Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Je, unafahamu kuwa, kukaa kwa muda mrefu mahali pamoja ni hatari ya kwa afya yako? Shirika la Afya Ulimwenguni WHO linakadiria kuwa takribani watu milioni 3.2 kila mwaka hufariki dunia kwa sababu ya kukosa kufanya mazoezi. Tatizo hilo sasa linaukumba ulimwengu mzima.
 
Daktari Mounir Dia wa Senegal anasema kuwa: "Kuna viungo vingi vya mwilini ambavyo huathiriwa kwa kukosa kufanya mazoezi." Anaongeza kusema kuwa, "mtu asipoyafanya mazoezi, kuna uwezekano mkubwa wa mapigo ya moyo wake kuongezeka na ni rahisi kupata magonjwa ya moyo."
 
Massata ni mfanyabiashara jijini Dakar, mji mkuu wa taifa la Senegal. Anasema kuwa alianza kufanya mazoezi ili kuboresha hali yake ya afya. Uamuzi huo umebadilisha maisha yake. Anasema kuwa, miaka sita iliyopita alikumbwa na ugonjwa. Ugonjwa huo huathiri maini. "Nilikuwa nahisi maumivu mgongoni." Anasema Massata, huku akiwa ametulia.
 
Daktari alimfahamisha kufanyiwa uchunguzi kwenye figo zake. Kwa bahati nzuri, matokeo ya uchunguzi yalibainisha kuwa hakuwa na tatizo lolote kwenye figo zake. Kwa bahati mbaya uchunguzi uligundua kuwa alikuwa na mafuta kwenye maini yake.
 
Ugonjwa aliokuwa akiugua ni kuwa ini huzungukwa na mafuta. Mara nyingi watu wenye ugonjwa huo, huwa hawaoneshi dalili zozote.

Hadi kufikia sasa hakuna dawa au matibabu ambayo yamethibitishwa kuponya ugonjwa wenyewe. Hata hivyo mabadiliko ya tabia ya kula pamoja na mazoezi ya mara kwa mara ni dawa mjaarabu kwa mujibu wa matabibu.
 
Kabla nianze kufanya mazoezi, nilikuwa na uzani wa kilo 86, lakini sasa uzani wangu ni kilo 76. Mazoezi yalinasaidia kupoteza kilo 10 kwa kipindi cha miezi mitatu." Massata anasema huku akionekana akiridhishwa na hali yake sasa.

Anaafiki kuwa mazoezi yana nafasi kubwa sana maishani mwake sasa. Zamani hakuwa na muda alioutenga kwa ajili ya mazoezi lakini sasa anasema, "mimi hufanya mazoezi kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa.
 
Tangu agundue umuhimu wa kufanya mazoezi, Massata, hajawahi kuwa mvivu katika maisha mapya aliyoanza kuyaishi. "Hapa huwa ninakuja kufanya mazoezi kuanzia siku ya Jumatatu hadi Ijumaa, isipokuwa mwishoni mwa juma. Misuli inahitaji kupumzika ili ikue." Massata ananifahamisha huku akiwa kwenye eneo ambalo hufanyia mazoezi akiwa na nguo za mazoezi.
 
Baada ya mazungumzo, mara Massata ananifahamisha kuwa kocha wake kwa jina Lamine ndiye mwokozi wake. Bila Lamine hali yake ingekuwa mbaya mno. "Nazungumzia umuhimu wa kuwa na mahusiano mema." Massata ananifahamisha kisha anamuita kocha wake.
 
Kisha kocha wake anafika huku akiwa mwingi wa tabasamu, "wakati mwingine sikumuona akija kufanya mazoezi. Ukweli ni kuwa alikuwa anatibiwa hospitalini. Aliporejea mazoezini aliniambia alikuwa ana furaha kubwa." Lamine anasema, kisha anaendelea kuzungumza, "nilimuuliza, nini kilichofanyika?"
 
Massata alimkumbatia na kumfahamisha kuwa, amepona. Amepona kwa ukamilifu.

Shirika la Afya Ulimwenguni linapendekeza mazoezi ya dakika 30 kwa watu wazima na saa moja kwa watoto. Bila hivyo, inachukuliwa kuwa hufanyi mazoezi.

Hata hivyo daktari Dia anasema kuwa mazoezi ya kila siku humsaidia mtu kufidia muda ambao alikuwa ameketi kwa kipindi kirefu.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…