KUTOKA MLONGA ANZILA MPAKA MLOGANZILA!
Mloganzila si eneo ama jina geni kwa baadhi ya watu ingawa wengi wetu jina hili ni geni masikioni mwetu.
Mloganzila ni eneo kilipojengwa Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Muhimbili (MUHAS). Eneo hili lipo Kisarawe mkoa wa Pwani.
Picha inayoonekana si ya Ulaya bali ni moja ya majengo ya Chuo hicho kilichojengwa kwa msaada wa Serikali ya Korea Kusini.
Kona ya Wahenga tulipata nafasi ya kwenda kutembelea eneo hili na tulipenda kufahamu asili na maana ya neno Mloganzila. Tulikutana na Mzee mwenyeji wa eneo hili na alitueleza yafuatayo;
"Jina Mloganzila linatokana na uwepo wa Bwana mmoja miaka hiyooo ambaye wengi hatukumjua jina lake halisi mpaka alipofariki."
"Bwana huyu alikuwa pandikizi la mtu lililoshiba hasa, alikuwa na misuli iliyotokeza na mikononi mpaka miguuni. Alikuwa na vigimbi na kifua kipana kama Simba. Licha ya umbo hilo kama mbuyu Bwana huyu alikuwa mkimya na mpole sana, watu wengi tulimuogopa kwa kweli."
"Bwana huyu alikuwa akipenda sana kuimba na kuongea njiani akiwa peke yake huku ameweka shoka, jembe na panga lake begani. Alitembea mithili ya askari wapitao mbele ya Rais kutoa saluti."
"Kutokana na kile kitendo chake cha kuongea njiani ndipo sisi wazaramo kwa lugha yetu tukawa tunamuita " MLONGA ANZILA" tukimaanisha
"Msema njiani." Jina hili lilikuwa sana ikafika wakati hata watu wa Kibaha, Kiluvya,Kongowe na Mlandizi walimfahamu. Yaani ilikuwa ukiuliza tu kwa Mlonga Anzila hata mtoto mdogo alikuwa anakupeleka."
"Miaka ilivyosonga na kuingia kwa wazungu kulipelekea kubadilika kwa uhalisia wa jina hili. Wazungu walishindwa kutamka neno Mlonga Anzila na wakatamka Mloganzila. Athari hiyo iliendelea mpaka leo hii."
"Kwa hiyo vijana wangu hiyo ndiyo asili na maana ya neno Mloganzila. Ni matumaini yangu mmeridhika."
Kona ya Wahenga tunasema asante Babu kwa kutupatia asili na maana ya jina ama neno Mloganzila.
Tuendelee kujuzana.
