Huwezi kufahamu vyema fursa zilizoko kwenye eneo fulani kama hutokwenda kwenye eneo hilo. Kwa njia ya kusafiri utaweza kuona fursa mbalimbali ambazo unaweza kuzifanyia kazi na ukajipatia kipato au ukaongeza kipato chako.
Hapa naikumbuka kampuni ya kitalii ya Bob Africa ambayo ilianzishwa na wanandoa wawili waliokuja Afrika kama watalii na baadaye wakaona fursa ya kuwekeza kwenye utalii.
Unaposafiri kwenda nchi nyingine inayozungumza lugha tofauti na ya kwako ni lazima ujifunze lugha ya nchi husika angalau kwa uchache.Hivyo, kwa njia hii utaongeza idadi ya lugha unazozifahamu na kuwa mwenye tija zaidi.
Faida nyingine ya kusafiri ni kupata mtazamo mpya tofauti na ule uliokuwa nao awali. Inawezekana kuna mambo ambayo huwa huyathamini uwapo nyumbani, lakini utayathamini uwapo safarini.
Inawezekana umepata likizo fupi au una muda fulani wa mapumziko kila baada ya kipindi fulani; badala ya kutumia muda wako kulala au kutazama televisheni siku nzima, unaweza kuutumia muda huo kwa kusafiri.
Msongo wa mawazo ni tatizo kubwa linalowatesa watu wengi kwenye dunia hii ya leo. Kwa njia ya kusafiri utaweza kuondoka kwenye mazingira au katikati ya watu wanaokufanya upate msongo wa mawazo.
Uwapo safarini utaweza kuona vitu vya kuvutia kama vile mazingira ya asili (mito, milima, mabonde, n.k.), wanyama pamoja na sanaa za eneo husika kama vile ngoma, maigizo, mavazi ya kitamaduni, n.k.
Hebu fikiri juu ya vyombo vya usafiri unavyovitumia, hoteli, viingilio utakavyolipa, n.k. Hivi vyote vinawapa kipato watu wengine na kuboresha maisha yao.