Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Kuwekwa gerezani kwa wanawake hawa, ambao ni wazi kabisa hawakuwa na uhusiano wowote na mauaji, kulionyeha kwa mara nyengine tena chuki ya serikali ya Zanzibar dhidi ya wanawake wa Kiarabu na chuki yake dhidi ya Waarabu. Ukiukwaji huu wa wazi na wa kikatili wa haki za binadamu ambao wanawake kama Fatma Hilal na Fathiya Humud walihukumiwa kwasababu ya vitendo vya waume wao (Fathiya aliwekwa gerezani hali akiwa ana mimba na mumewe amefariki) uliachiwa upite hivi hivi bila ya hata neno moja la kukaripia kutoka kwa Nyerere.
 
Maelezo yake ya mwaka 1969 (aliyoyatoa alipozungumzia vita vya Biafra) kuwa ‘kama hatukujifunza kuikosoa dhuluma ndani ya bara letu, tutajikuta tunauvumilia ufashisti katika Afrika, ilimradi tu unafanywa na serikali za Afrika dhidi ya wananchi wa Afrika’ (Pomerance, 1982) yalidhihirisha ya kuwa ni zoezi la kujibeza mwenyewe.

Lilikuwepo jaribio la kulifanya zoezi hili la ukamataji kuwa ni siri kwasababu pale alipoulizwa na waandishi wa magazeti kutoka nchi za nje, waziri wa mambo ya ndani aliyefanya ukamataji huo alikataa katakata kuwa Babu alikamatwa (Babu, 1975: 2). Ni wazi kuwa Nyerere aliona aibu, lakini kama ilivyokuwa kila mara, hakufanya lolote na kutochukua hatua kwake kulimfanya awe mshiriki wa kikamilifu katika ukatili huu.
 
Mke wa Babu, Ashura na watoto wao waliruhusiwa kumtembelea Tabora, ijapokuwa gharama na muda wa kwenda huko kuliwazuia kuweza kwenda huko kila mara isipokuwa kwa mara chache tu. Kwa kupitia kwao, alijua kuhusu kukamatwa kwa mamia ya wengine Zanzibar na taarifa za mateso ya kutisha.

Mwezi Machi 1973, makada wote wa Chama cha Umma, pamoja na Babu walihamishiwa katika gereza ovu la ulinzi wa hali ya juu la Ukonga nje ya Dar es Salaam. Kwa mara nyengine tena waliwekwa katika chumba cha wale waliohukumiwa kifo. Mazingira katika gereza la Ukonga yalikuwa ni ya kukatisha tamaa kabisa na vile alivyotendewa Babu, aliyekuwa waziri, na makomred wake, wengine wakiwa maafisa wa jeshi wa vyeo vya juu haikuwa tofauti na vile walivyotendewa wahalifu wa kawaida
 
Labda kama wangelikuwa wameshtakiwa kwa kuitia nchi katika umasikini basi pengine wangelitendewa vizuri zaidi na Ukonga ingelikarabatiwa na kuwekwa vyumba maalumu vya Watu Muhimu Sana, kama ilivyokuwa mwaka 2008 wakati wa matayarisho ya kesi ya waliokuwa mawaziri na watumishi wa serikali walioshtakiwa kwa uporaji wa kiasi kikubwa cha fedha (Jamiiforum, 2008).
 
Ilikuwa katika kipindi hiki ambapo Jumbe na Hassan Nassor Moyo, waziri wa nchi wa Zanzibar walipofika bara na kumwona Nyerere ili awaruhusu maofisa wanaosaili kutoka Zanzibar wafanye upelelezi bara. Hashil Seif aliuelezea ‘upelelezi’ huo katika mazungumzo yaliyoandaliwa katika Mkutano wa Sita wa Waarabu na Wazungu juu ya Haki za Binadamu, Berlin tarehe 12 Mei, 2011:

 
Hashil alionyeshwa picha za waliowekwa kizuizini kutoka Zanzibar, wengi wao walikuwa wamemtaja baada ya kuteswa. Baadaye, wote wawili, yeye na Hamed walilazimishwa kutia saini maelezo ya kukiri na walipokataa mateso yalianza tena.
 
Mmoja baada ya mmoja, kila mtesaji alikuwa na zamu yake ya kunipiga kwa waya za umeme mpaka nilishindwa kusimama kabisa na kuanguka chini nikiwa nimezimia huku damu ikinichuruzika mwilini. Waliendelea kusema ‘utajua nini kilichomtoa kanga manyoya’. Waliyarudia maneno hayo wakati wakiendelea kunitesa, mengine mnaweza kufikiria wenyewe. Wakati wakinitesa, nilijihisi kama niliyezama ndani ya moto. Walinitaka nikae juu ya kiti, walinivua shati langu kwa hiyo nilikuwa tumbo wazi na walianza kunitesa mpaka nikapoteza fahamu na kuanguka sakafuni. (Maandishi ya mazungumzo katika Mkutano wa Sita wa Waarabu na Wazungu juu ya Haki za Binadamu, Berlin, tarehe 12 Mei, 2011)
 
Hashil alitishiwa kubakwa, na ijapokuwa watesaji hawakufikia hatua ya kufanya hivyo, au kumfanyia unyanyasaji wowote wa kijinsia, ubakaji wa wanaume ulikuwa ni jambo la kawaida katika mfumo wa mateso na vitisho vya serikali ya Zanzibar katika kipindi hiki na kilichofuata baadae. Kwa mfano, mwaka 2001 Napoli na Saleh wanaelezea juu ya kampeni endelevu ya kuwashambulia wanaharakati wapinzani ambapo ukatili wa kijinsia ulitumiwa dhidi ya wote wanawake na wanaume kisiwani Pemba (Napoli na Saleh, 2005: 167).

Hata hivyo, unyama wa watu waliopelekwa na serikali ya Zanzibar kumtesa Hashil ulishuhudiwa na wenzao wa bara, na hata maafisa usalama na wasaili hawa wakakamavu kutoka Dar es Salaam walishitushwa na kile walichokiona. Walimwarifu mkurugenzi wa usalama wa Taifa wa Tanzania na yeye alimpigia simu Nyerere na kumwelezea kwa urefu juu ya matukio haya akitilia mkazo kuwa kama utesaji huu haukusimamishwa waathiriwa wanaweza kufa.
 
Nyerere aliamrisha kuwa utesaji usimame. Akiwa amejaribu kuficha ukweIi juu ya kutiwa kwao gerezani kwa vyombo vya habari vya nchi za nje na wanadiplomasia, alitishika na uwezekano wa kumtaka aelezee juu ya vifo vya makada hawa wa kilichokuwa Chama cha Umma. Vile vile aliamrisha kuwa kuanzia wakati huo wapelelezi waliopatiwa mafunzo ndio pekee wawahoji walio kizuizini. Aliamrisha vile vile kuwa watesaji wakamatwe na waadhibiwe. Kwa hakika walitiwa ndani lakini kwa mujibu wa Hashil, ‘waliachiliwa baada ya wiki chache, wakati mimi nilirudishwa gerezani ambako nilitumia miaka sita ya maisha yangu’ (Mahojiano na Hashil Seif, 2012).
 
Ni wazi kuwa nia ya serikali ya Zanzibar ilikuwa ni kuwaweka watu hawa gerezani maisha. Kama Hamed alivyonambia:

Kuhoji kuliendelea lakini wapelelezi weledi kutoka bara hawakuweza kupata lolote la kumtia mtu hatiani. Kabla ya mauaji washtakiwa walikwenda kuvua samaki. Hapajakuwepo na silaha ndani ya mashua yao – isipokuwa chakula tu! Kila kitu kilionyesha kuwa hawakuwa na hatia lakini hilo halikuwa na umuhimu kwasababu wale waliokuwa madarakani walichodhamiria ilikuwa ni kuendesha kesi ya maonyesho ili kuwasingizia ubaya washtakiwa na kuonyesha kuwa kuanzia sasa na kuendelea, wapinzani wote watasagwasagwa kikatili.
======

hassan nassor moyo
 
Kesi Katika Mahakama Bandia ya Zanzibar
Wakati watu wakihojiwa na kuteswa bara, huko Zanzibar mambo yalikwishatayarishwa kwa ajili ya kesi ya kimaonyesho ya wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto iliyokuwa iendeshwe katika mahakama ya wananchi. Miezi michache kabla ya kesi hiyo vyombo vya habari na wananchi walitayarishwa kwa ajili ya kesi hiyo. Mkutano mkuu wa kwanza wa Chama cha ASP katika kipindi cha miaka kumi, uliofanyika mwezi Disemba 1972 chini ya uongozi wa Jumbe ulitamka kuwa itakuwa ndiyo kesi. Mbele ya Nyerere na viongozi wengine wa TANU waliokuwepo, yalipitishwa maazimio manne, kila azimio likithibitisha ajenda ya kibaguzi ya kikabila ya wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia yenye nia ya kulipiza kisasi.
 
  1. Maazimio mawili ya kwanza yalieleza kuwa wale wote waliokuwa wanachama wa vyama vya ZNP, ZPPP na Chama cha Umma Party watapigwa marufuku kushika nafasi yoyote katika serikali ya visiwani
  2. au kuwa wanachama kamili wa Chama cha ASP.
  3. Azimio la tatu liliwapiga marufuku wale wasiokuwa wanachama wa Chama cha ASP kufanyakazi katika polisi na jeshi, na
  4. la mwisho lilitaka iendeshwe kesi na kuuliwa hadharani wote wale watakaopatikana na hatia katika kile kinachotuhumiwa kuwa ni njama dhidi ya Karume:
 
Kesi
Kesi yenyewe hasa ilianza tarehe 5 Mei, 1973 takriban mwaka mmoja baada ya kamatakamata za kiholela. Miongoni mwa wale walioshitakiwa, 81 walishitakiwa kwa kosa la uhaini wakiwa ni pamoja na 18 waliowekwa kizuizini bara. Wakati Jumbe alijaribu kutaka 18 hawa, pamoja na Babu, warudishwe Zanzibar, Nyerere aliendelea kukataa kufanya hivyo labda kwasababu alihisi kuwa kufanya hivyo kungelizusha lawama na hasira za kimataifa. Matokeo yake, watu hawa walishitakiwa wakiwa wenyewe hawapo. Nyerere hakufanya lolote lile kuzuia kile ambacho kilikuwa sio tu kitendo cha ukiukwaji mkubwa wa haki bali pia ni kitendo batili kwasababu, kwa mujibu wa sheria za Tanzania kesi za kumuhukumu mtu wakati mwenyewe akiwa hayupo haziruhusiwi na pia kwasababu kumuhukumu mtu wakati mwenyewe akiwa hayupo kunaleta dhana kuwa mtu huyo amekataa kufika mahakamani.
 
Kitendo cha Nyerere cha kuchukua au kutochukua hatua kuhusu suala hili na kushindwa kwake kuwasimamia watu wasiokuwa na hatia kama ilivyokuwa katika mahusiano yake na Uingereza na Marekani kabla ya Muungano, kunaonyesha dhahiri hali yake ya kukosa ujasiri na kutokuwa na uwezo wa kuwa na msimamo thabiti dhidi ya shinikizo la wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia.

Kesi ilifanyika katika Mahakama za Wananchi za Zanzibar, Khamis anakumbuka:

 
Kwa wale walioshitakiwa wakiwa wenyewe hawapo, kesi hiyo ilikuwa ni zoezi la kuwapaka matope kwa kutumia hadithi za kubuni zilizorudiwa mara kwa mara. Kesi ilichukua takriban mwaka mmoja na kuchapishwa takriban katika magazeti yote nchini. Kama Babu alivyomwandikia mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.

 
Familia za washtakiwa tayari zilikuwa zikiteseka sana. Katika kila hali zilikumbana na shida za kiuchumi wakati watafutaji wao wa riziki wakiwa wamefungwa gerezani. Sasa, wakati kesi ikijikongoja, familia hizo ziliendelea kuishi katika hali ya uonevu na kupata maumivu ya ziada.

‘Ushahidi’ ambao Wolfgang Dourado, mwendesha mashtaka, aliuwasilisha dhidi ya washtakiwa unajieleza wenyewe. Ulikuwa ni ushahidi wa maelezo ya watu tisa waliokiri kosa na kuhukumiwa kifo na wakisubiri matokeo ya ombi la msamaha. Watu hawa waliambiwa kuwa kukiri kosa kutawahakikishia hukumu yenye tahafifu, ijapokuwa hilo lilidhihirika kuwa ni uongo. Maelezo yao yaliwataja washitakiwa wote isipokuwa sita tu. Zaidi ya maelezo hayo yalikuwepo maelezo ya wale waliokiri wenyewe ambayo yote yalikanwa na washitakiwa wote waliokamatwa visiwani na sita wengine ambao hawakutolewa ushahidi wowote. Katika kila hali, ‘ushahidi’ huu ulipatikana kwa njia za utesaji.
 
Ushahidi’ mwengine uliochukuliwa ulihusu mahusiano binafsi na ya kisiasa kati ya washtakiwa na Babu, uhusiano ambao hawakuukana. Mwisho ulikuwepo ushahidi usio na ithibati kuhusu mahali Babu na washitakiwa wengine walipokuwepo wakati wa mauaji:

 
Khamis aliniambia kuwa aliulizwa na Mwendesha Mashtaka Dourado “Unajua kuwa Marx alisema kwamba dini ni kasumba kwa watu?” Nilimwuliza, “Kwani mimi ninashtakiwa kwa kuwa mfuasi wa Marx au kwa mauaji ya rais?” Dourado alitaka kuwafurahisha Wamarekani.

Ama kwa Babu, mawazo yake ya kikomunisti ndiyo yaliyoitawala kesi yote. Alilaaniwa katika maelezo ya Dourado na kuitwa shetani mwenye umbo la binadamu. Kwa mfano, Dourado alieleza:

 
Babu na makomred wenzake wanataka kuanzisha sera gani Zanzibar? Uzito wote wa ushahidi unaonyesha kuwa walitaka kuanzisha usoshalisti wa kisayansi. Mashahidi kama Miraji Mpatani, Qullatein Badawi na mshtakiwa mwenza Ali Sultan (anayeonekana kuzielewa siasa zao) walieleza kuwa usoshalisti wa kisayansi ni ukomunisti … Kama kuna mtu anayemwelewa Babu basi yeye si mtu anayeweza kuheshimu matakwa ya umma. Akiwa kiongozi wa Chama cha Umma Party, alizungumzia juu ya chama ‘Kiongozi’. Hii ina maana kuwa kikundi cha madhalimu kujifanya kuwa ni masoshalisti wa kisayansi kulazimisha matakwa yao kwa umma. (Chase, 1976: 25 -7)
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…