Watu wanaoishi karibu na mabonde ya Mto Amazon huko Amerika ya Kusini waliishi kwa kula muhogo kwa mamia ya miaka kabla ya mvumbuzi Christopher Columbus kusafiri huko.
Zao la muhogo ni maarufu sana duniani kote na hapa kwetu nchini Tanzania kwa sababu ni zao gumu linalovumilia ukame na kustawi vizuri bila ya uhitaji mkubwa wa mbolea ingawa hushambuliwa kwa urahisi na magonjwa yatokanayo na bakteria na virusi.
Wakazi wa kanda ya Ziwa Victoria nchini Tanzania wanafahamika sana kwa kula ugali unaandaliwa kutokana na unga wa zao la muohogo. Ni mojawapo ya vyakula maarufu sana katika mikoa ya Mwanza, Kagera, Kigoma, na Mara.
Katika maeneo mengine na hasa maeneo ya Ziwa Victoria, watu huvundika muhogo kabla ya kuutumia katika mfumo wa unga ufahamikao kwa jina maarufi la udaga.