Kwa upande mwengine, Kenya kabla ya kupata uhuru wake tarehe 12 Disemba 1963, siku mbili baada ya uhuru wa Zanzibar, ilikuwa imegawanyika sehemu mbili: Koloni la Kenya, au bara, na Himaya ya Kenya, au Mwambao. Sheikh Abdillahi Nassir ni mmoja kati ya viongozi wa Mwambao ambaye alihudhuriya mkutano wa Mwambao uliofanyika Lancaster House, London, baina ya tarehe 8–12 Machi mwaka 1962.
Anaelezeya Sheikh Abdillahi kwenye kanda iitwayo “Mwambao: Historia ya Pwani ya Afrika Mashariki,” kuwa Himaya ya Kenya ilikuwa ni nchi kabla ya Koloni la Kenya kuwa ni nchi kwa miaka isiyopunguwa 1,300, na namna chuki za uzalendo wa Kiafrika zilivyowaathiri Waislam na khasa chuki za kikabila na propaganda ya utumwa na Uarabu
Sehemu hizo mbili za Kenya, Koloni la Kenya na Himaya ya Kenya au Mwambao, zikawa ni nchi moja ya Kenya kwa makubaliyano ya mabadilishano ya barua baina ya Waziri Mkuu wa Kenya, Mzee Jomo Kenyata na Waziri Mkuu wa Zanzibar Bwana Mohammed Shamte walizoandikiyana London tarehe 5 Oktoba 1963.