Hawa wananchi siyo wajinga wa kubeba mapanga tu na kwenda kutishia mafundi. Ukiongea nao utagundua mengi sana. Pengine hayo mabomba hayana faida kwao. Pengine yanapita katika vyanzo vyao vya maji au sehemu takatifu za kabila lao. Au tu hawataki hayo maji na wana vyanzo vyao mbadala.
Kuna mtindo wa kudhani kuwa watu hawa wa vijijini ni wajinga na wasiostahili hata kushirikishwa katika maamuzi ya mambo yanayohusu maisha yao. Matokeo yake ndo haya. Unawatengenezea mabomba wanayaharibu kwa makusudi. Unaishia kusema watu hawa ni wajinga sababu hawajasoma. Unawapelekea vyandarua wanavigeuza nyavu za kuvulia samaki unabaki unaandika vipepa vyako ukiwalaumu jinsi wasivyopenda maendeleo. Unawalazimisha wachemshe maji ya kunywa kweli wanachemsha lakini hawayanywi. Unabakia kukuna kichwa. Unawapelekea chanjo ya Ebola wanakutoa mkuku kwa mapanga, uta na mishale...
Misaada na huduma za kweli ni lazima ziwe shirikishi. Kabla hujapeleka misaada au huduma zako, kaa chini uongee na walengwa. Kwa uwazi kabisa na uzingatie mapendekezo yao. Kufanya vinginevyo na kujaribu kuendeleza na kuhudumia watu kwa nguvu ni kupoteza muda. Wazungu watoa msaada kwa Afrika ndo wameanza kuligundua hili sasa. Kwamba Afrika kamwe haitaendelea kwa misaada kutoka nje bila kuwashirikisha walengwa hasa wa misaada hiyo; na hata kutafuta njia mbadala za jinsi ya kuitumia misaada hiyo kwa faida ya wote.