Alipochoka mwenyewe, ndipo na mimi nilipopata afuweni.
 
Lakini, wakati huo nilikuwa chordo! Chumba chote nikikiona kinazunguka na watu nikiwaona wanazunguka. Niliachwa katika hali hiyo kiasi cha muda mdogo, kisha Mandera aliniambia niinuke kwenye meza nikae katika kiti. Nilipojaribu kujizowazowa, miguu ilishindwa kukanyaga chini kwani bakora zilifika mpaka nyayoni na pia miguu ilikuwa ikinitetemeka. Nilikamatwa huku na huku na kuwekwa juu ya kiti. Mandera aliniuliza, "Umefunga wewe leo?" (kwani siku hiyo ilikuwa Ramadhani ya kumi na tano) Nilimjibu, "Naam, nimefunga!" Aliniambia, " Basi leo, utafuturu mikwaju". Wakati huo roho ilikuwa kavu, mate yamenikauka, jasho likinitoka kila sehemu ya mwili.
 
Matako yametutumka na 47 kupasuka pasuka. Kiti kilikuwa hakikaliki kwani kilikuwa kikinitonesha. Kwa hakika, nilikuwa katika hali mbaya sana. Baada ya Mandera kupumua kidogo, alirejea tena kuniuliza masuali yake yale yale aliyoniuliza mara ya mwanzo. Na mimi, nilimjibu kama nilivyomjibu mwanzo. Hapo, Mandera aliamrisha nitiwe ile kamba ya kitanzi na nikatiwa nayo shingoni. Baada ya kutiwa, ilichukuliwa ncha moja ikapitishwa dirishani. Dirisha hilo lilikuwa juu sana hata huyo aliyekuwa akipenyeza hiyo kamba ilimbidi apande juu ya meza kuitupia.
 
Wakati huo mimi nilikuwa nimekaa juu ya kiti na shingoni mwangu nimevalishwa hicho kitanzi cha kamba ya kitani. Wote walitoka nje, isipokuwa Mandera tu alibakia pamoja na mimi na kitanzi changu shingoni mwangu. Utafikiri n'gombe mkali wa kuchezwa. Wale waliyokuwa wametoka nje, kazi yao ilikuwa kuivuta ile kamba mfano wa mtu anapovuta ndoo ya maji kutoka kisimani kwa kutumia roda. Nilianza kunyanyuka, si kwa khiyari, bali kwa kule kuvutwa mpaka nilikiwacha kiti ikawa nafuata kule ninako vutwa.
 
Mandera kazi yake ilikuwa ni kuamrisha, "Vuta! Wacha!" Akisema vuta, huvutwa na akisema wacha huachiliwa. Na ilipokuwa ikiachiwa, nilikuwa nikishindwa kujizuwia kwahivyo nikianguka kama nanga ibwatikavyo baharini. Mandera alikuwa akinipiga kwa fimbo za mipera na huku akiniambia, "Simama!". Mradi kazi ilikuwa kama hivyo, mpaka walipotaka wenyewe, waliniachia na walinitoa hicho kitanzi. Mandera alitoka nje ya hicho chumba na aliniacha mimi na hao wasaidizi wake
 
Juma Musa aliniambia, "Sikiliza Aman! Wacha ushupavu wako utakuja kujidhuru mwenyewe. Hapa ni pahala pabaya sana. Matokeo ya gereza hili hutoyaweza wewe, kwani ni ya khatari sana na mwisho ni kuuliwa. Basi mimi nakuomba useme kweli wa hicho chama chenu upate kujinusuru na mateso". Mimi nilinyamaza kimya sikumjibu chochote, kwani nilielewa kuwa anatumia lugha alizofundishwa katika kazi yake hii. Juma Musa alipoona hakupata chochote kwangu, na yeye alitoka katika hicho chumba na kuniacha mimi na hao wasaidizi wao wengine.
 
Baada ya muda, Mandera na Juma Musa walirejea katika chumba, Mandera aliwauliza hao watu wake kama nimesema chochote na Juma Musa alimwambia Mandera kuwa, "Anajifanya hodari, hataki kutwambia ukweli. Mimi nimejaribu kumnasihi, hata hakuonesha kuwa ananibali kitu". Mandera alisema, "Kwa nini hatumuuwi, kwani patakuwa kitu gani tukimuuwa? Lete ile bastola!" Kijana mmoja katika wasaidizi wake akiitwa Mzee, aliruka kuileta hiyo bastola. Mandera aliniambia, "Unaiona hii bastola, basi towa shahada kabisa. Leo utafuturu kaburini". Aliamrisha nifungwe kitambaa cha uso. Makame Fidia ndiye aliyenifunga hicho kitambaa. Nilitoa shahada. Hapo sikuweza kujuwa yalipitishwa mazingaombwe gani kwani nilisikia mlio mkubwa wa risasi lakini haikunigusa wala haikuniuwa, lakini kwa khofu nilizokuwa nazo, nilianguka mpaka chini.
 
Nilipoanguka, niliwasikia wakicheka kwa tafrija na istihizai, na huku Mandera akisema, "Nyoo! Si unajitia uhodari wewe, mbona unaogopa kufa. Hii ya leo ni trai tu mchezo bado". Mandera aliamrisha nifunguliwe hicho kitambaa cha uso na baada ya kufunguliwa, aliniambia, "Leo tutakuachia ukapumzike na ukazidi kufikiri mpaka kesho. Utakapoletwa hapa uweumesha kata shauri juu ya kusema kweli au kuendelea na kuuficha ukweli. Lakini, nakwambia kuwa kesho ukitufanyia mchezo kama huu uliyoufanya leo, basi tutaanza kwa kukutoa kucha za vidole vya mikono, kisha tukutowe na vya miguu, na tutakupaka hina ya pili pili hoho. Sasa mrejesheni kwa wenzake. Wakati huo kin'gora cha saa nane unusu cha kutoka watu makazini kilikuwa kikilia. Mchezo ulianza tokea saa mbili za asubuhi mpaka wakati huo wa saa nane unusu ndipo ulipomalizika. Nilikuwa katika hali mbaya sana hata nilishindwa kwenda bila ya kusaidiwa kwa kukamatwa mkono utadhani mtoto mdogo anafundishwa kwenda tata.
 
Nilipofika katika chumba wenzangu waliponiona hali hiyo niliyokuwa wakati huo, jambo la mwanzo, walininasihi nisiendelee na saumu, na mimi nilihisi hivyo hivyo, kwani roho yangu ilikuwa kavu, midomo mikavu hata mate yalinikauka. Hapakuwepo na cha kukila kwa wakati huo, isipokuwa maji na hata kingekuwepo, basi nisingeweza kukila. Hayo maji nayo yalikuwa yakipita kwa shida. Mwili wangu ulikuwa umejaa mitutumko tutumko, na mipasuko pasuko ya bakora za Mandera hata nilikuwa na taabu kwa muda wa siku kadhaa kuweza kulala; bali hata kukaa kitako ilikuwa taabu.
 
Ilipofika laasiri, nilipata homa kubwa sana na wenzangu walijaribu kuwaita wachungaji wa gereza hilo kwa kuwagongea mlango ili wapate kuniombea dawa. Hapana aliyekuja. Kwa bahati Mzee Kenyatta alikuwa na akiba ya vidonge vya aspirin, aliweza kunigaia vidonge viwili, si haba viliweza kidogo kunisaidia. Usiku kucha nilikesha kwa maumivu niliyokuwa nayo na kwa khofu nilizokuwa nazo kwa kufikiria hayo yaliyokuwa yakiningojea patapo kucha. Mandera nilikuwa nikimuona amenisimamia machoni mwangu
 
Mkuu hii ni story ya kweli?.
 
Tulikaa katika gereza hilo la "Kwa Ba Mkwe" tokea Disemba 1968 mpaka taarikhi 3 Mei, 1969 tulipotolewa na kupelekwa katika Makao Makuu ya Magereza. Kupelekwa kwetu huko kulikuwa kwa ajili ya kufungwa gerezani. Tulipofika 'kotagadi', ilikuwa kiasi cha saa 11 za jioni. Kila mmoja alipewa viroba vyake, na shuka moja, na kirago cha kulalia pamoja na kopo la kunywiya maji. Tulizivua nguo zetu na tulivivaa viroba vya kifungwa. (Viroba ni shati lisilokuwa na ukosi na suruali kipande, kaputura). Tulipoona tumepewa viroba vya wafungwa, kila mmoja alipigwa na msangao na machozi yalikuwa ya kimlengalenga
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…