Ni watu wachache sana ndiyo wanaopenda na wanafahamu umuhimu wa kusoma vitabu. Watu wengi hasa waafrika hawapendi kusoma vitabu ikiwa hakuna kinachowalazimisha kufanya hivyo kama vile mtihani, kazi, n.k.
Lengo kubwa linalowafanya waandishi wa vitabu kuandika vitabu ni kuweka maarifa yao kwenye maandishi. Hivyo kwa kusoma vitabu unapata maarifa mbalimbali yaliyowekwa kwenye kitabu husika.Hivi leo kuna vitabu vinavyohusu takriban kila kitu; kwa hiyo maarifa yoyote unayoyahitaji unaweza kuyapata kwenye vitabu.
Kwa hakika vitabu huongeza sana uwezo wa kufikiri. Unaposoma vitabu unafahamu mambo ambayo yatakufanya ufikiri zaidi; mara nyingine kitabu kitakuacha na maswali ambayo yatakufanya utafakari kwa kina zaidi juu ya mambo mbalimbali.
Vitabu ni burudani ya kipekee na ya gharama rahisi unayoweza kutembea nayo mahali popote. Viko vitabu mbalimbali tena vya bei rahisi ambavyo vinaweza kukuburudisha na kukufurahisha.
Maisha yana changamoto mbalimbali; hivyo utahitaji kitu cha kukuhamasisha kutoka hatua moja hadi nyingine. Kwa kusoma vitabu vya hamasa kuhusu maswala mbalimbali ya maisha utaweza kuhamasika zaidi.
Huwezi kuwa mwandishi bora kama husomi vitabu vya waandishi wengine bora.Ni lazima ujifunze namna waandishi wengine wanavyopanga mawazo, wanavyotumia lugha pamoja na mbinu nyingine za kiuandishi.
Vipo vitabu vingi vinavyotoa maarifa juu ya kuboresha afya yako. Kwa kusoma vitabu hivi utapata maarifa juu ya mambo unayoweza kufanya ili afya yako iwe salama na bora zaidi.
“Fikiri kabla ya kuzungumza. Soma kabla ya kufikiri.”Fran Lebowitz
Ni ukweli usiopingika kuwa Fran Lebowitz alifahamu wazi kuwa huwezi kuzungumza kabla ya kufikiri na huwezi kufikiri kabla ya kusoma. Kusoma kunakupa uwezo wa kufikiri na kujenga hoja zenye nguvu.Ikiwa unataka kuzungumza ili watu wakuamini na wakusikilize, basi soma vitabu kila mara.
Waandishi mbalimbali wa vitabu wamekuwa wakiwafundisha wasomaji wao njia za kuongeza kipato chao. Vipo vitabu vinavyofundisha juu ya mikakati ya uwekezaji pamoja na mbinu mbalimbali za kuongeza kipato.