Vyakula au viungo vya chakula vyenye uchachu: Kinyume na dhana iliyozoeleka miongoni mwa watu wengi, baadhi ya vyakula vyenye uchachu na upilipili kama vile pilipili, ndimu, limao na masala havina uhusiano na uwezekano wa kupata vidonda vya tumbo.
Watu walio katika kundi la damu la O: Imeonekana pia kwamba kundi la damu lijulikanalo kama blood group O, halina uhusiano wa kusababisha vidonda vya tumbo.
Unywaji wa pombe: Unywaji wa pombe pekee hausababishi vidonda vya tumbo. Hata hivyo, unywaji wa pombe sambamba na maambukizi ya vimelea vya Helicobacter pylori huongeza madhara ya ugonjwa wa vidonda vya tumbo.
Vitu vingine: Vitu vinavyohusishwa na uongezaji wa madhara ya vidonda vya tumbo ni pamoja na upasuaji wa tumbo (major abdominal surgeries), kuungua kwa moto (burns), ugonjwa wa figo; na kubadilishwa kwa viungo vya mwili kama figo au ini.
Mtu mwenye vidonda kwenye tumbo (gastric ulcers) hupata maumivu makali sana kipindi anapokula au mara tu baada ya kumaliza kula wakati aliye na vidonda kwenye sehemu ya kwanza ya utumbo mdogo (duodenal ulcers) hupata maumivu makali anapokuwa na njaa na hupata nafuu pindi anapokula.
Kupata haja kubwa cha rangi nyeusi au kahawia chenye harufu mbaya sana. Hii humaanisha mgonjwa anapata haja kubwa au choo kilichochanganyika na damu kwa mbali
Uwepo wa dalili kama kiungulia cha muda mrefu, kucheua na kutapika baada ya kula na historia ya kutumia dawa za kupunguza maumivu (NSAIDs) kwa muda muda mrefu bila kufuata ushauri wa daktari ni ishara tosha ya kumfanya mgonjwa kumuona daktari kumpima na kumfanyia uchunguzi ili kujiridhisha kuwa hana tatizo la vidonda vya tumbo.
1. Vipimo vya kuangalia ndani ya utumbo ambavyo ni pamoja na
Kipimo cha oesophagogastroduodenoscopy (EGD) au Upper GI endoscopy au gastroscopy. Kwa kutumia kipimo hiki, daktari huangalia moja kwa moja ndani ya utumbo wa mgonjwa kuona sehemu iliyo na vidonda pamoja na ukubwa wa tatizo lake. Aidha vipimo hivi humuwezesha daktari kuchukua sehemu ya utumbo iliyoathiriwa kwa ajili ya kuchunguza zaidi maabara ili kutambua uwepo wa vidonda au tatizo jingine linalomsumbua mgonjwa tofauti na vidonda vya tumbo.
Kipimo kinachoitwa Rapid Urease Test ambacho hufanywa kwa kutumia kinyama kilichochukuliwa kutoka kwenye utumbo wakati wa kufanya OGD. Kipimo hiki huangalia tabia ya vimelea hawa wa H. pylori.