Wakati alipofika mkutano ulikuwa umeshaanza. Alipotaka kukaa, Twala amesema, Mzee Karume alimwambia Saleh, "
Kwanza usikae mpaka utwambie kwanini ukachelewa kuja katika mkutano mpaka wakati huu?"
Saleh alimjibu kuwa, "Nimetokewa na udhuru wa kumpeleka mke wangu hospitali".
Karume, alimwambia, "Kwani huna dereva wa kumpeleka? Lazima umpeleke weye?"
Saleh, alimjibu, "Kutokana na hali yake ilivyo, nimeona lazima na mimi niwepo kwa Daktari, ili nipate kuzungumza naye zaidi".
Karume alimwambia Saleh, "Kwani amepata maradhi gani, au maradhi ya Kaswende?" 'syphilis'.
Saleh Saadalla, alimwambia Karume, "Sasa Mzee tunatukanana? Ikiwa na mimi nitakwambia wewe lugha kama hiyo, utapendezewa? Huyo ni mke wangu".
Karume kwa kuambiwa maneno kama hayo, hakuweza kuchukua, alipandwa na hamaki na alichukua fimbo yake na kutaka kumpiga Saleh Saadalla.
Saleh alipoona yamejiri ya kutaka kupigwa, alichomoa akiba yake kibindoni,bastola lakini kwa bahati mbaya au nzuri, haikuwa na zana zake kwa hivyo, ilitishia tu, haikuweza kufanya kazi yake.